NDUGULILE ATOA ONYO KWA WATOA HUDUMA ZA MAWASILIANO KUVUJISHA TAARIFA BINAFSI ZA WATEJA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 26 January 2021

NDUGULILE ATOA ONYO KWA WATOA HUDUMA ZA MAWASILIANO KUVUJISHA TAARIFA BINAFSI ZA WATEJA

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (katikati mwenye suti ya bluu) akishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa kupeleka mawasiliano vijijini baina ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mtendaji Mkuu Justina Mashiba na Kampuni ya simu ya Tigo, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma. Kulia kwake ni Naibu wake Mhandisi Andrea Kundo, wa pili kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula na wa pili kushoto ni Naibu wake dkt Jim Yonazi.


Na Faraja Mpina -WMTH

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe, Dkt. Faustine Ndugulile ametoa onyo kwa watoa huduma za mawasiliano nchini kuacha tabia ya kuvujisha taarifa binafsi za wateja kwa kuwadhibiti baadhi ya watumishi wao wasio waaminifu.


Ndugulile amebainisha hayo wakati akizungumza na watoa huduma za mawasiliano katika hafla ya kutia saini Mkataba baina yao na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wa kupeleka huduma za mawasiliano katika vijiji 173 vilivyo katika mikoa 16 nchini.


Amesema kuwa hapendezwi na tabia ya baadhi ya watumishi wa makampuni hayo kuchapisha taarifa binafsi za wateja na kuzitoa kwa wagomvi wao na kwa watu wasio na nia njema.


“Niwaombe sana makampuni ya simu, someni vizuri sheria, vyombo vya dola ndivyo vinavyoruhusiwa kupata taarifa binafsi za mteja kwa malengo mahsusi na sio vinginevyo”, alisisitiza Ndugulile


Ameongeza kuwa suala hilo atalisimamia kwa umuhimu wake na kampuni ya simu itakayotolewa malalamiko na wananchi kwa kuvujisha taarifa zao, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya kampuni husika.


Kwa upande wa Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Andrea Kundo ametoa rai kwa watoa huduma za mawasiliano kuwa watafiti na wabunifu kwa kufanya uwekezaji kwa kutumia teknolojia nyepesi itakayowezesha mawasiliano ya uhakika kwa wananchi.


Aidha Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko huo imetoa ruzuku ya kiasi cha shilingi Bilioni 6 za kitanzania kwa makampuni ya simu ya Airtel, Vodacom na Tigo na kusaini Mkataba wa kupeleka mawasiliano katika vijiji 173 ifikapo Oktoba 2021.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari


No comments:

Post a Comment