KAMWELWE: BARABARA YA MBINGA - MBAMBA BAY KUKAMILIKA DISEMBA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 5 August 2020

KAMWELWE: BARABARA YA MBINGA - MBAMBA BAY KUKAMILIKA DISEMBA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akizungumza na Wakandarasi wa kampuni ya CHICO wanaojenga barabara ya Mbinga - Mbamba Bay (km 66) kwa kiwango cha lami, Mkoani Ruvuma. Ujenzi wa Barabara hiyo unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2020.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akifafanua jambo kwa wananchi wa eneo la Mbamba Bay wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara ya Mbinga - Mbamba Bay (km 66) kwa kiwango cha lami, Mkoani Ruvuma. Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 62.


Kazi za ujenzi wa barabara ya Mbinga - Mbamba Bay (km 66) kwa kiwango cha lami ukiendelea, Mkoani Ruvuma. Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 62 na ikikamilika itarahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa maeneo ya Kanda ya Kusini na  Nyanda za Juu.


Kazi za ujenzi wa barabara ya Mbinga - Mbamba Bay (km 66) kwa kiwango cha lami ukiendelea, Mkoani Ruvuma. Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 62 na ikikamilika itarahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa maeneo ya Kanda ya Kusini na  Nyanda za Juu.


WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amewatoa hofu wananchi wa Wilaya ya Mbinga na Nyasa kwa kile wanachoambiwa kuwa ujenzi wa barabara ya Mbinga - Mbamba Bay  (km 66) hautokamilika mwaka huu.

Kamwelwe ameyasema hayo akiwa Mbamba Bay Wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, wakati alipokutana na wananchi na kusikiliza changamoto wanazozipata katika barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi CHICO kwa gharama  zaidi ya shilingi Bilioni 129.

Amewaeleza wananchi hao kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Disemba mwaka huu kwa kiwango cha lami ambapo hadi sasa mkandarasi ameshakamilisha kujenga kilometa 32.

"Nimekagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huu unaridhisha, na kwa mujibu wa mkataba utakamilika mwishoni mwa mwaka huu kama ulivyopangwa na sisi kama Serikali  hatuna  maombi yoyote maalumu ya mkandarasi ya kuongeza muda", amesema Waziri Kamwelwe.

Aidha, amewaeleza wananchi hao kuwa utekelezaji wa barabara hiyo ni ahadi ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya maendeleo ya wilaya hizo  ambao hawajawahi kupata barabara ya lami kwa kipindi kirefu na pia ni wazalishaji wazuri wa mazao ya chakula na biashara.

"Hamuwezi mkazaliwa mpaka Mwenyezi Mungu akawachukua mkiwa  bado mpo kwenye vumbi, Serikali ipo kwa ajili ya wananchi wake sasa ni lami tu", amesisitiza Waziri Kamwelwe.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutafungua fursa nyingi za kiuchumi na kijamii ikiwemo kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa eneo la Kanda ya Kusini na  Nyanda za Juu.

Sambamba na barabara hiyo, Waziri Kamwelwe ameeleza miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali kwa wakazi wa Wilaya ya Nyasa ambayo ni ujenzi wa gati la Ndumbi, na hivi karibuni ujenzi wa gati la Mbamba Bay kwa ajili ya kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani ikiwemo Malawi, Zambia na Msumbiji utaanza.  

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Ruvuma Mhandisi Lazeck Alinanuswe, amemueleza Waziri huyo pamoja na wananchi wa Nyasa kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatekelezwa kwa muda wa miezi 33 na hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 62.

"Kazi zinaendelea na sisi tunaendelea kuusimamia kwa karibu mradi huu ili ukamilike kwa wakati na kwa mujibu wa mkataba", amesema Mhandisi Alinanuswe.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Bw. Edmond Mapunda ambaye ni mkazi wa Mbamba Bay, amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwa utekelezaji makini wa ujenzi wa miundombinu hapa nchini hususani ya barabara, bandari na viwanja vya ndege kwani matunda yake wanazidi kunufaika nayo kila leo katika maisha yao.

Ujenzi wa Barabara ya Mbinga - Mbamba Bay (km 66) ndiyo sehemu pekee iliyokuwa imebaki kujengwa kwa kiwango cha lami katika ushoroba wa Mtwara unaounganisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma na hivyo kukamilisha jumla ya  urefu wa kilometa 1,024 za barabara kwa kiwango cha lami katika ushoroba huo.


No comments:

Post a Comment