WAMILIKI WA VIWANDA VYA KAHAWA KAGERA WAOMBWA KUANZISHA MIGAHAWA YA KAHAWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 5 August 2020

WAMILIKI WA VIWANDA VYA KAHAWA KAGERA WAOMBWA KUANZISHA MIGAHAWA YA KAHAWA

Katibu tawala Mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamuzora akionja kahawa inayotengenezwa na kiwanda cha AMIMZA kilichopo wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera alipofanya ziara kiwandani hapo Agosti 05, Mwaka huu.


Na Allawi Kaboyo, Bukoba

MKOA wa Kagera ni miongoni mwa mikoa inayolima na kuzalisha kwa wingi zao la Kahawa hapa nchini ambapo imeelezwa kuwa pamoja na uzalishaji huo wananchi wa mkoa huo hawana utamaduni wa kunywa kahawa wanayoilima wao.

Hayo yamesemwa na katibu tawala wa mkoa huo Prof. Faustine Kamuzora Agosti 05, Mwaka huu alipofanya ziara katika kiwanda cha kahawa cha AMIMZA kilichopo halmashauri ya wilaya Bukoba Mkoani humo ambapo amesema kuwa wananchi wa mkoa huo ni wakulima wazuri wa kahawa ila sio watumiaji wa kahawa yao.

Prof. Kamuzora ameongeza kuwa Kahawa inayolimwa Kagera imekuwa Kahawa bora Duniani ambayo hupelekea baadhi ya makampuni huko ulimwenguni kuitumia kwa kuiwekea Rebo nyingine ambao hunufaika Zaidi na kahawa yetu kutokana na faida zilizopo kwenye zao hilo.

“Watanzania hasa wanakagera hawana utamaduni wa kunywa kahawa pamoja ya kuwa sisi wenyewe ni wazalishaji wa kubwa wa Kahawa hapa nchini, naona ipo haja ya watu wetu kuelimishwa faida za unywaji wa kahawa. Nikuombe wewe ni mwenzetu na bahati nzuri kiwanda chako kiko hapa mkoani kwetu utufungulie Mgahawa wa Kahawa ili watanzania na wanakagera waanze kujifunza umuhimu na faida za unywaji wa Kahawa.” Amesema Prof. Kamuzora.

Amrongeza kuwa Mkoa wa Kagera unayo fursa nyingi za uwekezaji hasa za viwanda na kuwasihi wawekezaji kujitokeza kuja Kagera kwa kuwa usalama ni wa kutosha na kuongeza kuwa zao la kahawa linatakiwa kuwa zao bora nchini kama watanzania wataamua kulipa umuhimu na nafasi.

Aidha amewataka wanunuzi binafsi kujitokeza kununua Kahawa za wakulima ili wakulima hao wanufaike na zao lao kwa kuwa milango sasa iko wazi kwa wanunuzi hao ambapo amewata kufata taratibu zilizowekwa na serikali katika kununua kahawa hiyo.

“Sisi kama serikali tayari tumefungua milango kwa wanunuzi binafsi wa kahawa yetu alimuhimu fateni utaratibu, sisi tunachotaka kahawa ya mkulima inunuliwa na imunufaishe mkulima moja kwa moja na bei iwe ya kuridhisha.” Amesisitiza Prof. Kamuzora.

Kwaupande wake mmiliki wa kiwanda cha AMIMZA Alhaj Amir Hamza amesema kuwa kiwanda hicho kipo katika maboresho kwa kuongezea baadhi ya idara na kuongeza kuwa kikikamilika kitaweza kutoa ajira kwa watanzania Zaidi ya 200 hadi 400 wa kudumu na watu 600 hadi 1000 wa ajira za muda.

Alhaj Amir ameongeza kuwa kiwanda kikikamilika kitaweza kuzarisha kahawa mumunyifu tani 6,000 sawa na tani 18,000 za kahawa safi  ambazo ni sawa na tani 36,000 za kahawa ya maganda ambayo ni mara mbiri kutokana na gredi ya kahawa hivyo kupelekea mahitaji kuwa tani 72,000 za kahawa ya maganda kwa mwaka.

“Mpaka sasa pamoja na uzarishaji unaoendelea tumeajiri watu 40 pamoja na kutoa ajira nyingine kwa wananchi ambao ni majirani zetu hapa ambapo pia tumejenga kiwanda kikubwa Africa Mashariki na kati, niseme tu sisi soko letu lipo nje ya nchi ila kwasasa tumerudi nyuma baada ya janga hili la Covid-19 unaosababishwa na Virusi vya Corona baada ya baadhi ya nchi kufunga mipaka yake.” Amesema Alhaj Amir.

Sanjali na hayo ameiomba serikali kuwasaidia kupata mikopo yenye riba nafuu ili kuweza kuboresha miundombinu ya kiwanda hicho pamoja nakupata malighafi kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji ambapo pia ameomba serikali kushughulikia changamoto za umeme ambao umekuwa tatizo na kusababisha hasara kutokana na kukatika hovyo.


No comments:

Post a Comment