LISSU MWISHO WA UBAYA NI AIBU…! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 5 October 2020

LISSU MWISHO WA UBAYA NI AIBU…!

Tundu Lissu.


Na Mwandishi Wetu

INASIKITISHA lakini inasadia kufungua macho ya akili zetu kuona, kutambua na kupambanua jema na ovu, kiongozi wa kweli na asiyetutakia mema, mwenye nia ya dhati kuwasaidia wananchi na mwenye agenda iliyofichika dhidi ya hatma ya taifa letu.

Kwamba mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu, kasema uongo kuhusu Rais John Magufuli kuwakusanya Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini jijini Dodoma kufanya nao kikao ili kushawishi ushindi wake, ni suala lisilokuwa na ubishi, ushahidi wote umethibitisha kwamba alidanganya.

Kwamba kanuni za maadili ya uchaguzi zinakataza kusema uongo, ni jambo ambalo limekubaliwa na kupitishwa na vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi na kwamba ukikiuka kanuni hizo utachukuliwa hatua.

Tume wamewita Lissu kujieleza kuhusu kusema uongo huo, amekataa hadharani kila mtu kasikia, kamati ya maadili inayohusisha vyama vyote wamechukua hatua kumsimamisha kampeni kwa siku saba, akatamka hadharani kwamba hatasimama, ataendelea na kampeni.

Hatimaye amekubali lakini kihasidi hasidi, anasimamisha kampeni lakini anaendelea na kazi za siasa kama Makamu Mwenyekiti wa chama, kwa maana hiyo ataendelea kupanda majukwaani. Swali la kujiuliza  akipanda jukwaani atasema nini wakati huu wa kampeni? Ni wazi lazima atanadi ilani na sera za chama chake na wagombea wake.

Hii mana yake nini? Ni kwamba atakuwa anaendelea na kampeni ambazo Kamati ya Maadili ya uchaguzi, imemzuia kufanya. Kwa hiyo hii ni kuzifanya kanuni za maadili ya uchaguzi na kamati yenyewe kutokuwa na maana, na watanzania wote wenye mapenzi mema kuwafanya wajinga, na tafsiri yake fupi ni kwamba anajiona yuko juu ya sheria.

Amedanganya hadharani, ameitwa kujieleza hataki, amepewa adhabu ameikataa na bado anataka Watanzania tuendelee kuamini kwamba huyu anaweza kuwa kiongozi wa taifa hili, hapana tunaipenda nchi yetu.

Si mjinga, ni mwerevu, anayo agenda ya siri, ni kuuvuruga uchaguzi huu uwe na fujo ili kiu yake na dhamira yake aliyokuwa akiitangaza muda wote akiwa nje ya nchi itimie, hataki Tanzania iwe  na amani.

Vinginevyo mtu wa aina hii anataka nini, analazimisha kupanda jukwaani, hatua zichukuliwe, ahamasishe wafuasi wake kwamba anaonewa, alishakubali kutumikia adhabu ya siku saba, sasa alikuwa anafanya kazi ya makamu mwenyekiti, amenyimwa haki na Tanzania hakuna uhuru wa kisiasa, wafuasi wake walipuke, nchi iingie kwenye machafuko, huyu ni hatari kuliko ukoma kipeuo cha pili.

Amekuwa nje ya nchi muda mrefu kwa matibabu, kama binadamu na mtanzania mwenzetu, tulisikitika naye, na tumemuombea kheri, tunamshukuru Mwenyezi Mungu amemponya na kuruda salama, lakini kuumizwa kwake kusiwe sababu ya kuiweka rehani amani ya Taifa letu.

Anachokifanya sasa hivi Lissu, unaweza ukitafsiri vyema kwenye kauli ambazo zimekuwa zitokelewa na wakili wake, Bob Amsterdam, wanataka kuivuruga amani yetu kwa malengo ambayo yanajulikana vyema na wao wenyewe.

Anachokifanya sasa hivi, ni kutaka kutekeleza malengo au ahadi zake walizopeana na wahisani wake, ambao hawafurahishwi na jinsi Tanzania inavyochukua hatua za kujitegemea na kusimamia misimamo yake yenyewe, wao wangependa waendelee kutuburuza, lakini kwa ujasiri wa Rais Magufuli wanaona hili linashindikana kwa Tanzania.

Walitutisha, wakatuogopesha kuhusu msimamo wetu kwenye kushughulikia korona, wakakuta Rais Magufuli ni madhubuti na imara, wakaanza kuomba dua za kuku, tutaokota maiti barabarani, Mungu wetu tunayemtumaini akasimama na sisi, akawafedhehesha.

Sasa wanatafuta njia ya kutushikisha adabu, wamepata upenyo kupitia uchaguzi huu, wanatumia kila njia inayowezekana, kutusambaratisha. 

Tunawambia kama tulivyoshinda kwenye janga la korona, tunawahakikishia kwa kuwa Mungu wetu yuko na upande wetu, kwenye njama hizi za kutaka kumpaka matope Rais Magufuli ili kuchafua rekodi ya kazi zake zilizotukuka, tutashinda na zaidi ya kushinda, na Lissu pamoja na mabwana zake, wataabika.


Magufuli mitano tena

No comments:

Post a Comment