WANAWAKE SINGIDA WATOA YA MOYONI, RC DTK. NCHIMBI AWAPA UJASIRI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 19 February 2020

WANAWAKE SINGIDA WATOA YA MOYONI, RC DTK. NCHIMBI AWAPA UJASIRI

 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi katikati mwenye miwani akiwa na baadhi ya washiriki wa Kongamano la Wanawake Kanda ya Kati, lililofanyika Singida juzi.
 Baadhi ya washiriki kutoka mikoa ya Tabora, Dodoma na Singida wakisikiliza mada mbalimbali kwenye Kongamano la Wanawake Kanda ya Kati, lililofanyika mkoa wa Singida.
 Kongamano la Wanawake likiendelea.
 Wanawake wakiwa kwenye kongamano hilo.
 Wakina baba wakijumuika kwenye kongamano hilo.
 Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Singida, Jonathan Semiti akiwasilisha mada katika kongamano hilo.
Mshiriki wa Kongamano hilo Stela Mwenigoha kutoka Faraja Centre akichangia.
Na Godwin Myovela, Singida
WAKIWASILISHA hali halisi ya takwimu za vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini kwa kati ya mwaka 2016/18, Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, John Mapunda na Juliana Ntukey kwa nyakati tofauti, kupitia Kongamano la Wanawake kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani mkoani hapa jana, walisema vitendo hivyo vinazidi kuongezeka.
2016 idadi ya matukio ukatili wa kijinsia na unyanyasaji yaliyoripotiwa yalikuwa 31,996 na ilipofika 2018 yaliongezeka na kufikia 43,487 huku mikoa 6 iliyoonyesha kukithiri kwa matukio hayo ikiwa Dar es Salaam, Morogoro, Singida, Dodoma, Tanga na Arusha.
Kwa mujibu wa takwimu 2016 Temeke (4, 101), Morogoro (3,073), Singida (2,567), Arusha (2,890) na Tanga (1,904), huku mwaka uliofuata 2017 Kinondoni iliongoza kwa matukio (7,854), Dodoma (3,927), Temeke (3,163), Singida (2,890) na Arusha (2,790).
Mwaka 2018 mkoa ulioongoza kwa matukio ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji ulikuwa Kinondoni (5,386), Temeke (3,999), Arusha (3, 904), Tanga (3,252), Dodoma (1,882).
Huku idadi ya watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia katika kipindi hicho ikiongezeka kutoka (10, 551) mwaka 2016 hadi kufikia (14, 491) mwaka 2018. Takwimu zinaonyesha idadi hasa ya watoto wa kike ni kubwa na imekuwa ikiongezeka mwaka hata mwaka, ilinganishwa na wale wa kiume.
“2016 watoto wa kike walioripotiwa kufanyiwa ukatili walikuwa 8, 496 huku wa kiume wakiwa 2, 055, mwaka 2017 wakike walikuwa 9,810 wakiume wakiwa 3647, na mwaka 2018 watoto wa kike walikuwa 11, 789 huku wa kiume wakiwa 2, 702,” anasema Mapunda.
Baada ya takwimu hizo kuwasilishwa wanawake walipata fursa ya kuchangia, ambapo pamoja na mambo mengine, imeshauriwa kuanzishwa kwa vikundi huru vya wanafunzi kwenye maeneo ya shule ambavyo vitasimamiwa na walimu wa shule husika (clubs).
Lengo la vikundi inaelezwa kuwa itakuwa ni kupeana elimu  na kuhamasishana juu ya masuala yote yanayohusu ukatili na hatua zinazopaswa kuchukuliwa punde tu tukio hilo linapojitokeza miongoni mwa mtoto yeyote.
Kupitia Kongamano hili linalofadhiliwa na Mfuko wa Ruzuku kwa Msaada wa Kisheria (LSF) chini ya uratibu wa shirika la SEMA lenye makao yake makuu mkoani hapa, imebainika wazi kwamba watoto wengi kwa sasa wameonekana kubakwa na wengine kulawitiwa kwa siri wakiwa majumbani na mashuleni, na hutishiwa na wahalifu kwamba wasiripoti popote.
Watoto wanaendelea kukaa kimya wakiteseka ndani kwa ndani kwa maumivu makali-hatimaye inapita mda mrefu-hana wa kumweleza,  mzazi yupo ‘bize’ na shughuli za maisha, hana hata mda wa kumsikiliza mtoto.
“Kwa kukosa uhuru na wazazi wao wa kuwaeleza matatizo yanayowapata wahanga wengi wamegundulika kuwa wamebakwa na kulawitiwa baada ya mda mrefu kupita,” alisema Stela Mwenigoha mmoja wa washiriki wa sherehe za maadhimisho ya siku ya Wanawake, kupitia Kongamano hili la Wanawake wa Kanda ya Kati.
Pia Kamati za ulinzi wa mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto, wazee, wanawake na wenye ulemavu kuanzia ngazi ya taifa hadi vijiji zimeonyesha kufanya kazi kwa kusuasua kutokana na ufinyu wa bajeti, huku nyingi zikiwa zimekufa na hakuna tija yoyote katika utendaji wake hali inayozidisha idadi ya matukio ya ukatili kwa watu kufanya chochote bila hofu, hasa maeneo ya vijijini.
“Mtoto anabakwa hadi anakuja kujulikana unakuta tayari ana mimba ya miezi sita, kiukweli inasikitisha wazazi hawapo kabisa karibu na watoto wao, na hata hizo kamati kuna nyingine zinafanya kazi zinaibua matukio lakini hakuna kinachoendelea,” anasema Mwedinuu Kassim.
Huku katika hilo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, ambaye ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa Kongamano hilo la Kanda ya Kati, anaagiza Makatibu Tawala wote wa Singida, Dodoma na Tabora wahakikishe wanazifufua kamati hizo za ulinzi wa mtoto, na ndani ya miezi mitatu  watoe taarifa za hatua kwa hatua juu ya utekelezaji wa mpango wake.
Aidha, kuwepo na mpango mkakati kila kota, kwa kila mkoa, ambapo tutapata fursa ya kujadili takwimu za hali halisi ya matukio ya ukatili na mwelekeo, zinatolewa na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, kwa lengo la kuangalia namna ya kupunguza matukio hayo.
Aziza Kamata, kutoka Hospitali ya Mkoa wa Singida anaweka wazi kwamba mtindo uliopo kwa sasa ni wazazi kuwaozesha watoto wa kati ya umri wa miaka 13 na 14 kwa tama ya mali, huku akisisitiza kwamba kinachoenda kufanyika kwenye ndoa hiyo ya utotoni ni ubakaji, na wengi wa watoto hao ni wanaomaliza darasa la saba.
Salome Gabrieli kutoka Tabora anamweleza Mkuu wa Mkoa, Rehema Nchimbi kuwa “watoto wa sasa wanalelewa na Televisheni na wahudumu wa majumbani (house girls) akinamama wengi hawatimizi wajibu wao hali inayotia hofu juu ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika muktadha wa Tanzania ya kesho kimaadili,”.
 Aidha, katika hoja ya jukumu la mwanamke katika ulinzi wa mazingira na upatikanaji wa maji safi na salama, suala linalojitokeza hapa ni kwamba ili kulinda mazingira kikamilifu basi ni vema serikali ikaangalia namna bora ya kushusha bei ya gesi ya kupikia majumbani ambayo huuzwa kwa kati ya sh 48 na 160.
Bei ya gesi bado sio rafiki sana kuwezesha mazingira yetu kuendelea kuwa hai, wanawake wataendelea tu kukata miti, wataendelea kutumia mkaa na kutumia kuni kama gharama ya gesi haitapungua, wanawake wengi hasa waishio vijijini hushindwa kuimudu.
“Naiomba serikali ishushe bei ya gesi ili twende sambamba na kampeni yetu ya mkoa wa Singida kikamilifu inayoongozwa na mama yetu Nchimbi ya ‘Achia shoka kamata Mzinga’,” anasema mshiriki wa Kongamano hilo, Ana Mwahole, kutoka Dodoma.
Awali, Dkt. Nchimbi akifungua kongamano hilo lililobeba kauli mbiu ya ‘Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya sasa na ya baadaye’ hasa akizungumzia dhana ya usawa wa kijinsia, anasema Mungu hakumuumba mwanamke na mwanaume ili watengane hapana!.
“lengo hasa ni kuwa wamoja, kushirikiana, kulea familia pamoja na huo ndio usawa wenyewe wa kijinsia- uwe ni usawa ambao utaonyesha kuthamini uumbaji wa Mungu, uwajibikaji wa pamoja na kwa kutumia miundombinu ya pamoja,” alisema Dkt. Nchimbi.
Kuhusu mwanamke katika utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji, anawataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha jamii haikumbwi na mafuriko yanayotokana na sababu za kibinadamu, jamii haikati miti na kuchoma mkaa, badala yake jamii sasa iende na kampeni ya ‘achia shoka kamata mzinga’.
“Tufuge nyuki, nyuki ana faida kubwa sana, utavuna asali, nta na mazao mengine, pia asali ni lishe, ni tiba, kipato na ni ajira-achia shoka sasa kuokoa mazingira na vyanzo vya maji sote tukamate mzinga,” alisema Nchimbi.
Kuhusu fursa mbalimbali za uongozi kwa mwanamke,  hasa mwaka huu taifa linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, Mkuu wa Mkoa anawataka wanawake kujikubali, kujiamini wasiwe na hofu na badala yake wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali huku akisisitiza ‘wanawake tunaweza’.
“Naomba tutoke hapa na azimio la kumuunga mkono mwanamke mwenzetu yeyote tunayeona anafaa, ni lazima tutengeneze nguzo na misingi ya usawa wa kijinsia ya kuwa na wanawake wengi ndani ya uongozi sio tu kwa idadi bali pia kwa ubora,” anasema mama Dkt. Nchimbi.

No comments:

Post a Comment