WANANCHI WAOMBA DARAJA LA MUDA BAADA YA WATU WANNE KUZAMA MTONI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 28 February 2021

WANANCHI WAOMBA DARAJA LA MUDA BAADA YA WATU WANNE KUZAMA MTONI

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipofika katika mto momba uliozamisha kinamama wawili na watoto wao wawili kufanya tathmini ya namna ya kutafuta njia mbadala kwa wananchi mara baada ya kusikia mkasa huo uliotokea tarehe 24.2.2021 na kufika hapo tarehe 25.2.2021. 



Baadhi ya Wataalamu na Watumishi wa Serikali wakisukuma gari ya mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (kaunda suti ya kijivu) iliyokwama karibu na Kijiji cha Tululu mara tu baada ya kutoka katika kijiji hicho.

WANAWAKE wawili pamoja na watoto wakiwa migongoni mwao wa Kijiji cha Tululu, Kata ya Kaoze, Bonde la Ziwa Rukwa Wilayani Sumbawanga wanasadikiwa kuzama katika mto momba na kufariki baada ya mtumbwi waliokuwa wamepanda kushindwa kuhimili kasi ya maji ya mto huo na kusababisha kupinduka kwa mtumbwi huo.

Kina mama hao ambao walikuwa wakitoka ng’ambo ya mto huo unaotenganisha Mikoa ya Rukwa na Songwe kufuata huduma mbalimbali zikiwemo za afya walipatwa na kadhia hiyo wakiwa Pamoja na wananchi wengine watatu ambao walipona baada ya kupata msaada wa kuokolewa baada ya Mwenyekiti wa Kijiji kufika eneo la tukio hilo.


Akielezea kwa kwa ufupi mkasa huo uliotokea tarehe 24.2.2021 Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Tululu Frank Simon alisema kuwa walipata taarifa ya kadhia hiyo wakati wakijiandaa kwa mkutano wa Kijiji ndipo walifika kwenye eneo hilo na kukutana na mtoto wa umri wa miaka mitano aliyekuwa akilia akiwa majini karibu na ukingo wa mto huku akiwa ameshika kichwa cha mtumbwi uliokuwa umezama.


“Kama mimi Mwenyekiti kwa uchungu uliokuwepo sikupata muda wa kufikiria, nilitumbukia kwenye maji, nikaogelea hadi kumwokoa mtoto yule, na kuanza kumhoji na kujua idadi ya watu waliotumbukia kwenye mto kuwa ni watu sit ana dereva wa Saba, tukarudi tena kuhangaika na kumpata kijana mwenye umri wa miaka 19, tukamuokoa, tumejitahidi kuitafuta miili hiyo lakini mpaka hivi sasa haijapatikana, lakini tulitoa taarifa, ofisi yaka, kituo cha polisi, ofisi ya tarafa Pamoja na Kijiji cha jirani, Kijiji cha Mkulwe, kata ya Mkulwe, Tarafa ya Kamsamba, Wilaya ya Momba, Mkani Songwe,” Alisema.


Aidha alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kuwatafutia ufumbuzi wananchi wa Kijiji hicho kwa kuwapatia daraja la dharura ili wananchi hao waepukane na majanga hayo na kuwasadidia kumalizia zahanati yao ambayo imefikia usawa wa linta kwa nguvu za wananchi wa kaya 276 za Kijiji hicho.

Naye Diwani wa Kata ya Kaoze Gidion Fungameza alisema kuwa changamoto kubwa ya wananchi wa Kijiji hicho ni kutokuwa na zahanati hali inayowafanya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya kwa kuzingatia kuwa barabara kutokuwa nzuri hasa katika kipindi hiki wakati mvua zikiendelea kunyesha.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Apolinary Macheta alisema kuwa miongoni mwa miradi walioipitisha katika vikao vya bajeti ya halmashauri hiyo ni Pamoja na ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Kaoze.


“Kwa kutumia mapato ya ndani tumeamua tuhakikishe tunakamilisha kituo cha afya kimoja, na moja ya kituo ambacho tumekipitisha kwenye baraza, ni kituo cha afya cha kata ya Kaoze, kwahiyo jambo hili la kufuata huduma mbali kwaajili ya kituo cha afya, tutakapokuwa tumekamilisha kama bunge litapitisha bajetihii kama tulivyokuwa tumeomba, ndio kituo cha afya cha Kaoze kitatusaidia kusogeza huduma za afya kwa watu wa kapenta na kipeta,” Alisema.


Pamoja na hayo Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule aliushukuru uongozi wa Kijiji hicho kwa ushirikiano walioutoa kwa serikali katika kusaidiana kuwatafuta watu hao waliozama ambapo alisema kuwa baada tu ya kupata taarifa hiyo alihakikisha jeshi la Zimamoto na uokoaji wanafika katika eneo hilo na kutoa msaada.


“Pamoja na hilo, niwashukuru sana hasa wale waliojitolea kutumbukia mule kwenye mto kuwatafuta, nimeambiwa sasa hivi mmehamia pale kirando (Kijiji cha jirani), tunawaomba vijana wote pale mtakapohitajika na uongozi wa Kijiji au wa kata, basi mjitolee ili tuweze kuwatafuta hawa wenzetu mpaka tuwapate,” Alisema.


Dkt. Khalfan Aliongeza kuwa huduma muhimu zinapatikana katika Kijiji cha Kipeta ambacho hakifikiki kutoka kijijini hapo kutokana na kukosekana kwa barabara yenye km 14 inayounganisha Kijiji hicho cha Kipeta na Kijiji cha Tululu.


Wakati akitoa salamu zake za rambirambi kwa wanakijiji wa Tululu Mh. Wangabo alimuagiza Mkurugezi wa halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa zahanati iliyoanza kujengwa na wananchi wa Kijiji hicho inamalizika ndani ya mwaka huu wa 2021 na aidha alimuagiza Mratibu wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha wanafanya matengenezo ya dharura katika barabara ambazo zipo kwenye hatari ya kuwakosesha wananchi mawasiliano na maeneo muhimu wanayofuata huduma za kijamii.


“Fedha zilizotengwa kwa mwaka 2021/2022 ni lazima iwekwe kwenye dharura, maeneo haya yanashida nyingi, barabara huku haipitiki, wakienda kuvuka mto wanaliwa na mamba, wanatumbukia, mitumbwi inabinuka na watu wanakufa, sasa hawa watu wakimbilie wapi? huko hewani? Ni lazima tutatue matatizo hapa ardhini kwenye barabara yetu lakini pia kwenye zahanati na tatu kwenye mto, hay ani maeneo makuu matatu ambayo ndio msingi wa matatizo makubwa ya Kijiji hiki na vingine na kata hizi mbili,” Alisema.

No comments:

Post a Comment