Wananchi wakishangilia Kivuko kipya cha MV. UKARA ambacho kimejengwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 na kina uwezo wa kubeba abiria 300 na magari 10 sawa na tani 300. |
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack Kamwelwe ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), kuhakikisha huduma ya uendeshaji wa vivuko inakuwa salama na ya uhakika wakati wote.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kivuko kipya cha Mv. UKARA II kitakacho toa huduma kati ya Kisiwa cha Ukara na Bogorora wilayani Ukerewe, Eng. Kamwele amewataka Temesa kuwa wabunifu, wazalendo na wanaojifunza kila mara ili kuepuka kero na ajali zinazoepukika.
"Hakikisheni abiria na mizigo inayopakizwa kwenye kivuko inazingatia uwezo ili kulinda usalama wa abiria na mali zao", alisisitiza Waziri, Eng. Kamwelwe.
Ameongeza kuwa upo umuhimu wa Shirika la Wakala wa Meli, TASAC kukagua na kutoa elimu ya kutosha kwa wadau wote wa usafiri majini ili kuufanya usafiri huo kuwa salama wakati wote.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Ujenzi Arch. Elius Mwakalinga amesema Wizara itafunga mtambo wa Tehama utakaowezesha vivuko vyote nchini kufuatiliwa vinavyofanya kazi kwa kutokea Wizarani ili kupunguza changamoto zinazosababishwa na binadamu.
"Tumejipanga kuboresha usafiri kayika maziwa na bahari ili kuongeza fursa za ajira na uchumi kwa watanzania," amesisitiza Arch. Mwakalinga.
Aidha Katibu Mkuu huyo amempongeza mkandarasi Songoro Marine kwa kujenga kivuko hicho kipya na chakisasa kwa muda mfupi. Mtendaji mkuu wa Temesa Eng. Japhet Masele kilichogharimu shilingi bilioni 4.2 kina uwezo wa kubeba tani mia moja ikiwa ni abiria 300 na magari 10 kwa wakati mmoja.
Zaidi ya shilingi Bilioni 36.3 zimetumika katika ujenzi wa vivuko saba ambavyo ni Mv Ilemela, Mv, Mwanza, Mv Ukara II, Mv. Tanga, Mv. Kazi, Mv Chato na Mv. Mafia ambavyo kwa pamoja vitahuisha huduma za usafiri katika baadhi ya maeneo ya ziwa Victoria na Pwani ya Bahari ya Hindi.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment