Muonekano wa Boksi Kalavati lililopo Mto Nalingwenya katika Barabara ya Michiga-Makong’ondela lenye upana wa mita 4 likiwa limekamilika na kuanza kutumika.
Na. Thereza Chimagu
WANANCHI WA VIJIJI vya Makong’ondela, Pachani na Kilimanihewa
katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara wamepongeza Serikali kwa
kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja, vivuko na mitaro wilayani hapo
ikiwa ni sehemu ya kufungua fursa za kiuchumi na ukuaji wa miji katika maeneo
mbalimbali nchini.
Wakizungumza katika
mahojiano maalum hivi karibuni wilayani hapo, wananchi hao walisema
uthubutu uliofanywa na
Serikali katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa
barabara, madaraja na vivuko mbalimbali utaacha alama ya kihistoria kwa vizazi
vijavyo kuhusu wajibu wa Serikali katika kuwatumikia wananchi.
Bw. Juma Mazoea Mkazi wa Kijiji cha Makong’ondela ameipongeza Serikali kwa kwa kukamilisha ujenzi wa boksi
kalavati lililopo Mto Nalingwenya katika barabara ya Michiga-Makong’ondela na
kukiri kuwa kukamilika kwa Kalavati hilo kumerahisisha na kuimarisha
mawasiliano na usafirishaji ikiwemo usafirishaji wa mazao ya kilimo.
“Hapo mwanzo kulikuwa
na shida ya usafiri hasa mvua ikinyesha kwani kulikuwa na matope mengi ambayo
yalisababisha magari kushindwa kupita na kufanya tulipe nauli ya Shilingi 2000
lakini sasahivi magari yanapita bila matatizo na nauli imepungua tunalipa
Shilingi 1000 hivyo imetusaidia kuvusha mazao yetu kwa urahisi”, alisema Bw.
Mazoea.
Naye, Bi. Fatuma
Maliki Mkazi wa Kijiji cha Pachani alisema hapo mwanzo walikuwa wanapata shida
kuvuka kwenda upande wa pili, lakini hali ni tofauti kwani ujenzi wa daraja
hilo umewasaidia wananchi wa vijiji vya Makong’ondela na Pachani kwenda kwenye
maeneo yao ya uzalishaji hasa mashambani na si wakulima pekee pia imewasaidia
wanafunzi wanaotoka vijiji jirani kuvuka kwenda kwenye Kata yao kwa ajili ya
masomo.
Kwa upande wake, Bw.
Islam Mahela Mkazi wa Kijiji cha Kilimanihewa ameishukuru serikali kwa kujenga mtaro
eneo la sokoni kwani umewasaidia wafanyabiashara kuepukana na usumbufu wa maji
kujaa hasa kipindi cha mvua.
“Kabla ya mtaro huu
kujengwa wafanyabiashara wa hapa sokoni tulikuwa tunapata usumbufu mkubwa sana
wakati wa mvua kwasababu maji yalikuwa yanaingia hadi kwenye maduka lakini
tumeona mvua ya juzi kwakweli kuna ahueni maji hayatusumbui tena na tunaahidi
kuutunza kwa kufanya usafi ili uweze kudumu”, alisema Bw. Mahela.
Meneja wa TARURA
Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu Mhandisi Mwombeki Hussein alisema, TARURA
Wilaya ya Nanyumbu imefanya matengenezo ya kawaida ya kuchonga barabara jumla
ya Kilomita 442 katika Kata zote 17 wilayani hapo kwa lengo la kufungua fursa
za kiuchumi.
“Sisi kama Wakala
tumeamua kuzifungua barabara zote zaidi ya km 26 hapa mjini na barabara hizo
tumeziwekea vibao vya alama za barabarani kwa ajili ya usalama kwa watumiaji wa
barabara hizi, tumezifungua barabara hizi kwa lengo la kuboresha huduma za
kijamii na kiuchumi”, alisema Mhandisi Mwombeki.
Mhandisi huyo
aliongeza kuwa, mbali na uchongaji wa barabara pia wametekeleza ujenzi wa boksi
kalavati moja katika Mto Nalingwenya lenye upana wa mita 4 na kuweka changarawe
urefu wa Km 1 Barabara ya Michiga-Makong’ondela ambako kulikuwa hakupitiki
kabisa. Pia, wamejenga mtaro eneo la sokoni Kilimanihewa wenye mita
150 na upana kipenyo 0.9 ambao umeshakamilika na wananchi wanaendelea
kunufaika.
Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu unaendelea na
utekelezaji wa miradi mbalimbali wilayani humo ili kuwawezesha wananchi
kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment