BAHATI NASIBU YA VISA: IFAHAMU VISA AMBAYO SERIKALI YA MAREKANI IMEIZUIA KWA WATANZANIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday 1 February 2020

BAHATI NASIBU YA VISA: IFAHAMU VISA AMBAYO SERIKALI YA MAREKANI IMEIZUIA KWA WATANZANIA




Takribani visa 50,000 hutolewa na Marekani kwa bahati nasibu kila mwaka.

IJUMAA Januari 31, 2020 utawala wa rais Donald Trump wa Marekani ulitangaza kuizuia Tanzania kushiriki katika bahati nasibu ya visa nchini Marekani. 

Hatua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na wengi wakijiuliza bahati nasibu hiyo ikoje na Watanzania wangapi hunufaika nayo kila mwaka.

Bahati nasibu hiyo ilipitishwa kisheria nchini Marekani mwaka 1990 na bahati nasibu ya kwanza ikafanyika mwaka 1995.

Toka wakati huo, takribani watu 50,000 kila mwaka kutoka nchi mbalimbali duniani hushinda bahati nasibu hiyo na kupata visa ya kuingia Marekani na kufanya kazi kama mkaazi wa kudumu.

Washindi wa visa hiyo pia huweza kuhamia nchini humo na wenza wao pamoja na watoto walio chini ya umri wa miaka 21.

Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, katika kipindi cha miaka 10 kutoka 2008 mpaka 2017, jumla ya Watanzania 643 walishinda bahati nasibu hiyo.

Katika kipindi hicho, mwaka ambao Watanzania walishinda wengi zaidi ilikuwa 2009 watu 137 na mwaka ambao walishinda wachache ilikuwa mwaka 2014 watu 28.

Zaidi ya Watanzania 10,000 hutuma maombi ya kushiriki bahati nasibu hiyo.

Kwa mwaka 2017 pekee, Watanzania 13,733 walituma maombi, kati yao 6,919 waliingia kwenye kinyang'anyiro na mwishowe walioshinda bahati nasibu walikuwa 46.

Hata hivyo, ushiriki na ushindi wa Watanzania ni mdogo ukilinganisha na baadhi ya mataifa nchini Afrika.

Sudan nayo ambayo imepigwa marufuku kama Tanzania katika kipindi hicho cha mwaka 2008-2017 raia wake 8,127 walishinda bahati nasibu hiyo.

Majirani wa Tanzania nchi ya Kenya katika miaka 10 hiyo imeshuhudia raia wake 15,172 wakishinda bahati nasibu hiyo.

Kwa mwaka 2017 pekee, Wakenya 360,023 walituma maombi, kati yao 249,397 waliingia kwenye kinyang'anyiro na mwishowe walioshinda bahati nasibu walikuwa 1,014.

Kushiriki bahati nasibu hiyo kuna masharti makuu mawili.

Sharti la kwanza ni kuwa nchi yako iwe miongoni mwa nchi zinazoruhusiwa kushiriki bahati nasibu hiyo.

Sharti hili ndilo ambalo litakalowazuia Watanzania kwa sasa. Hata hivyo kuna njia mbili za kuliepuka.

Njia ya kwanza ni kupitia uraia wa mume au mke wa muombaji.


Trump ameshaweka wazi msimamo wake dhidi ya bahati nasibu hiyo

Kwa Watanzania wenye wenza ambao ni raia wa nchi ambazo hazijapigwa marufuku kushiriki wao wanaweza kuendelea na bahati nasibu hiyo.

Pili, iwapo ulizaliwa katika nchi ambayo haijapigwa marufuku kushiriki bahati nasibu hiyo na endapo mzazi wako hakuwa raia wa nchi hiyo ama hakuwa mkazi halali wa nchi hiyo.

Sharti la pili ni kuhitimu elimu ya sekondari. Elimu ambayo kwa ujumla wake iwe imekuchukua jumla ya miaka 12 kuipata.

Unaweza kuliepuka sharti hilo kama una uzoefu wa kazi wa wiki mbili (ndani ya miaka mitano iliyopita) katika fani ambayo inahitaji uisomee kwa miaka miwili ya kuisomea. Fani husika hutangazwa na Wizara ya Kazii ya Marekani.

Hata hivyo Trump ameshaweka wazi kuwa haiungi mkono bahati nasibu hiyo na mwaka 2017 aliliomba bunge libadili sheria na kuifuta.

Jumla ya nchi sita zimeingizwa kwenye marufuku mpya iliyotangazwa na utawala wa Trump.

Tanzania na Sudani wao wamefunguwi kushiriki katika bahati nasibu.

Nchi nyengine nne, raia wake wamepigwa marufuku kabisa kuomba viza za kuhamia Marekani.

Nchi hizo ni Nigeria, Eritrea, Myanmar na Kyryzstan.

Afisa wa ngazi ya juu nchini Marekani amesema kuwa nchi hizo sita zimeshindwa kufikia "kiwango stahiki cha ulinzi na kupashana taarifa".

"Nchi hizi, kwa sehemu kubwa, zinataka kutoa msaada lakini kwa sababu mbali mwali zimefeli kufikia viwango vya chini tulivyoviweka," Naibu Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani Chad Wolf amewaambia wanahabari Ijumaa, Januari 31.

Bwana Wolf amesema maafisa wa Marekani watakuwa tayari kushirikiana na nchi hizo sita ili kuimarisha matakwa ya ulinzi kwa nchi hizo ili iwasaidie kutoka kwenye listi hiyo.

Nchi hizo mpya zinaungana na nchi nyengine saba ambazo raia wake wamepigwa marufuku kuingia Marekani toka mwaka 2017.

Nchi hizo, nyingi zikiwa na raia wengi Waislamu ni Libya, Iran, Somalia, Syria, Yemen.

Aidha nchi za Korea Kaskazini na Venezuela pia zimo kwenye marufuku hiyo.

-BBC

No comments:

Post a Comment