Na Mwandishi Wetu,Monduli
Wajasiriamali wilayani Monduli mkoani
Arusha wametakiwa kuboresha vifungashio pamoja na ubora wa bidhaa zao ili
ziweze kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika Maonyesho ya Ubunifu,Ujasiriamali
na viwanda vidogo yaliyoandaliwa na
shirika lisilokua la kiserikali la Okoa New Generation ,Afisa Mipango wa Wilaya
ya Monduli Colex Mwakyelu alisema kuwa wajasiriamali wakiboresha bidhaa zao
wanaweza kupata masoko ya nje na kuepuka utegemezi wa masoko ya ndani.
Aliwataka wajasiriamali kuboresha
vifungashio na kuzitangaza bidhaa zao katika maonyesho makubwa yanayofanyika
ili kupata fursa za masoko na kunufaika kiuchumi.
Mkurugenzi wa shirika lisilokua la
kiserikali la Okoa new Generation ,Neema Robert amesema kuwa maonyesho hayo
yanalenga kuwapatia fursa za kimasoko pamoja na mafunzo ya wajasiriamali ambayo
wamekua wakiyatoa katika majukwaa ya vijana yaliyoko katika wilaya hiyo.
Neema aliwataka vijana kutumia fursa
zinazowazunguka kubadilisha maisha yao kwa kuwa wathubutu na wabunifu ili
waweze kufanikiwa kiuchumi .
"Vijana wanapaswa kujitoa kufanya
shughuli za kujitolea na uzalishaji Mali badala ya kusubiri ajira wakati
wanaweza kutengeneza fursa kwa kuamua kujitolea kwanza" Alisema Neema
Kwa upande wake Mmoja wa washiriki wa
maonyesho hayo Neema Saidi alisema kuwa kupitia maonyesho hayo yamekua fursa ya
kupata wateja na kujifunza kupitia wafanyabiashara wengine juu ya ubunifu na
uboreshaji wa bidhaa.
No comments:
Post a Comment