Na Shamimu Nyaki – WHUSM, Zanzibar
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimepongeza Baraza la Kiswahili Tanzania pamoja na Baraza la Kiswahili Zanzibar kwa kazi kubwa waliyofanya katika kuandaa waraka wa ushawishi wa kuingiza kiswahili kama moja ya lugha rasmi ya mawasiliano katika nchi za SADC.
Pongezi hizo zimetolewa katika kikao cha ushirikiano baina ya Wizara zenye dhamana ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kati ya Serikali ya Jamahuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ngazi ya Makatibu Wakuu kilichofanyika Zanzibar Machi 03, 2020.
Akizungumza katika kikao hicho ngazi ya Makatibu Wakuu Mwenyekiti ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bw. Saleh Yusuf Mnemo amesema kuwa BAKITA na BAKIZA zimefanya juhudi kubwa katika kukuza lugha ya Kiswahili ambayo ni nguzo muhimu katika kudumisha muungano wetu.
“Mabaraza haya mawili yanafanya kazi kubwa sana katika kukuza lugha yetu ya Kiswahili ni lazima tuyapongeze lakini ni vizuri yakaendelea kushirikiana katika kuelimisha watanzania matumizi mazuri na sahihi ya lugha hiyo ili iendelee kuwa miongoni mwa lugha bora duniani,” alisema Bw. Saleh Yusuf.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi ameyataka mabaraza hayo kuendelea kutafuta nama bora zaidi ya kukuza lugha hiyo nje ya nchi kwa kutumia fursa za uhitaji wa watalaam wa lugha hiyo zinazojitokeza kwakua tayari ina kanzidata ya watalaamu hao.
“Sekta hizi zina umuhimu mkubwa katika Muungano wetu ni vizuri wakuu wa idara na taasisi kuwa na utaratibu wa kukutana angalau mara moja kwa mwaka ili kujadili utekelazji wa maazimio ya maeneo ya ushirikiano pamoja na kutatua changamoto ambazo zinajitokeza kabla mamlaka za juu hazijafanya hivyo,” alisema Dkt. Possi.
Hata hivyo sekta hizo zimeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali ambapo zimefanikiwa kuandaa na kushiriki tamasha la JAMAFEST 2019 lililofanyika jijini Dar es Salaam na matamasha mengine kama ZIFF, SIFF pamoja na Sauti za Busara ambayo yanaendelea kuimarisha muungano.
Kikao hicho cha ngazi ya Makatibu wa Wakuu ni maandailizi ya kikao cha Mawaziri wanaosimamia sekta hizo kitakachokuwa na lengo la kupitia utekelezaji wa maazimio ya maeneo ya ushirikiano waliyotiana saini mwezi julai 2019 Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment