Na Dotto Mwaibale
WANAMUZIKI Maarufu Nchini Stara Thomas na Hafsa Kazinja ni miongoni mwa baadhi ya wanamuziki watakao pata kadi za bima ya afya ya Taifa (NHIF) zitakazotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa.
Bashungwa ambaye atakuwa mgeni rasmi atatoa kadi hizo katika Kongamano la Fursa kwa wanamuziki litakalofanyika Februari 20, 2021 Jijini Arusha.
"Mastaa hawa Stara Thomas na Hafsa Kazinja tayari wametimiza vigezo vya kupata kadi hizo za bima ya afya baada ya kukutana na Rais wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), Eric Kisanga na Katibu Mkuu wa umoja huo, Stella Joel ambao ndiyo waandaaji wa kongamano hilo.
Akiwazungumzia Wanamuziki hao Katibu Mkuu wa TAMiUFO Stella Joel alisema wanaishukuru Serikali kwa kuwakumbuka kuwapatia kadi hizo ambazo zitawasaidia kupata vipimo na matibabu katika hospitali za Serikali na binafsi.
Joel alisema kabla ya hapo wanamuziki wengi wamekuwa wakipoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za vipimo na matibabu.
"Kwa hatua hii iliyochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano hakika wanamuziki wote tunakila sababu ya kuipongeza kwa kutekeleza ahadi yake kwa vitendo ya kutusaidia wasanii" alisema Joel.
Rais wa TAMUFO, Eric Kisanga alisema kongamano hilo ni la kipekee kwani litawahusisha wanamuziki wa kada zote na kuwa maandalizi yote yamekwisha kamilika.
"Maandalizi yote ya kongamano letu ili la fursa kwa wanamuziki yamekwisha kamilika kwa asilimia kubwa na sasa tupo kumalizia mambo madogo yaliyosalia," alisema Kisanga.
No comments:
Post a Comment