DK CHAULA AONGOZA WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI KUANDAA MPANGO MKAKATI WA UTENDAJI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 20 January 2021

DK CHAULA AONGOZA WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI KUANDAA MPANGO MKAKATI WA UTENDAJI

Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Zainab Chaula akizungumza na Menejimenti, maafisa, wawakilishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora (hawapo pichani) wanaofanya kazi ya kuandaa Mpango Mkakati wa Utendaji kazi na ufuatiliaji wa Wizara hiyo katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma. 


Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti, maafisa na wawakilishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainab Chaula (hayupo pichani) kabla ya kuanza kazi ya kuandaa Mpango Mkakati wa Utendaji kazi na ufuatiliaji wa Wizara hiyo katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.

Na Faraja Mpina, Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Zainab Chaula ameongoza Menejimenti, maafisa waandamizi na wawakilishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kuandaa Mpango Mkakati wa utendaji kazi na ufuatiliaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, kazi itakayofanyika kwa siku 12 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma.


Dkt Chaula amesema kuwa maandalizi ya kuandaa Mpango huo yalikuwa yamekwishafanyika  lakini msukumo mkubwa umetokana na kuundwa kwa Wizara mpya ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari yanayoenda sambamba na mabadiliko ya kimuundo kulingana na mahitaji ya Wizara pamoja na kuongeza uwajibikaji wenye matokeo chanya.


“Mpango Mkakati huu tunaouandaa utarahisisha kupima utendaji wetu kama Wizara katika kufikia malengo, kujua  mchango halisi wa Wizara katika kuinua pato la Taifa na kujua maeneo ambayo Wizara imechangia pato hilo “, alizungumza Dkt Chaula


Ameongeza kuwa kazi ya kuandaa mpango huo inahitaji ushirikishaji, umakini na utulivu mkubwa ili kupata Mpango Mkakati bora, wenye viwango na wenye muda wa utekelezaji unaopimika na kusisitiza Mpango huo uwe  katika lugha ya Kiingereza  na Kiswahili.


Naye mwezeshaji wa kuandaa Mkakati huo Beltila Mgaya kutoka Ofisi Ya Rais Utumishi na Utawala Bora, amempongeza na kumshukuru Dkt Chaula kwa kushiriki na kuipa kipaumbele kazi hiyo ambayo baadhi ya Watendaji Wakuu wa Sekta ya umma huwa hawashiriki kwa karibu.


Ameongeza kuwa kazi hiyo itafanyika kwa siku 12 ambapo siku 6 za mwanzo ni uandaaji wa  Mpango Mkakati wa Wizara na kuanzia siku ya 7 hadi 12 ni uandaaji wa Mpango wa ufuatiliaji wa Mpango huo, na kusisitiza kufanya kazi kwa bidii na ufanisi kwasababu kila siku ina kipengele cha kufanyia kazi. 


Kwa upande wa Jane Kaji mwezeshaji kutoka Ofisi Ya Rais Utumishi na Utawala Bora amesema kuwa Mpango Mkakati wa Utendaji Kazi na Ufuatiliaji ni mfumo wa Utendaji kazi ambao unatoa mwongozo kwa watumishi wa umma katika kutoa huduma bora kwa jamii, uwazi na uwajibikaji.


Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WMTH)



No comments:

Post a Comment