| Mkuu wa Chuo Kikuu cha Leadimpact, Askofu Mkuu Dk. Cletus Bassay DD akizungumza kabla ya kuwatunuku Shahada ya Uzamivu ya Heshima wanamaafali hao. |
CHRISTINA Onyango, askari polisi wa kike katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, na mwasisi wa wazo la kuanzisha kituo cha huduma za pamoja kwa waathitrika wa ukatili wa kijinsia katika Hospitali ya Amana, ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Leadimpact cha Colorado, Marekani.
Kutokana na hatua hiyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema Jeshi hilo limeipokea heshima hiyo kwa mikono miwili na kwa heshima kubwa.
“Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam tumeichukulia Tuzo ya Heshima ya Udkatari wa Falsafa ya Heshima kwa uzito mkubwa. Utumishi wake uliotukuka ndio umefanya chuo kikuu cha kimataifa (Leadimpact) kumpaisha na kwa kweli, hata sisi ametupaisha. Polisi tutaendelea kutambua na kuenzi heshima hii aliyotuletea…” alisema Kamanda Mambosasa.
Baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Dk Christina Onyango alisema analipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kuwa tuzo hiyo ni matokeo ya malezi bora ya polisi nchini kwa watumishi wake.
Wengine waliopewa tuzo hiyo ya tabia za binadamu na utamaduni (utu) maarufu PhD in Humanity jijini Dar es Salaam ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Jumaa Mhina na baadhi ya viongozi wa dini wakiwamo kutoka Kenya, Botswana Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania.
Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe hiyo, Askofu John Bagenyeka, alisema: “Tuzo hii ya shahada ya uzamivu ya heshima katika humanity, hupewa watu waliofanya mambo ya kibinadamu kusaidia wengine kwa kiwango kisicho cha kawaida; waliojitoa sana kuliko wajibu wao, hasa kwa kusukumwa na wito.”
| Mmoja wa wanandugu wa Dk. Christina Onyango akimpongeza mara baada ya kupokea cheti cha heshima hiyo. |
Akaongeza: “Upekee wa huyu ni kwamba ni askari mwanamke mwenye ajira, majukumu na mashahara wake, lakini amejitoa sana kusaidia waathirika wa ukatili wa kijinsia na kutoa elimu hata kwa viongozi wa dini na makundi mbalimbali; hata makanisa na amekuwa akifuatilia sana kuona waathirika wanasaidiwa ipasavyo…, watu wajue wajibu mkubwa walio nao katika kuwalinda watoto na kupambana dhidi ya ukatili…”
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Leadimpact, Askofu Mkuu Dk Cletus Bassay DD katika barua yake ya anuari 16, mwaka huu kwa Christina mintarafu tuzo hiyo anasema: “Kwa niaba ya Bodi ya Chuo Kikuu cha Leadimpact USA, ninakuandikia kukupongeza kwa kuteuliwa kupokea shahada ya Udaktari wa heshima katika tabia za binadamu na utamaduni (humanity).
Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WilDAF) Tanzania, Anna Kulaya, alisema: “Christina ni miongoni mwa askari polisi wanaojitoa kwa hali na mali kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto na kulinda hjaki za binamadamu; kwa kweli, anastahili sana na Tanzania tungepata watu wengi kama Christina katika hili, ukatili wa kijinsia huenda ungekoma.’
Kwa mujibu wa uchunguzi, miongoni mwa mambo yaliyokifanya Chuo Kikuu cha Leadimpact kumpa tuzo hiyo, ni pamoja na namna alivyojitoa kutetea haki za binadamu hasa ulinzi wa haki za mtoto na kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

No comments:
Post a Comment