TAKUKURU KAMILISHENI UCHUNGUZI MAPEMA-MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 13 January 2020

TAKUKURU KAMILISHENI UCHUNGUZI MAPEMA-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiweka jiwe la msingi, wakati alipozindua jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jenerali John Mbungo, Januari 13, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikata utepe, wakati alipozindua jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, Januari 13, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Taasisi ya Kuzua na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ukamilishe mapema uchunguzi dhidi ya madudu yaliyoibuliwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 na wizi uliofanywa na viongozi wa AMCOS kwa wakulima wa ufuta na korosho ikiwemo wilaya ya Ruangwa.
Ameyasema hayo leo wakati akizindua jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Ruangwa lililogharimu zaidi ya sh. milioni 142. Ametoa wito kwa TAKUKURU kuwa imara na kuweza kutembea kifua mbele katika mapambano hayo.
Waziri Mkuu amesema  pamoja na TAKUKURU kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku pia ameuagiza uongozi wa taasisi hiyo ukamilishe mapema utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoyatoa kwao kwa nyakati tofauti.
Amesema ameshuhudia kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya kupitia uchunguzi na ufuatiliaji wa madai ya malipo ya wakulima wa zao la ufuta na korosho.“Kamilisheni chunguzi hizi zote kwa wakati ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wale wote waliopatikana na hatia.”
Amesema rushwa huathiri utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. “Kutokana na ukweli huo, Serikali imetoa msukumo wa pekee katika kushughulikia vitendo vya rushwa na ufisadi. Msukumo huo, umechangia kwa kiasi kikubwa hususan katika kipindi hiki, utekelezaji wa miradi mikubwa na ya kimkakati kwa ufanisi na kwa wakati.” 

Amesema wananchi wanatakiwa wafahamu kwamba kwamba nchi yoyote ambayo rushwa imetamalaki siyo rahisi kuwa na uwezo wa kiuchumi utakaoiwezesha nchi hiyo kumudu kulipa madeni ya ndani na ya nje. “Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania tunashuhudia jinsi Serikali ya awamu ya tano inavyolipa madeni.” 
Kwa mfano, kati ya Julai na Septemba, 2019, sh. bilioni 85.72 zimetolewa ikiwemo bilioni 50 za madai ya pensheni; bilioni 22 za madai ya watumishi wa umma ikiwemo kiinua mgongo kwa wastaafu 3,019 na malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 1,435; bilioni 10.24 zimelipa watoa huduma na zaidi ya bilioni 2 kwa ajili ya wakandarasi na wahandisi washauri. Hayo ni matokeo ya jitihada za kupambana na rushwa zinazofanywa na Serikali.

Amesema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, imekuwa ikijipambanua na vita dhidi ya rushwa na ufisadi. Hivyo, kitendo hicho cha kuendelea kulipa madeni ni ishara ya mafanikio ya Serikali katika jitihada zake za kuzuia na kupambana na rushwa nchini. Serikali itaendelea kudhibiti mianya yote ya rushwa katika utendaji mzima wa Serikali.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema tafiti za hivi karibuni zilizofanywa na wadau wa mapambano dhidi ya rushwa na Utawala Bora kama vile Transparency International (TI), MO Ibrahim na Afrobarometer zinaonesha kuwa kwa miaka mitatu mfululizo, yaani 2016 hadi 2018 Tanzania imeendelea kufanya vyema katika mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora. 
Amesema mafanikio hayo ya kujivunia ni jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kusimamia kwa dhati mapambano dhidi ya rushwa kwa usimamizi wa Taasisi ya Kuzua na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambayo ndicho chombo kilichopewa dhamana kisheria.  
“Tambueni kwamba uongozi mzima wa juu kabisa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu) uko pamoja nanyi katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi. 
Pia ameagiza kuanzishwa kwa vilabu vya kupambana na rushwa katika shule ili wanafunzi waweze kuwa na uelewa na kuweza kutoa taarifa za rushwa. 
Akizungumzia kuhusu jengo alilolizindia amesema muhimu sana kwa taasisi nyeti kama ya TAKUKURU kumiliki majengo yake yenyewe. Kuhusu hali ya majengo ya ofisi za TAKUKURU katika ngazi ya mikoa na hata wilaya, amemwagiza Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt Mary Mwanjelwa alishughulikie suala hilo.
Kwa upande wake,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo amesema jengo hilolimejengwa kwa muda wa miezi saba kuanzia tarehe 11/06/2018 na kukamilika tarehe 25/01/2019.Hadi kufikia hatua hii ya uzinduzi, jengo hili limegharimu jumla ya Sh. 142,857,142.86.”
Akizungumzia kuhusu uchunguzi kiongozi huyo amesema kwa kipindi cha mwaka 2019 TAKUKURU imefanya uchunguzi kwenye tuhuma kubwa ikiwemo ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Magufuli aliyoyatoa Jumanne Oktoba 15, 2019 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Ruangwa.

“Kupitia uchunguzi ule, tumebaini kwamba zaidi ya vyama 30 vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) vya Mkoani Lindiviliwadhulumu wakulima wa zao la ufuta kiasi cha zaidi ya sh.Bilioni sh. 1.23.  Kupitia uchunguzi huo tuliwakamata na kuwahoji zaidi ya viongozi 300 wa AMCOS zilizokuwa zinahusika katika dhuluma hii. Tulifanikiwa kuokoa zaidi ya sh. bilioni 1.042. Fedha hizi zilikuwa ni mali ya wakulima wa ufuta ambao walidhulumiwa fedha hiyo na Viongozi wa Vyama vya AMCOS.” 
Kadhalika Brigedia Jenerali Mbungoamesema pamoja na kufanikiwa kujenga majengo ya ofisi za TAKUKURU katika wilaya saba bado inakabiliwa na uhaba wa majengo ya kudumu ya ofisi. Amesema TAKUKURU ina jumla ya ofisi 28 za mikoa na ofisi 117 za wilaya huku mahitaji halisi ni majengo 28 kwa ofisi za Mikoa na majengo 117 kwa ofisi za wilaya. 
Naye, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt Mary Mwanjelwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuendeleza mapambazo dhidi ya rushwa, hivyo uzinduzi wa jengo hilo ni miongozi mwa harakati hizo.

No comments:

Post a Comment