BENKI ya NMB kwa kushirikiana Kampuni ya Reliance Insuarance, wamezindua huduma mpya na ya kipekee ya bima, inayolenga kulipia gharama za matengenezo ya simu za mkononi za wateja wao wanaotumia huduma ya NMB Mkononi pale zinapoharibika.
Huduma hiyo iliyo chini ya mwamvuli wa BancAsuarance, inatambulika kama Muamala Wako, Bima Yako, ambako simu yenye NMB Mkononi, itakayotumia huduma hiyo angalau mara moja kwa mwezi, italipiwa gharama za matengenezo isiyozidi Sh. 500,000.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, alisema Muamala Wako, Bima Yako ni huduma inayoenda kufaidisha zaidi ya wateja milioni 3 wanaotumia huduma ya NMB Mkononi kote nchini.
Aliongeza kuwa, ubunifu wa kihuduma ni kipaumbele cha benki yake na kwamba wanaamini wateja wao wataifurahia sana bima hiyo na kwamba kutokana na kuongezeka kwa watumiaji wa simu za mkononi, wameona umuhimu wa kugusa mahitaji ya kila mteja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji (CEO) wa Reliance Insuarance, Ravi Shankar, aliliita tukio hilo la uzinduzi huo kuwa ni la kihistoria, huku akiwahakikisha wateja wa NMB Mkononi huduma bora na za haraka za malipo ya bima za matengenezo ya simu zao.
“Naipongeza NMB kwa ubunifu uliozaa huduma hii bora, ya aina yake, inayoenda kugusa moja kwa moja maisha ya mamilioni ya Watanzania wanaotumia NMB Mkononi, nasi kama washirika, tunaahidi kutokuwepo kwa ucheleweshaji wa malipo ya bima,” alisema Shankar.
“Kwa sasa Tanzania uchumi wake unakua kwa kasi, kundi la kipato cha kati linaongezeka maana yake wanaomiliki simu za mkononi nao wameongezeka. Hivyo, bidhaa hii ya bima ya simu ya mkononi ni kitu cha kipekee sana nawasifia NMB kwa kupata wazo kama hili ambalo litawagusa watu wengi,” alisema Shankar.
Alibainisha kuwa, anaamini hata utaratibu wa malipo kwa watakaopata majanga ya simu zao utakua wa uhakika kwa kuwa Reliance Insurance na Benki ya NMB wanasifika kwa kulipa wateja wao kwa wakati wanapopata majanga kupitia bima zao.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Sheria wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA), Emily Kiria, alizipongeza NMB na Reliance Insuarance kwa huduma hiyo, aliyosema inaunga mkono jitihada za Serikali kupitia mamlaka yake ya kuongeza uelewa na matumizi ya bima miongoni mwa Watanzania.
“Huduma hii inaenda kuongeza nguvu katika mpango mkakati wa Serikali wa kuongeza idadi ya Watanzania wenye uelewa wa masuala ya bima kutoka asilimia 36 ya sasa hadi kufikia asilimia 80 ya wenye uelewa na asilimia 50 ya watumiaji wa bima hizo.
“TIRA tunazipongeza NMB na Reliance Insuarance kwa ushirika wao huu. Uaminfu wa Reliance katika ulipaji wa bima na ubora wa kihuduma wa NMB, unatupa uhakika wa huduma bora itakayomaliza changamoto ya malalamiko ya wateja katika Sekta ya Bima,” alisema Kiria.
Kupitia Muamala Wako, Bima Yako, watumiaji wa simu wenye huduma ya NMB Mkononi watakaoharibikiwa simu zao kwa namna yoyote ile, watanufaika na malipo ya matengenezo yatakayofanyika kwa mafundi wanaotambulika na TRA ndani ya siku 1 hadi 10.
No comments:
Post a Comment