Na Prudence Constantine Dar es Salaam
MAAFISA Ustawi na Maendeleo ya Jamii nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu kutoa elimu kwa umma dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona ili kuepusha ongezeko la maambukizi ya virusi hivyo.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu wakati akifungua mafunzo kwa maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Kata za Mkoa wa Dar Es Salaam yaliyofanyika katika Manispaa ya Temeke.
Dkt. Jingu amesema kuwa elimu kwa umma hasa katika ngazi ya Kata na mitaa inategemea zaidi maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii ili kukabiliana na maabukizi.
"Kama tutatimiza wajibu wetu kwa jamii kwa kutanguliza maslahi ya taifa, Tanzania itaepuka maambukizi zaidi ya virusi vya Corona" alisema.
Dkt. Jingu alikiri kuona kazi kubwa inayofanywa na watendaji mbalimbali ikiwa ni pamoja kusambaza Vitakasa mikono na barakoa katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kupambana na maambukizi.
Akiwasilisha mada katika kikao hicho, Mtaalamu kutoka Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma Dkt. Tumaini Haonga aliwataka washiriki kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam ili jamii inayowazunguka ipate elimu sahihi.
"Sio kila mwenye homa na kukohoa anachukuliwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona lazima mshukiwa aonyeshe sifa za ziada ama awe amesafiri kwenda au kutoka nje ya nchi iliyo na maambukizi, amechangamana na watu walioambukizwa au kuwahudumia waathirika ndani ya siku 14 zilizopita" alisisitiza.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dkt. Naftali Ng'ondi amewataka maafisa hao kujiepusha na misongamano isiyo ya lazima ili kuepusha maambukizi katika maeneo yao.
"Kama ni kwenda sokoni, hakuna sababu ya kuandamana watu wanne wa familia moja na tunapokwenda sokoni twende kimkakati" alisema.
Aliongeza kuwa maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii wanawajibika kuwaelimisha wananchi juu ya madhara ya msongamano hasa kwa kipindi hiki wakati wa tishio la virusi vya Corona.
Mgonjwa wa kwanza aliripotiwa nchini Tarehe 16 Machi, 2020 na hadi sasa watu 13 wamethibitika kupata virusi vya Corona.
No comments:
Post a Comment