| Huduma za mkono kwa mkono zinazotembea maarufu ‘One Stop Center Mobile’ zikitolewa kwenye Kata ya Chanika. |
| Huduma za mkono kwa mkono zinazotembea maarufu ‘One Stop Center Mobile’ zikitolewa kwenye Kata ya Segerea. |
| Huduma za mkono kwa mkono zinazotembea maarufu ‘One Stop Center Mobile’ zikitolewa kwenye Kata ya Segerea. |
WANANCHI 752 wamejitokeza katika huduma za mkono kwa mkono zinazotembea maarufu ‘One Stop Center Mobile’ kupata huduma anuai ikiwemo kuelezea madhira waliyoyapata vikiwemo vitendo vya kutelekezewa watoto, dharau na kupigwa na wake zao. Katika huduma hizo za siku mbilimbili zilizotolewa Kata za Chanika, Pugu na Gongolamboto, wanaume walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa kwenye misululu wakisubiri na kisha kupata huduma hizo zikiwamo za upimaji wa macho, kisukari, shinikizo la damu na unasihi kwa waathirika wa unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ukiwamo dhidi ya wanawake na watoto.
Hata hivyo, huduma za one stop center katika maeneo hayo zilienda sambamba na kuwafikishia watu elimu katika maeneo yao kupitia vipeperushi, matangazo na mazungumzo ya ana kwa ana kuhusu maana, aina, madhara, kutambua na namna ya kupambana na ukatili huo. Takribani wananchi 3,600 sawa na wastani wa watu 600 kwa siku, walifikiwa na elimu ya masuala ya unyanyasaji wa kijinsia.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Janeth Magomi na pamoja na Mratibu wa One Stop Center katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Dk. Christina Onyango, wakizungumza kwa nyakati tofauti wakiwa Segerea wanabainisha kuwa, mafanikio hayo yametokana na kutolewa kwa elimu dhidi ya ukatili wa kijinisa.
“Polisi Ilala tuliona baada ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, tuje na mwendelezo kwa kutoa huduma ili waathirika baada ya kuelewa, sasa wachukue hatua na kufunguka ndiyo maana tunawasogezea huduma katika maeneo yao,” alisema Kamanda Magomi.
Kwa upande wake Onyango alisema idadi hiyo ya waliojitokeza ni mafanikio makubwa, kwani licha ya kupata idadi hiyo lipo kundi la akinababa lilijitokeza pia kupata huduma hizo. "... Kama kwa miezi miwili au zaidi kituoni mnaweza msipate mwanaume hata mmoja, anayelalamikia ukatili wa kijinsia, lakini hapa kwa siku sita tumepata wanaume 341 na elimu kufikia watu zaidi ya 3,600 kwa siku sita, ni mafanikio makubwa.”
Alisema katika vituo hivyo vya huduma zinazotembea, watu 752 wakiwamo watoto 60; wanawake wakiwa 411 na wanaume 341, walijitokeza kutafuta huduma zikiwamo za afya. Alisema wananchi waliohitaji huduma za polisi walikuwa 300, huduma za wanasheria 225, huduma za ustawi wa jamii 112 na huduma za afya 106. Kwa afya, karibu asilimia 90, walitaka huduma za upimaji wa macho na miwani.
Kwa mujibu wa Onyango, miongoni mwa wanaume waliojitokeza, wengine walilalamikia kupigwa na wake zao, ulevi wa kupindukia wa wake zao, kukosa uaminifu katika ndoa, wanawake kutelekeza watoto siku nzima bila huduma na wanawake hao kurudi nyumbani usiku wakiwa wamelewa na kutukana ovyo.
“Wakasema wakienda kazini wanaporudi nyumbani, wanakuta watoto peke yao na hawajala, wanalia, wamechafuka na hivyo, wanaume hao kulazimika kuingia jikono kupikia watoto, lakini pia wengine wakasema wake zao wakirudi usiku, wanawatukana, wanawafokea na kuwanyima unyumba,” alisema Onyango.
Kuhusu huduma za polisi na maofisa wa ustawi wa jamii, watu wengi hasa wanawake walieleza vitendo vya kupigwa, ubakaji hata katika ndoa, ulawiti na mateso dhidi ya watoto.
“Kwa upande wa sheria, wengi walitaka elimu kuhusu migogoro ya ardhi na mirathi….Hawa wengi kesi zao ziko mahakamani hivyo, walitaka elimu ili wajue sheria zinasemaje kuhusu masuala yao,".
Akitoa maoni yake kuhusu changamoto anazoziona katika utoaji wa huduma za one stop center mobile, Mkurugenzi wa Mradi katika taasisi ya Friedrich Naumann Foundation for Freedom, East Africa kwa Tanzania na Kenya, Veni Swai, alisema: “Changamoto kubwa ni upungufu wa rasilimali yaani muda, watoa huduma na vifaa maana huduma zinatolewa kwa siku mbili kwa kata na hapo, ndipo watu wanaanza kuongezeka na kufanya wahudumu na vifaa vilivyopo kutokidhi idadi ya watu.”

No comments:
Post a Comment