Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha kuchakata mafuta ya alizeti cha Yaza Investment kilichopo Wilaya ya Iramba mkoani hapa, Yusuph Nalompa, akizungumza mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki (katikati), sababu ya kiwanda hicho kushindwa kuanza uzalishaji alipokitembelea wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kutembelea miradi ya uwekezaji mkoani hapa jana. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula ya alizeti cha Singida Grains and Oil Mills au Singida Fresh, Khalid Ally (wa pili kushoto) akimuelekeza jambo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki alipotembelea kiwanda hicho wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kutembelea miradi ya uwekezaji mkoani hapa jana.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki, akitoka kuangalia mtambo wa kutengeneza mafuta ya alizeti katika Kiwanda cha Meru Millers Ltd.
Meneja wa Kiwanda cha Biosustain Tz Ltd, Salum Khalfan (katikati), akimuelekeza jambo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki alipotembelea kiwanda hicho. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Sajjad Haider.
Wafanyakazi wa Kiwanda cha Biosustain Tz Ltd wakiwa katika eneo la kiwanda.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki akiwa ameongoza na viongozi mbalimbali wakati akienda kukagua Kiwanda cha Yaza Investment. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula.
Wananchi Kijiji cha Ndago na viongozi wa Wilaya ya Iramba wakimsikiza Waziri Kairuki (hayupo pichani) wakati akizungumzia kuhusu Kiwanda cha Yaza Investment ambacho hakifanyi kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Dk. Rehema Nchimbi, akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Ndago kuhusu kiwanda hicho.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Ndago kuhusu kiwanda hicho.
Askari Polisi wa Wilaya ya Iramba wakiimarisha ulinzi wakati wa ziara ya Waziri Kairuki katika Kiwanda cha Yaza Investment.
Moja ya jengo la Kiwanda cha Yaza Investment.
Makofi yakipigwa wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Ndago kuhusu kiwanda hicho.
Mwananchi wa Kata ya Ndago. Hassani akizungumzia kiwanda hicho.
Diwani wa Kata ya Ndago, Hewery Nkandi akizungumzia changamoto wanazopata wananchi kutokana na kiwanda hicho kutofanya kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula ya alizeti cha Singida Grains and Oil Mills au Singida Fresh, Khalid Ally (katikati) akienda kumtembeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki kwenye kiwanda hicho.
Wananchi wakimsikiza Waziri Kairuki (hayupo pichani) wakati alipofika kutembelea Kiwanda cha Singida Grains and Oil Mills
Meneja wa Kiwanda cha Mount Meru Millers Ltd, Nelson Mwakabuta (katikati) akimuonesha Waziri Kairuki mafuta yanayozalishwa na kiwanda hicho. Kulia ni Operation Meneja wa kiwanda hicho, Sanjay Chourasya.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida na viongozi wengine wa mkoa huo kwa kuhimiza uwekezaji hususani wa viwanda vya uzalishaji wa mafuta ya kula ya alizeti.
Kairuki alitoa pongezi hizo jana wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kutembelea miradi ya uwekezaji mkoani hapa ambapo alikagua viwanda vitano vya Yaza Investment, Kiwanda cha Singida Grains and Oil Mills au Singida Fresh, Kiwanda cha Meru Millers Ltd, Kiwanda cha Biosustain Tz Ltd na Kiwanda cha Q-STEK Tz Ltd.
" Kipekee nikupongeze mkuu wa mkoa Dk. Rehema Nchimbi kwa namna unavyohimiza uwekezaji katika mkoa wa singida ambao mpaka sasa una viwanda 1800" alisema Kairuki.
Hata hivyo Kairuki alisikitishwa na Kiwanda cha kuchakata mafuta ya alizeti cha Yaza Investment kilichopo Wilaya ya Iramba mkoani hapa chenye uwekezaji mkubwa wa zaidi ya bilioni 10.2 kikiwa hakifanyi kazi licha ya miundombinu yake yote ikiwaimekamilika.
Kairuki alisema kiwanda hicho kilitegemea kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 50 huku ajira zisizo za moja kwa moja zaidi 1000, kuzalisha mbegu, pamoja na wasafirishaji.
" Jambo ili linaumiza sana moyo na kusikitisha." alisema Kairuki.
Alisema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji imekuwa ikihimiza mara kwa mara kama juu ya uwekezaji kama ambavyo Waziri Mkuu mwenye wizara hiyo amekuwa akiweka mkazo katika kilimo cha mazao mkakati na hivi karibuni alionekana mkoani Kigoma akigawa miche ya mbegu za michikichi takriban milioni 1.8.
Alisema amekuwa akifanya hivyo sehemu mbalimbali lengo likiwa ni kuona Taifa linajitosheleza katika mafuta ya kula kwani kwa sasa tunaagiza mafuta hayo zaidi ya asilimia 60.
Kairuki alisema Mkoa wa Singida umejaaliwa na kuwa una baraka kwani zao la alizeti linastawi vizuri na kuwa Kiwanda cha Yaza Investment ni moja ya kiwanda kikubwa katika Wilaya ya Iramba na mwekezaji ni mzawa hivyo haitawezekana uwekezaji huo hupotee hivi hivi.
Alisema wizara inahimiza kuwepo na viwanda vingi vya kuzalisha mafuta ya kula na kuwa kama Taifa zaidi ya sh.bilioni 443 tunapoteza kwa ajili ya kuagiza mafutà na ukiangalia katika zao la alizeti zaidi ya asilimia 70 kwenye mafuta yanatokana na zao hilo hivyo ni lazima likapewa kipaumbele.
Msimamizi wa Kiwanda cha Singida Grains and Oil Mills, Jamal Juma akitoa taarifa kwa Kairuki alisema tozo mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kushindwa kutoa leseni ya athari za mazingira zimesababisha
kiwanda hicho kuchelewa kuanza kufanya kazi.
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda cha Mount Meru Millers Ltd, Nelson Mwakabuta alisema ili kuongeza hamasa ya wanafunzi kuzingatia masomo hususan wa shule za msingi na kwa nia ya kukuza mahusiano mema mema na jamii, kampuni ina utaratibu wa kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi tangu mwaka 2015.
Alisema mpaka sasa wanatoa huduma hiyo kwa shule za msingi 45 Arusha zenye jumla ya wanafunzi 65,743 na shule moja Singida yenye wanafunzi 1,288 na kuwa katika baadhi ya maeneo ya wakulima wametoa mbegu bora ya alizeti ili wakulima wavune
zaidi kwa ekari na kupata mafuta mengi kutoka kilo moja ya mavuno.
No comments:
Post a Comment