DK. HUSSEIN MWINYI APUNGUZA SHAMRA SHAMRA MAADHIMISHO YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 12 January 2021

DK. HUSSEIN MWINYI APUNGUZA SHAMRA SHAMRA MAADHIMISHO YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imelazimika kupunguza baadhi ya shamra shamra za maadhimisho ya kusherehekea miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ili kuokoa fedha na kuzielekeza katika matumizi mengine ya serikali, ikiwemo huduma za kijamii.


Dk. Mwinyi amesema hayo katika kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizofanyika leo katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini hapa. Amesema Serikali ilikuwa na azma ya kuzipamba sherehe hizo kwa shamra shamra mbali mbali kama ilivyozoeleka na Wazanzibari wote, lakini kutokana na hali ya uchumi, sherehe hizo zimetekelezwa kwa njia tofauti na ilivyozoeleka.


Alisema hali ya uchumi wa Dunia imeyumba sana kutokana na madhara ya ugonjwa wa COVID 19, hivyo kuilazimu Serikali kutumia fedha za sherehe hizo katika kufidia mapengo ya wajibu kwa wananchi, ikiwemo huduma za elimu, afya na nyenginezo.


Alieleza kuwa hali hiyo ni ya mpito na kubainisha kawa pale itakapotengemaa (katika siku za usoni), utaratibu wa kawaida wA maadhimisho ya sherehe hizo utarejea. Dk. Mwinyi alisisitiza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuendelea kuyalinda Mapinduzi ya 1964 katika msukumo mpya wa kiuchumi. Alisema wakati umefika kwa Wazanzibari kujikita katika Uchumi wa Buluu, kwa kuzingatia shabaha ya Mapinduzi hayo ambayo ni kustawisha maisha ya wananchi wake.


Aidha, alisema Wazanzibari wanapaswa kupata huduma bora na stahili, ikiwemo elimu, afya na maji na kwa wale watakaohitaji kufanya biashara waweze kufanya shughuli zao bila kiuzuizi wala vikwazo vitokanavyo na rushwa. Alisema Mapinduzi ya kiuchumi ndio mapinduzi yatakayotoa majibu ya changamoto ziliopo na vizazi vijavyo. 


“Tunapaswa kuleta Mapinduzi katika sekta za Uvuvi ili wavuvi wetu wavue kwa zana za kisasa na tuweze kufaidika na rasilimali za bahari kuu, tunapaswa kuleta Mapinduzi katika kilimo ili wakulima  wetu waongeze tija na kutuondolea utegemezi wa chakula kutoka nje pamoja na kuinua zao la karafuu na Mwani”, alisema.


Alisema Wazanzibari wanahitaji Mapinduzi katika sheria na taasisi ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila bughudha wala vikwazo pamoja na kuwepo Mapinduzi katika Sanaa na Michezo  ili kila mmoja aweze kutumia uwezo na kipaji chake kucheza na kujiendeleza kimaisha.


Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alisema Mapinduzi yanayohitajika yatawezekana endapo mambo tofauti yatatekelezwa, ikiwemo kuufungua Uchumi kwa kuweka mazingira mazuri.

Alisema ni azma ya serikali anayoiongoza kuvutia Wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kuendeleeza uchumi wa buluu.


“Lengo ni kufungamanisha sekta za uvuvi, utalii na uchukuzi kwa kupanua shughuli za Utalii ikiwemo uwekezaji wa Utalii kisiwani Pemba, kujenga Bandari mpya za Mangapwani na Maruhubi ili kuwawezesha wavuvi wetu kuvua kisasa zaidi ikiwemo uwekezaji wa Uvuvi wa Bahari kuu”, alisema.


Aidha, alisema eneo jengine linalohitaji Mapinduzi ni kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa kodi mbali mbali. Alisema hatua hiyo italiwezesha Taifa kuendelea sambamba na kumudu kupanua wigo katika utoaji wa huduma za kijamii kama vile  afya, elimu na  nyenginezo, ikizingatiwa kuwa hivi sasa ahuuduma hizo zinaztolewa bure na serikali.


Alieleza  suala la umoja wa kitaifa ni nguzo muhimu katika ujenzi wa Zanzibar mpya na  kusema ndio sababu zilizomsukuma kuchukua hatua za haraka katika kujenga maridhiano ya umoja wa kitaifa. 


Alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 toleo la 2010 lililobainisha haja ya kundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa hapa nchini, hivyo akawataka Viongozi kufanya kazi ya kuyatafsiri maridhiano hayo ili kuwaletea neema Wazanzibari.


Akigusia changamoto ya vitrndo vya Unyanyasaji wa Kijinsia unaolikabili taifa, Dk. Mwinyi alisema jambo hilo linafedhehesha sana na kuchafua taswira ya Zanzibar.


Alisema katika kulikabili jambo hilo, kilio chawananchi kimeelekezwa kwa vyombo vya husika kwa kushindwa kuchukua hatua pale taarifa zinapotolewa pamoja na baadhi ya wazazi na ndugu kuyamaliza masuala hayo kifamilia kwa kile kinachodaiwa kuficha aibu na kunusuru udugu.


Alitoa wito wa kukomeshwa vitendo hivyo mara moja pamoja na kuagiza kuwachukulia hatua za kisheria watu wote watakaopatikana huhusika na vitendo hivyo bila kuzingatia uhusiano uliopo ama uzawa.


Alisema kushindwa kuwachukulia hatua wahalifu wa matukio ya udhalilishaji ni kuwasaliti watoto wa Zanzibar ambapo Serikali ina wajibu wa kuwalinda. Rais Dk. Mwinyi, akasisitiza umuhimu wa kuhifadhi ‘Mali Kale’ , akibainisha kuwa ni urithi muhimu katika Historia ya Taifa hili.


“Sote tumesikitishwa kwa tukio la kuangauka sehemu ya jengo la Kihistoria la Beit el Ajaib ambalo lilikuwa katika ukarabati, naungana na Wanzazibari wote na kutoa pole kwa ndugu na jamaa wa wananchi wawili waliopoteza maisha”, alisema.


Alieleza kuwa kuanguka kwa jengo hilo kunawakumbushwa Wazanzibari umuhimu wa kuyakarabati mara kwa mara majengo yaliopo Mji Mkongwe, ikiwa ndio alama ya Zanzibar.


Aidha, Dk. Mwinyi aliwashkuru Viongozi, Wapiganaji wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, watumishi, waandishi wa habari  na wananachi kwa kufanikisha  vyema sherehe hizo pamoja na kutumia fursa hiyo kuwataka wananchi hao kuwaombea dua Maehemu wote waliotoa maisha yao katika Ukombozi wa taifa lao.


Mapema, Mwenyekiti wa Kmaati ya sherehe ambae pia ni Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla alisema Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 yalikuwa na lengo la kumkomboa Mzanzibari kutokana na dhuluma za  kutawaliwa.


Alisema  maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, yamehusisha matukio mbali mbali ikiwemo usafi wa  mazingira, ufunguzi na uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi mbali mbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 46.1.


Aidha, alisema kulifanyika mazoezi ya viungo, Tamasha la Biashara, upigaji wa Fash-fash pamoja na kufanyika michezo mbali mbali ikiwemo Kombe la Mapinduzi.


Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha miradi mitatu iliowekewa mawe ya msingi inakamilika kwa ufanisi mkubwa, ili kuweza kutoa huduma bora kwa jamii.


Alitoa shukurani kwa wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika sherehe hizo, sambamba na kwenye matukio ya uwekeaji mawe ya msingi, hatua aliyosema inabainisha utayari walionao katika kuendeleea kuyalinda Mapinduzi hayo.


Sherehe hizo zilihudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Rais mstaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  Ali Hassan Mwinyi pamoja Marais wastaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohamed Shein.


Wengine ni  Viongozi wakuu wa Kitaifa kutoka Serikali ya Jamuhuri ya Muuungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wake wa Viongozi wakuu wastaafu wa SMT na SMZ, Mabalozi wadogo wa  nchi mbali mbali waliopo Zanzibar, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Wakuu wa Mikoa ya Zanzibar, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Mawaziri, Viongozi wa Vyama vya Siasa,Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama.


Aidha, sherehe hizo zilipambwa kwa maonyesho mbali mbali, ikiwemo maandamano yalioongozwa na Kikundi cha Bendi ya Chipukizi, Vijana wa makundi mbali mbali, wananachi kutoka mikoa mitano ya Unguja na Pemba, Skauti pamoja na vijana wa Chipukizi.


Vile vile , kuliwepo maonyesho ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama, vilivyoshirikisha JWTZ, Polisi, Uhamiaji, KMKM, Mafunzo, JKU pamoja na KVZ  ambapo kwa njia tatu tofauti walitembea (root much) kutoka Kambi ya JWTZ Mtoni hadi Ziwani Polisi na hatimae kupita mbele ya Mgeni rasmi na kutoa heshima, sambamba na kuwepo maonyesho ya ‘Showforce’, ambapo magari na vifaa mbali mbali vinavyotumiwa na wapiganaji hao vilipita mbele ya mgeni rasmi Dk. Hussein Mwinyi.


No comments:

Post a Comment