WANANCHI WA NYANDA ZA JUU KUSINI CHANGAMKIENI FURSA ZA UTALII - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 13 January 2020

WANANCHI WA NYANDA ZA JUU KUSINI CHANGAMKIENI FURSA ZA UTALII

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Serengeti Rebeka Msambusi  akiongea na waandishi wa habari wa mikoa ya Mbeya na Iringa juu ya fursa za kiutalii zinavyokuza uchumi wa mwananchi moja moja na jamii kwa ujumla.

Paulina Boma mfanyabiashara wa Mugumu Serengeti akizungumza waandishi wa habari mikoa ya Mbeya na Iringa juu ya fursa za kiutalii zinavyokuza uchumi wa mwananchi moja moja na jamii kwa ujumla.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Serengeti Rebeka Msambusi  akiongea na waandishi wa habari wa mikoa ya Mbeya na Iringa juu ya fursa za kiutalii zinavyokuza uchumi wa mwananchi moja moja na jamii kwa ujumla.


NA FREDY MGUNDA, IRINGA.

WANANCHI wanaozungukwa na hifadhi za taifa wametakiwa kutumia fursa za kiuchumi ambazo zinapatikana katika hifadhi hizo ili kuleta maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.

Akizungumza waandishi wa habari mikoa ya Mbeya na Iringa Paulina Boma mfanyabiashara wa Mugumu Serengeti alisema kuwa amefanikiwa kupata mafanikio mengi kutokana na biashara ya bidhaa za kitalii katika hifadhi ya taifa ya Serengeti.

“Nimefanikiwa kupitia uuzaji wa bidhaa za kitalii kwa kuwasomesha watoto wangu wane kwa ngazi ya chuo kikuu na wengine wanaendelea kusoma ngazi za chini za elimu ya sekondari,lakini pia nimewasidia vijana wengine kuwaongezea elimu kwenye vyuo mbalimbali kulingana na vipaji vyao” alisema Boma

Boma aliongeza kwa kusema kuwa kupitia biashara ya kuuza bidhaa za kitamaduni kwa watalii wanatembelea hifadhi hiyo amefanikiwa kujenga nyumba nne na amenunua gari kwa ajili ya shuguli zake binafsi na ndoto zake ni kuhakikisha anakuwa na kampuni ya utalii ambayo itamuongezea kipato na kuleta maendeleo kwa taifa kwa ujumla.

Aidha Boma aliwataka wananchi wa mikoa ambayo inazungukwa na hifadhi za taifa kuchangamkia fursa zilizoko kwenye hifadhi hizo ili kuleta maendeleo binafsi na taifa kwa ujumla.

“Kwenye hifadhi hizi kuna kila aina ya fursa za kibiashara ambazo zipo wazi kwa kila mtanzania anaweza kuzitumia hivyo watanzania wanatakiwa kuwa wabunifu tu,labda ukiangalia bidhaa nazoziuza hapa nazinunua katika mikoa ya nyanda za juu kusini,Iringa,Mbeya,Njombe na songwe na nakuja kuziuza huku hivyo hata wao wanaweza kuziuza kwa watalii wanaotembelea vivutio vya mikoa yao” alisema Boma

Lakini Boma aliwataka wanaume kuwaruhusu wanawake kufanya shughuli za kiamendeleo kwa kuwa wanauwezo wa kufanya kazi na kuongeza kipato kwenye familia hivyo ukimpa fursa mwanamke basi umeikomboa jamii kwa ujumla.

“Niwaombe wananchi wa nyanda za juu kusini waje huku kaskazini wajifunze shughuli hizi za kitamaduni ambazo tumekuwa tukiwauzia watalii mbalimbali na kupata faida ambayo imekuwa inaendesha maisha yangu vizuri na kuchangia maendeleo ya taifa” alisema Boma

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Serengeti Rebeka msambusi alisema kuwa utalii umesaidia kukuza uchumi kwa wananchi wa wilaya hiyo kutokana na kuuza bidhaa mbalimbali kwa watalii.

“Saizi wanauza vyakula mbalimbali kwenye hotel na kambi za kitalii ambazo zipo hifadhi ya taifa ya Serengeti na usafiri pia umechangia kukuza uchumi wa wananchi” alisema Msambusi

Msambusi aliwataka wananchi wa nyanda za juu kusini kuchangamkia fursa zilizopo katika hifadhi ya taifa ya Ruaha ili kukuza uchumi kama ilivyo katika mikoa ya kaskazini ambao wamekuwa wakitumia vizuri fursa ya utalii kwa kujipatia maendeleo.

Ikumbukwe kuwa  Hifadhi ya Ruaha ndiyo hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania ambapo ina ukubwa wa kilomita za mraba 20,226 na ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Afrika baada ya hifadhi ya Kafue iliyopo nchini Zambia.

Ni maarufu kwa kuwa na wanyama aina ya Kudu wakubwa na wadogo ambao hupatikana kwa wingi ambapo hustawi wa hifadhi hii unategemea mto ruaha ambao aina mbalimbali za Samaki, Mamba na viboko hupatikana katika mto huu.

Wanyama kama Pofu na swala hunywa maji katika mto huo wa Ruaha ambao ni mawindo makubwa ya wanyama wakali wakiwemo Simba, Chui, Mbweha, Fisi na Mbwa mwitu. Pia eneo hili Tembo hukusanyika kwa wingi kuliko eneo lolote la hifadhi zilizopo katika nchi za Afrika Mashariki.

Katika hifadhi hii utajionea Magofu yanayosadikiwa kuwa yalikuwa makazi ya watu wa kale katika Kijiji cha Isimila kiasi cha Kilomita 120 kutoka Iringa. Magofu haya ni miongoni mwa historia ya kale barani Afrika.

Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ili kuangaliwa wanyama wakubwa ni wakati wa kiangazi kuanzia Mei hadi Desemba, lakini kuangalia ndege na maua wakati wa masika ni Januari –April .


No comments:

Post a Comment