AWESO AAGIZA MRADI WA MAJI KYAKA BUNAZI KUKAMILIKA KWA WAKATI KAMA ALIVYOELEKEZA RAIS MAGUFULI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 27 January 2021

AWESO AAGIZA MRADI WA MAJI KYAKA BUNAZI KUKAMILIKA KWA WAKATI KAMA ALIVYOELEKEZA RAIS MAGUFULI

Waziri  wa Maji Mhe. Jumaa Aweso akipanda juu ya kusalimiana na mafundi wanaojenga mtambo wa kutibia maji unaonedelea kujengwa kwenye kilima cha kijiji cha kituntu  kata ya Kyaka ambapo mradi wa maji Kyaka Bunazi unajengwa.


Na Allawi Kaboyo –Missenyi

WAZIRI wa maji Jumaa Aweso amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji Kyaka Bunazi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa muda ambao umepangwa kwa mujibu wa mkataba na kusisitiza kuwa hakutokuwa na muda wa nyongeza kwenye mradi huo.

Mhe. Aweso ametoa maagizo hayo January 26, mwaka huu alipotembelea mradi huo ili kujionea maendeleo yake akiwa ameambatana na naibu katibu mkuu mhandisi Nadhifa Kemikimba, ambapo mradi huo unajengwa na mkandarasi aitwaye China civil engineering consultant & cooperation  na kusimamiwa na mamlaka ya maji Mwanza kwa gharama ya shilingi bilioni 15.1 hadi kukamilika kwake.

Aweso amesema kuwa mradi huo unatakiwa kuisha haraka na kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi husika hivyo wao kama wizara hawatakuwa kikwazo cha wananchi kukosa huduma hiyo ya maji kwa kisingizio chochote.

“Ikumbukwe kuwa mradi huu ni ahadi ya Mhe. Rais Magufuli na tayari mradi  upo kwenye ilani, na siku chache zilizopita  Mhe. Rais alipita hapa na akauliza maendeleo ya mradi huu na kimsingi hakuridhishwa na kasi yake na akatoa maelekezo, kwanza niseme tu maelekezo hayo tumeyapokea na tunayatekeleza na ndio maana mimi waziri mwenye dhamana ya maji niko hapa, nikuombe mkandarasi tusijekuonana wabaya nataka mradi huu ukamilike kwa wakati uliopangwa ikiwemo pia kupitia upya gharama za mradi  huu.” Amesema Waziri Aweso.

Akitoa taarifa ya mradi kwa waziri, Leonard Msenyele Kaimu mkurugenzi wa MWAWASA ambaye ni msimamizi mkuu wa mradi huo amesema kuwa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 35% ambapo mkandarasi anatakiwa kujenga chanzo cha maji katika kingo za  mto Kagera, kulaza bomba la kilomita 1.6, kujenga mtambo wa kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha  lita milioni 6.57 kwa siku na tanki la kuhifadhia maji safi lenye ujazo wa lita milioni 2.

Msenyele ameongeza kuwa mkandarasi atatekeleza kazi hizo kwa gharama ya shilingi bilioni 9.4 huku akisisitiza kuwa malengo yao ni kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya miezi 6 iliyobaki na anauhakika watamaliza.

Akiongea na watumishi wa walioko chini ya wizara hiyo katika ukumbi wa mkuu wa mkoa Kagera, waziri Aweso amewataka watumishi hao kuwa waaminifu na wabunifu katika kutekeleza miradi ya maji kwenye maeneo yao ili kuhakikisha wananchi wananufaika na pesa inayotolewa na serikali yao.

Amewataka mameneja wa wilaya zote za mkoa wa Kagera kufikia tarehe 22 mwezi machi mwaka huu ambayo itakuwa ni siku ya kilele cha wiki ya maji, kuhakikisha wawe wamekamilisha miradi yote ya maji inayoendelea hasa miradi  kichefuchefu, na kuitumia siku hiyo kuikabidhi na kuzindua miradi  hiyo ikiwa inatoa maji safi  na salama na yenye kutosheleza.

Aidha amewaagiza mameneja wa mamlaka za maji wa mikoa na wilaya pamoja na mameneja wa wakala wa maji vijijini RUWASA wa mikoa na wilaya kujenga tabia ya kuongea na watumishi wao kuhusu mwenendo mzima wa utekelezaji wa majukumu yao huku akiwataka pia kuboresha maslahi  yao sambamba na kuwapa motisha pale wanapofanya vizuri.

Hata hivyo awali aliweza kupokea taarifa mbalimbali za maji kutoka RUWASA, MAABARA, BONDE na BUWASA ambapo wameeleza mafanikio makubwa waliyoyapata katika kipindi hiki cha miaka mitano huku BUWASA wakibainisha changamoto kubwa inayowasumbua ni ulimbikizaji wa madeni hasa taasisi za serikali mojawapo ikiwa ni Magereza Bukoba ambayo inadaiwa zaidi ya shilingi milioni 9.

No comments:

Post a Comment