Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji akiapishwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi. |
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwaapisha baadhi ya viongozi hao. |
Na Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemuapisha Mhandisi Zena Ahmed Said kuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na katibu Mkuu Kiongozi, akichukua nafasi ya Dk. Abdulhamid Yahya mzee aliestaafu.
Hafla hiyo ya kiapo imefanyika Ikulu Jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na na Viongozi mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Mawaziri, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Dk. Abdulhamid Yahya Mzee pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid.
Wengine ni pamoja na Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Askofu Dickson kaganga, Wakuu wa Vikosi vya SMZ pamoja na wanafamilia.
Rais Dk. Mwinyi amemuapisha kiongozi huyo kushika wadhifa huo baada ya kumteua January mosi mwaka huu, kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 49 (1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Kabla ya uteuzi huo Mhandisi Zena Ahmed Said alikuwa Katibu mkuu Wizara ya Nishati katika Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika hatua nyengine, akizungumza na vyombo vya habari, Mhandisi Zena alisema atajitahidi kufanya kazi zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliopo ili kufikia matarajio ya Wazanzibari.
Alisema atafuata kanuni na sheria na kujiongeza katika ubunifu ili aweze kufikia malengo, huku akiahidi Serikali kuangalia kwa undani umuhimu wa ajira kwa vijana.
Aidha alitowa wito kwa wanawake nchini kote kujiamini na kufanya kazi zao kwa weledi pamoja na kuwataka kufanya shughuli zao kwa kuzingatia wakati na nafasi zao, sambamba na kutosubiri kusaidiwa.
Mhandisi Zena Ahmed Said, anakuwa mwanamke wa kwanza nchini kushika wadhifa wa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, tangu Mapinduzi ya 1964.
No comments:
Post a Comment