Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akijibu maswali Bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 3 Februari 2020.
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet
Hasunga (Mb) amesema kuwa njia pekee ya kumkomboa mkulima ni kuondokana na
kilimo cha kujikimu badala yake kuwekeza katika kilimo cha kibiashara.
Waziri Hasunga ameyasema hayo
Bungeni Jijini Dodoma jana tarehe 3 Februari 2020 wakati akijibu hoja za
wabunge mbalimbali walizozitoa wakati wa bunge la kumi na nane.
Katika kuimarisha sekta ya
kilimo tayari wizara ya Kilimo imeanza kutoa elimu kupitia wataalamu mbalimbali
kuhusu umuhimu na ulazima wa kusimamia tija katika kilimo pamoja na kuongeza
uzalishaji wa mazao.
Mhe Hasunga amesema kuwa ili
kuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo tayari serikali imeanza
kuchukua hatua za makusudi ambazo ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa ndani wa
mbegu.
Kwa mujibu wa takwimu
alizozitoa Mhe Hasunga amesema kuwa uhitaji wa mbegu nchini ni Tani 187,500
lakini mbegu zilizopatikana katika msimu wa kilimo wa 2019/2020 ni Tani 71,207
ambapo kati ya mbegu hizo Tani 66,033 sawa na asilimia 93% zimezalishwa nchini.
Amesema kuwa mbegu
zilizoingizwa kutoka nje ya nchi ni Tani 5,175 sawa na asilimia 7% tu ya mbegu
zote zilizopatikana hapa nchini ambapo kiasi hicho kinachoagizwa nje ya nchi ni
kiasi kidogo ukilinganisha na kinachozalishwa nchini.
Amesema kuwa matumizi ya
mbegu mpya kwa wakulima ni madogo sana ukilinganisha na mahitaji jambo hilo
linasababishwa na wakulima kuendelea kutumia mbegu za asili badala ya mbegu
mpya na bora. Ambapo amesihi wakulima kuhakikisha kuwa wanaachana na matumizi
ya mbegu za asili badala yake kutumia mbegu mpya.
Waziri Hasunga amesema kuwa
serikali inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli inaendelea na juhudi
zake za kuimarisha uzalishaji wa mbegu ili kuhakikisha kuwa Taifa linakuwa na
uwezo mkubwa wa kuzalisha mbegu wakati wa kiangazi kwa kuimarisha skimu za
umwagiliaji.
Hasunga amezitaja hatua
zingine zinazoendelea kuchukuliwa na serikali kuwa ni pamoja na kuimarisha
upatikanaji wa mbolea kwa wingi zenye bei nafuu na kwa wakati ambapo hata hivyo
mahitaji ya mbolea yameongezeka kwa kiasi kikubwa kwa kuwa wakulima wengi
wamejitokeza na kuwekeza katika kilimo.
Amesema kuwa mahitaji ya
mbolea nchini ni Tani 586, 000 kwa mwaka lakini upatikanaji mpaka kufikia
Februari 3, 2020 ni Tani 454,339 ndizo zilizopatikana ambapo kati ya hizo zipo
mbolea za kupandia DAP ambazo ni Tani 71,000 mbolea ya kukuzia UREA Tani
100,021.
Amesema kuwa aina zote za
mbolea zinapatikana nchini isipokuwa aina moja ya mbolea ya UREA zilizopungua
ambapo tayari Tani 43,000 zipo bandarini na Tani 222,000 zimeagizwa na
zinatarajiwa kuwasili hivi karibuni.
Waziri Hasunga aliongeza kuwa
lengo la kuagiza mbolea hizo nyingi ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na mbolea za
kutosha ili ziweze kuuzwa kama nguo zinavyouzwa madukani.
Akihitimisha hoja hizo Waziri
Hasunga amesema kuwa sekta ya Kilimo inachangia kwa asilimia 28.7% kwenye Pato
la Taifa, inachangia asilimia 65% mpaka asilimia 75% ya ajira mbalimbali ambazo
watu wameajiriwa, Inachangia kwa asilimia 66% katika malighafi za viwandani
huku ikichangia kwa ailimia 100% katika chakula chote kinachopatikana nchini pamoja
na lishe.
Kadhalika amesema sekta ya
kilimo inachangia kwa asilimia 30% ya fedha zote za kigeni.
No comments:
Post a Comment