Malori yakiwa mpakani. |
IDADI ya wagonjwa wa virusi vya corona nchini Kenya imeongezeka hadi 700 baada ya wagonjwa wapya 28 kuthibitishwa katika kipindi cha saa 24. Katibu Mtendaji Wizara ya Afya Kenya, Rashid Aman amesema kwamba kati ya wagonjwa hao wapya 10 wanatoka Mombasa , 9 kutoka Kajiado na 7 kutoka Nairobi huku 2 wakitoka Wajir.
Wagonjwa wote tisa kutoka Kajiado ni madereva wa malori ya masafa marefu ambao walikuwa wanarudi kutoka Tanzania katika mpaka wa Namanga. Aman amesema kwamba madereva hao kutoka kajiado walipimwa katika mpaka wa Namanga pamoja na wenzao wa Tanzania.
''Madereva wa Tanzania waliokuwa wakiingia Kenya kupitia mpaka huo wanapimwa upande wao wa eneo lao la mpakani. Madereva wa tano wa Tanzania pia walikutwa na virusi vya ugonjwa huo na tayari tumewasiliana na mamlaka ya taifa hilo kulishughulikia suala hilo'', alisema.
Jumla ya sampuli 841 zilifanyiwa vipimo katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Afisa huyo wa afya alitangaza wagonjwa wengine 12 waliopona na hivyobasi kufanya idadi ya wale waliopona kufikia 251.
Amesema kwamba wagonjwa wengi ambao wamefariki na ugonjwa huo katika kaunti ya Mombasa ni watu wenye umri mkubwa.
Hata hivyo, Aman alitangaza kifo kimoja zaidi mjini Nairobi na hivyobasi kuongeza idadi ya waliofariki kutokana na ugonjwa huo kufikia watu 23. Aman ameongezea kwamba idadi ya kaunti zilizoathiriwa na ugonjwa huo zimeongezeka.
''Ni wazi kwamba ugonjwa huu utasambaa katika taifa zima huku tukiingia katika mwezi wa tatu ni lazima tulindane'', alisema.
Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari siku ya Jumatatu , afisa huyo alisema kwamba lengo la serikali ni kupunguza usambazaji katika jamii. Aman amewataka Wakenya kuripoti katika hospitali zilizo karibu nao kuhakikisha kwamba wanasaidika kabla ya dalili hizo kuwa mbaya.
-BBC
No comments:
Post a Comment