RAIS MAGUFULI AMTUMBUA WAZIRI KANGI LUGOLA, AFANYA MABADILIKO...? - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 24 January 2020

RAIS MAGUFULI AMTUMBUA WAZIRI KANGI LUGOLA, AFANYA MABADILIKO...?

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi akitangaza  mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam leo Alhamisi Januari 23, 2020.

RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesikitishwa na kitendo cha viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutia saini makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Euro Milioni 408.5 (sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 1) kutoka kampuni moja ya nchi za nje bila kufuata sheria.
Mhe. Rais Magufuli amesema ameshangazwa kuona viongozi hao wameingia makubaliano hayo ilihali zabuni hiyo haijapangwa kwenye bajeti wala kupitishwa na Bunge, huku kukiwa na mazingira ya ukosefu wa uadilifu kutokana na aina ya vifaa vilivyotajwa katika zabuni hiyo na viongozi hao kusafirishwa kwenda nchi husika kwa kugharamiwa na kampuni waliyokubaliana kusambaza vifaa hivyo.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Jacob Kingu kwa kuandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake ili kuwajibika kwa dosari hiyo, na amewashangaa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola na Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias Andengenye kutowajibika kwa dosari hiyo.
“Nakueleza Mhe. Lugola na Kamishna Jenerali Andengenye, ninawashangaa kuwaona mpo hapa, ninawapenda sana lakini huu ndio ukweli, sitaki kuwa mnafiki, shilingi Trilioni 1 na kitu mtu anasaini wakati sheria zote zinajulikana, mwenye mamlaka ya kukopa fedha ni Wizara ya Fedha pekee yake, wanajua, ikiwa hivyo basi kila wizara itakopa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema maafisa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliohusika kupitisha makubaliano hayo wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi akiwa msibani (alipofiwa na mkewe) pamoja na Maafisa wengine wa Wizara ya Mambo ya Ndani waliohusika katika kashfa hii wajitafakari.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 23 Januari, 2020 wakati wa sherehe za ufunguzi wa majengo 12 yenye makazi ya familia 172 za Maafisa na Askari Magereza katika Gereza la Ukonga Jijini Dar es Salaam.
Ujenzi wa majengo hayo umegharimu shilingi Bilioni 13 ambapo awali Mhe. Rais Magufuli aliagiza Jeshi la Magereza lipewe shilingi Bilioni 10 lakini baada ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) iliyopewa zabuni ya ujenzi kushindwa kumaliza kazi kwa miezi 27 wakiwa wamefikia asilimia 45 tu, aliagiza kazi hiyo ikabidhiwe kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao walipatiwa shilingi Bilioni 3 na kufanikiwa kukamilisha ujenzi huo kwa muda wa miezi 7.
Ameipongeza JWTZ kupitia JKT kwa kazi nzuri waliyoifanya katika ujenzi huo na ujenzi wa miradi mingine ikiwemo ukuta wa eneo la madini ya Tanzanite Mirerani Mkoani Manyara, kambi ya JWTZ Ngerengere Mkoani Morogoro na ujenzi wa Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.
Hata hivyo amelitaka Jeshi la Magereza kujirekebisha na kujifunza kutoka JKT kwa kuwa linayo nguvu kazi ya wafungwa takribani 13,000 ambao wanaweza kutumika katika uzalishaji mali na kujenga miundombinu ya jeshi hilo yakiwemo makazi ya Maafisa na Askari badala ya kusubiri kujengewa na majeshi mengine ama kutumia wakandarasi.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa kwake na kusuasua kwa ujenzi wa jengo la kiwanda cha kutengeneza viatu cha Gereza Kuu Karanga kilichopo Moshi Mkoani Kilimanjaro ambacho licha ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF (ambao ni wabia) kutoa shilingi Bilioni 9 tangu Oktoba 2019, hadi sasa Jeshi la Magereza limeshindwa kuharakisha ujenzi huo ambao umefikia asilimia 45 tu, ilihali mitambo inayopaswa kufungwa katika jengo hilo imeshawasili Bandari ya Dar es Salaam.
Amemuagiza Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Phaustine Kasike kuhakikisha majengo mapya 12 yaliyojengwa katika Gereza la Ukonga yanatunzwa na kuendeleza utaratibu wa kujenga nyumba za Maafisa na Askari wake pamoja na kukarabati zilizopo, kwa kuwa haridhishwi na hali duni ya makazi ya Maafisa na Askari Magereza hapa nchini.
Pia amemtaka CGP Kasike kuhakikisha maji yanaingizwa katika nyumba za makazi ya Maafisa na Askari Magereza katika majengo mapya 12 ya Ukonga, kwa kuwa wakati wa ukaguzi amebaini kuwa makazi hayo hayajaunganishwa na mtandao wa maji ndani ya nyumba.

No comments:

Post a Comment