SERIKALI YATOA ONYO KWA MSIMAMIZI WA UJENZI WA SOKO LA KIMKAKATI MWANZA KWA KUCHELEWESHA KAZI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 9 January 2021

SERIKALI YATOA ONYO KWA MSIMAMIZI WA UJENZI WA SOKO LA KIMKAKATI MWANZA KWA KUCHELEWESHA KAZI

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb), (katikati) akisikiliza maelezo ya Mkandarasi wa Ujenzi wa Soko la Kisasa la Mjini Kati Wilayani Nyamagana, Mhandisi Taher Jafferji, kuhusu changamoto ya upatikanaji wa Saruji, jambo lililosababisha ujenzi wa Soko hilo kukamilika kwa asilimia 8.

Moja ya jengo lililopo katika mradi wa Soko la Kisasa la Kimkakati la Mjini Kati Wilayani Nyamagana, Mwanza.

5.

Na Peter Haule na Farida Ramadhani, Mwanza

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis, amemwagiza Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa Soko la Kisasa la Mjini Kati Jijini Mwanza  kuwepo eneo la ujenzi muda wote ili mradi huo ukamilike kwa wakati.


Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis, ametoa maagizo hayo alipotembelea na kukagua ujenzi wa Soko hilo pamoja na Kituo cha Mabasi cha Kisasa cha Nyegezi kilichoko Wilaya ya Nyamagana jijini humo.


“Nimepata taarifa kwamba msimamizi mmoja anasimamia miradi yote miwili jambo ambalo halikubaliki na linasababisha miradi hii kuchelewa na kuna hatari itatekelezwa chini ya kiwango kutokana na kukosa usimamizi makini,” Alisema Mhe. Mwanaidi.


Alisema kuwa nilazima msimamizi huyo awepo eneo la ujenzi saa 24 kuangalia ufanisi wa kazi ili kupata majengo na miundombinu imara itakayosadifu juhudi za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, za kujenga miundombinu bora itakayochochea maendeleo ya wananchi kwa ujumla.


“Kama msimamizi hakai eneo la ujenzi basi aondolewe awaachie wengine ambao wanaweza kufanya kazi hiyo, iwapo msimamizi hayupo ni vema Serikali ikajulishwa ili iweze kuchukua hatua stahiki bila kuchelewesha miradi”, alieleza Mhe. Mwanaidi Ali Khamis.


Aidha Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ametoa siku mbili kwa uongozi wa Wilaya ya Nyamagana kuhakikisha changamoto ya uhaba wa saruji katika miradi hiyo miwili ya kimkakati inayopewa fedha na Hazina ili kuziwezesha halmashauri kujitegemea kimapato, inatatuliwa haraka.


Awali Mkandarasi kutoka Kampuni ya Mohamemedi Builderrs anayejenga miradi hiyo, Mhandisi Taher Jafferji, alilalamikia changamoto ya upatikanaji wa Saruji licha ya kulipa fedha nyingi kwenye viwanda vya Saruji, jambo ambalo linapunguza kasi ya ujenzi.


Alisema kuwa, amepewa mkataba wa ujenzi wa miezi 18 ambapo anatarajiwa kukamilisha ujenzi wa Soko hilo Aprili, 2022, hivyo ni vema Serikali ikalitafutia ufumbuzi suala hilo kwa kuwa yeye anamorali wa kazi na ni mzalendo wa kweli.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Phillis Nyimbi, amesema kuwa uongozi wa Wilaya hiyo utahakikisha maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango yatatekelezwa kikamilifu, kwa kuwa lengo lao ni miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuchangia maendeleo ya Jiji na Mwanza na kutatua changamoto ya ajira kwa wananchi.


Naye Mkurugenzi wa Wilaya ya Nyamagana Bw. Kiomoni Kibamba alisema kuwa  mradi wa ujenzi wa Soko la kisasa la Mjini Kati utagharimu shilingi bilioni 20.7 wakati Ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha cha Nyegezi kitagharimu shilingi bilioni 15.8 ambapo ujenzi wa soko umefikia asilimia 8 na ujenzi wa Kituo cha mabasi umefikia asilimia 10 ambapo Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imetoa kiasi cha shilingi bilioni 7.13.

No comments:

Post a Comment