WAGONJWA 23 WA CORONA WATHIBITISHWA ZANZIBAR, WAWILI WAFARIKI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 19 April 2020

WAGONJWA 23 WA CORONA WATHIBITISHWA ZANZIBAR, WAWILI WAFARIKI

Waziri wa Afya Zanzibar, Hamadi Rashid 


WIZARA ya Afya Zanzibar imethibitisha kuwa na ongezeko la wagonjwa wapya 23 wa virusi vya corona na kufikia wagonjwa 58 waliothibitika kuambukizwa ugonjwa huo visiwani humo. Kati ya wagonjwa wapya hao, wagonjwa 21 wanaishi Kisiwani Unguja na wawili Kisiwa cha Pemba.

Huku wagonjwa 21 ni raia wa Tanzania wengine wawili ni raia wa kigeni, (Ufaransa na Cuba) wote wanaishi visiwani humo. Wagonjwa wawili kati ya wagonjwa wapya walifariki nyumbani kabla ya kuchukuliwa vipimo, na kufanya jumla ya wagonjwa waliofariki kwa maambukizi ya corona kufikia watatu.

Wizara ya afya nchini Uganda jana ilithibitisha kuwa ipo katika harakati za kumtafuta raia wa Tanzania aliyepatikana na virusi vya corona kwa lengo la kumrudisha nyumbani.

Mtu huyo wa miaka 34, ambaye ni dereva wa lori kutoka Dar es Salaam, Tanzania aliwasili katika kituo cha mpakani cha Mutukula Aprili 16, 2020. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya mtu huyo hakuonesha dalili zozote za Covid-19.

Hatua ya Uganda kuwarudisha makwao raia wa kigeni waliopatikana na ugonjwa wa corona imezua gumzo kali katika mitandao ya kijamii ndani na nje ya nchi hiyo.

Siku ya Alhamisi Waziri wa Afya Ruth Jane Aceng alisema kuwa mataifa wanachama wa Muungano wa Afrika Mashariki yalikubaliana kila raia wa nchi hizo ambaye atakayepatika na virusi vya ugonjwa wa corona atarejeshwa nyumbani kwa matibabu.

Alisema kuwa Uganda kila siku huwapokea hadi madereva 3,000 wa malori kutoka mataifa ya Kanda ya Afrika Mashariki na kwamba nchi hiyo haina uwezo wa kuwapa huduma za matibabu.
-BBC

No comments:

Post a Comment