Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali Bungeni jijini Dodoma, Januari 30, 2020. |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea
kukemea utendendaji usioridhisha pale inapoona mambo hayaendi sawa
katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na Zanzibar.
Amesema maagizo aliyoyatoa Jumamosi,
Januari 18, 2020, wakati alipotembelea kiwanda cha kuzalisha sukari cha
Zanzibar kilichopo Mahonda, wilaya ya Kaskazini ‘A’, mkoa wa Kaskazini
Unguja ni sahihi kwa kuwa yanalenga kuboresha maendeleo na kulinda
wawekezaji.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Januari 30, 2020) wakati
akijibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashimu Ayoub (BLW) katika kipindi cha
maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kufahamu
ni lini Serikali itaruhusu sukari inayozalishwa na kiwanda cha Sukari
Zanzibar iuzwe Tanzania Bara.
Amesema
alipofanya ziara katika kiwanda hicho, alikuta tani 3,200 zikiwa
hazijanunuliwa. “Nilipofika kiwandani hapo nilikuta sukari nyingi kwenye
bohari kwa madai kuwa imekosa soko. Ingawa mbunge amesema anahitaji
soko la Tanzania Bara lakini mahitaji ya sukari Zanzibar ni tani 36,000
kwa mwaka na kiwanda kinazalisha 6,000.”
Waziri
Mkuu amesema mpango wa uagizaji sukari kutoka nje ya nchi hauko sahihi
kwani wanunuzi walitakiwa kwanza wanunue sukari inayozalishwa ndani
ndipo waagize nje kiasi kinachopungua.“Haiwezekani
sukari inayozalishwa ndani ikakosa soko kutokana na uingizwaji wa
sukari kutoka nje. Hii inawavunja moyo wawekezaji wetu,” amesema.
Hivyo,
amesema yeye na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi
ndio wenye jukumu la kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM
na kwamba suala la viwanda limo katika utekelezaji wa ilani hiyo.
“Ninapokuta
Ilani haitekelezeki popote pale nchini lazima niwe mchungu, lazima
tuweke mpango wa kuwalinda wawekezaji wa ndani na kuwahakikishia masoko
na tunajua masoko hayo tunayo,” amesema.
“Pale
wapo waagizaji wa sukari watatu tu, sasa kwanini wasipewe masharti
rahisi ya kuanza kununua sukari ya ndani na kiasi kinachopungua ndio
waagize. Lazima tulinde viwanda vyetu… halafu mtu anasema nimewachefua
Wazanzibari. Hivi nimewachefua Wazanzibari ama nimewachefua wanunuzi?”
amehoji.
Amesema
sera ya nchi inasisitiza umuhimu wa kulinda wazalishaji wa ndani ambao
bidhaa zao zimethibitishwa na mamlaka husika. Hivyo, ni lazima kuwalinda
wawekezaji kwa kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika.
Waziri
Mkuu amesema viwanda vinasaidia katika kuondoa tatizo la ajira,
vinawapa wakulima soko la uhakika la mazao yao pamoja na Serikali kupata
kodi ya uhakika. “Kiwanda kile kimeajiri watu 400 na Serikali inapata
kodi zinazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.”
No comments:
Post a Comment