WAZIRI HASUNGA: TUNATAKA MBEGU BORA ZA MAZAO YA KILIMO ZIZALISHWE NCHINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 24 January 2020

WAZIRI HASUNGA: TUNATAKA MBEGU BORA ZA MAZAO YA KILIMO ZIZALISHWE NCHINI


Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati alipofungua kikao kazi cha Menejimenti ya wizara, taasisi na bodi za mazao  zilizo chini ya wizara ya Kilimo tarehe 23 Januari 2020 jijini Dodoma. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza ulazima wa serikali kuzalisha mbegu za mazao ya kilimo nchini wakati alipofungua kikao kazi cha Menejimenti ya wizara, taasisi na bodi za mazao  zilizo chini ya wizara ya Kilimo tarehe 23 Januari 2020 jijini Dodoma.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati alipofungua kikao kazi cha Menejimenti ya wizara, taasisi na bodi za mazao  zilizo chini ya wizara ya Kilimo tarehe 23 Januari 2020 jijini Dodoma.

Na Revocatus Kassimba, Dodoma

WAZIRI wa Kilimo Japhet Hasunga ameagiza wataalam wa wizara na taasisi za wizara ya Kilimo nchini kutumia utaalamu na uwepo wa fursa nzuri ya umwagiliaji kuzalisha mbegu bora kwa matumizi ya wakulima.

Amesema kauli hiyo tarehe 23 Januari 2020 jijini Dodoma wakati alipofungua kikao kazi cha Menejimenti ya wizara, taasisi na bodi za mazao  zilizo chini ya wizara ya Kilimo.

Hasunga amesema Tanzania haina haja ya kutegemea mbegu za mazao toka nje wakati ina eneo linalofaa kwa uzalishaji la kutosha na wataalam wabobezi kwenye sekta ya uzalishaji mazao ya kilimo.

“Tunataka mbegu zizalishwe kipindi cha kiangazi kupitia kilimo cha umwagiliaji, ili wakati wa mvua wakulima wapande wala sio muda wa kuzalisha mbegu” alisema Hasunga

Waziri Hasunga ametoa takwimu kuwa kwa sasa Tanzania inatumia tani 186,000 za mbegu ambapo uzalishaji ndani ya nchi ni chini ya tani 71,000 kwa mwaka hali inayosababisha kuendelea kutegemea mbegu zinazozalishwa nje.

Ameitaja changamoto ya upungufu wa mbegu za miche ya chai, korosho, michikichi, kahawa, mihogo  na jamii ya mikunde hivyo kuchangia ukuaji mdogo wa tasnia za mazao hayo.

Waziri huyo wa kilimo aliwaambia watendaji na watalaam wa wizara yake kuwa tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kuwa nchi iwe na mkakati maalum wa kuongeza uzalishaji kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji.

Hasunga amesema katika kutekeleza agizo la Rais Magufuli, wizara yake tayari imeagiza taasisi zake kutumia fursa ya umwagiliaji kuongeza uzalishaji mbegu nchini.

Amesema Tanzania ina eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji hekta milioni 29.4 ambapo zinazomwagiliwa hadi sasa ni hekta 475,000 tu hivyo wataalam wahakikishe mbegu zinazalishwa kwa wingi muda wote wa mwaka.

Wakati huo huo Waziri Hasunga ameonya dhidi ya kuongezeka kwa mbegu, mbolea na viuatilifu visivyo bora(fake) hali inayowaumiza na kusababisha hasara kwa wakulima nchini.

“Madawa na viuatilifu ambayo hayaruhusiwi kutumika yapo mengi sana. Hata mimi (Waziri) mwaka jana nilipigwa madawa yasiyo na ubora katika shamba langu Songwe na magugu hayakufa “ alitoa mfano Waziri Hasunga. 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Prof.Siza Tumbo amemhakikishia Waziri kuwa watendaji wa wizara na taasisi zake wataendelea kutekeleza maagizo ya serikali muda wote ili tija katika uzalishaji mazao nchini iongezeke.

Kikao hiki cha Menejimenti ni cha nne tangu Waziri Hasunga alipoteuliwa kuongoza wizara hiyo mwaka 2018 ambapo taarifa za utendaji kazi hujadiliwa pamoja na kuweka mpango wa utekelezaji kwa nusu ya pili ya mwaka 2020 iliyobakia.

Wizara ya kilimo ina bodi za mazao na taasisi zinazojitegemea jumla 22 ambapo wakurugenzi wakuu na wenyeviti wake wa bodi  wote wanashiriki kikao hiki cha Waziri wa Kilimo mwaka huu.

No comments:

Post a Comment