SERIKALI imeanza kuyaruhusu magari yaliyokwama katika Barabara Kuu ya Dodoma - Morogoro katika eneo la Kiyegeya, wilaya ya Kilosa kupita katika njia ya mchepuo ambayo imejengwa ili kupunguza msongamano mkubwa wa magari uliopo katika barabara hiyo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, wakati akisimamia hatua za ujenzi wa barabara hiyo ya mchepuo ambapo pamoja na mambo mengine amesema hadi sasa zaidi ya malori 60 yameshavuka katika barabara hiyo.
"Tumeanza kupitisha magari makubwa kupita katika barabara hii na yote yamepita vizuri kasoro yale ambayo kidogo yana hitilafu lakini tumejipanga tunayo mitambo ya kuvuta magari yote yatakayokwama katika njia hii", amesema Mhandisi Kamwelwe.
Waziri Kamwelwe amesisitiza kuwa hadi sasa pamoja na kuruhusu magari kupita magari yanayopewa kipaumbele ni magari madogo yote, magari ya abiria na malori yenye mizigo inayoharibika na yale yaliyobeba wanyama.
Kuhusu ujenzi wa kalvati la kudumu katika barabara hiyo, Waziri amefafanua kuwa kazi ya kurekebisha eneo hilo inaendelea na tayari taratibu za kujenga kalvati la zege imeanza ili kuunganisha na lile la awali pamoja na kujaza tuta ili kuwezesha magari mawili kupita kwa wakati mmoja.
"Eneo maalum la kutengenezea kalvati lipo katika hatua ya mwisho kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa inakamilisha ujenzi wa barabara hiyo na foleni inamalizika na hali ya usafiri inarejea kama awali" ameisitiza Waziri Kamwelwe.
Aidha, Waziri Kamwelwe amewataka wenye malori kuwa na nidhamu ya matumizi ya barabara kwani wasipofanya hivyo njia itajifunga na kusababisha msongamano mkubwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo Elius Mwakalinga, amesema kuwa Sekta yake inaendelea na zoezi la ukaguzi wa miundombinu ikiwa ni pamoja na kuainisha barabara na madaraja yote yaliyoathariwa na mvua na hivyo kuhitaji matengenezo ya haraka.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare, amesema kuwa ukamilikaji wa barabara hiyo ya mchepuo itasaidia sana kupunguza foleni iliyopo katika upande wa Morogoro na Dodoma kwani magari yamesimama hadi kilometa 20 kuanzia eneo la Kiyegeya.
"Magari yamezidi kuwa mengi na sisi kama Mkoa ni jukumu letu kuhakikisha usalama wa wananchi wanaosafiri pamoja na wasafirishaji unaimarishwa kwa hali ya juu", amefafanua Mkuu wa Mkoa huyo.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Tanzania, Fortunatus Muslim, ametoa wito kwa madereva kuwa wavumilivu katika kipindi hiki pamoja na kufuata maelekezo ya askari barabarani wanapowaongoza ili kuepuka kufunga barabara.
Ujenzi wa barabara hiyo ya mchepuo ni agizo lililotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, alipotembelea na kuzungumza na wasafiri na wasafirishaji waliokwama katika eneo la Kiyegeya kwa muda wa siku 5.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment