VIFAA VYA KUPAMBANA NA CORONA VYAGAWIWA SONGWE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 14 April 2020

VIFAA VYA KUPAMBANA NA CORONA VYAGAWIWA SONGWE

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akipokea vitakasa mikono kutoka kwa Balozi wa Kampeni ya Mikono Safi, Tanzania Salama Mrisho Mpoto ambapo Wizara ya Afya imetoa vitakasa mikono lita 150 kwa Mkoa wa Songwe.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akipokea vitakasa mikono kutoka kwa Balozi wa Kampeni ya Mikono Safi, Tanzania Salama Mrisho Mpoto ambapo Wizara ya Afya imetoa vitakasa mikono lita 150 kwa Mkoa wa Songwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe George Kyando akinawa mikono kwa kutumia mashine ya kunawia bila kushika koki ambapo Wizara ya Afya imetoa mashine hizo mbili kwa Mkoa wa Songwe, moja itawekwa katika Mpaka wa Tunduma na moja itawekwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa vifaa mbalimbali vya kupambana na ugonjwa wa Virusi vya Corona kwa Mkoa wa Songwe huku ikiridhishwa na namna ambavyo Mkoa umechukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Hayo yamebainishwa mapema leo na Mkuu wa Kitengo cha Maji Salama na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya Anyitike Mwakitalima wakati akikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe vitakasa mikono lita 150, mashine za kutolea vitakasa mikono 30 na mashine mbili za kunawia bila kushika koki.
Mwakitalima amesema Wizara ya Afya inaendesha Kampeni ya Mikono Safi, Tanzania Salama ambapo pamoja na kutoa vifaa vya kupambana na ugonjwa wa virusi vya Corona kama vile vitakasa mikono pia hutoa elimu kwa wananchi namna ya kujikinga na Corona hasa kwa Mikoa iliyoko Mipakani kama Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameipongeza Wizara ya Afya kwa kutoa vifaa hivyo hasa kwa Mkoa wa Songwe ambao upo Mpakani na ni Lango la kuingilia nchi za SADC ambapo vitakasa mikono 50 vinapelekwa katika jeshi la Polisi na 100 katika halmashauri zote.
Brig. Jen. Mwangela amesema,“Sisi Songwe ni Lango la SADC tukizubaa, tusipotoa elimu vizuri kwa Wananchi, tusipo chukua tahadhari ya kutosha tunaweza kuingiza Ugonjwa kutoka nchi jirani ambazo nazo zimeahirika na Corona”.
Ameongeza kuwa mpaka kufikia jana jumla ya wasafiri 180 wamewekwa karantini katika Halmashauri za Tunduma na Ileje  kwa muda wa siku 14 ikiwa ni jitihada za Serikali katika kuchukua tahadhari ya Ugonjwa wa Corona ambapo pia hakuna mshukiwa wa ugonjwa huo kwa Mkoa wa Songwe hadi sasa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe George Kyando ameishukuru Wizara ya Afya kwa kutoa kipaumbele kwa Jeshi hilo kwa kuwapatia vitakasa mikono kwakuwa wamekua wakisahaulika na wadau wengine huku akieleza kuwa anaendelea kutoa elimu kwa askari wachukue tahadhari zote muhimu wawapo katika majukumu yao.
Amesema katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Corona Jeshi la Polisi lina mchango mkubwa katika kulinda karantini na maeneo waliyotengwa wagonjwa wa Corona, pia kukagua mabasi na magari yote ya abiria hivyo wako katika hatari ya kuambukizwa.
Balozi wa Kampeni ya Mikono Safi, Tanzania Salama Mrisho Mpoto maarufu kama Mjomba amesema vita ya kupambana na Ugonjwa wa Virusi vya Corona inahitaji ushirikiano wa wananchi wote waweze kunawa kwa maji tiririka na sabuni kila wakati bila kuchoka na kutoona kama adhabu.
Mpoto amesema wananchi wa Songwe wanapaswa kuacha mila za kusalimiana kwa kushikana mikono, kukumbatiana, kubusiana kuepuka misongamano isiyo ya lazima kwa kuwa mafanikio yatapatikana kwa umoja ikiwa wananchi wote watazingatia kauli mbiu ya Jilinde na Umlinde Mwenzio.

No comments:

Post a Comment