Iran inasema mashambulio hayo ni hatua ya kilipiza kisasi mauaji ya kamanda wa jeshi lake Qasem Soleimani. |
Karibu kambi mbili za wanajeshi wa Marekani nchini Iraq zimeshambuliwa kwa makombora kadhaa, kwa mujibu wa idara ya ulinzi ya Marekani.
Runinga ya kitaifa ya Iran imetangaza kuwa shambulio hilo ni la kulipiza kisasi mauaji ya kamanda mkuu Qasem Soleimani aliyeuawa katika shambulio la ndege isiyokuwa na rubani mjini Baghdad, kufuatia agizo la rais wa Marekani Donald Trump. Pentagon inasema kuwa karibu kambi mbili zilishambuliwa, mjini Irbil na Al Asad. Bado haijafahamika kama kuna majeruhi wowote kutokana na shambulio hilo.
"Tunafahamu ripoti ya mashambulizi dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq. Rais amefahamishwa kuhusu tukio hilo na anafuatilia kwa karibu hali ikoje katika eneo hilo ili kushauriana na kamati ya kitaifa ya usalama," Taarifa ya msemaji wa ikulu ya White House, Stephanie Grisham.
Jeshi la ulinzi la Iran Revolutionary Guard limesema kuwa shambulio hilo ni la kulipiza kisasi kifo cha Soleimani cha Ijumaa iliyopita.
"Tunaonya washirika wote wa Marekani, ambao wameruhusu vikosi vya Marekani kuwa katika ardhi yao, kwamba wakijaribu uchokozi wa aina yoyote dhidi ya Iran yatalengwa," ilisema kupitia taarifa yake iliyotolewa shirika la habari la Iran, IRNA news agency.
Mashambulio hiyo yalifanyika saa kadha baada ya mazishi ya Soleimani. Shambulio la pili lilifanyika katika mji wa Irbil muda mfupi baada ya roketi ya kwanza kugonga Al-Asad, kituo cha televisheni cha Al Mayadeen kiliripoti.
Awali, rais Trump alisema kuwa hatua ya kuondoa vikosi vyake Iraq itakuwa na athari mbaya sana kwa nchi hiyo. Marekani ina karibu wanajeshi 5,000 nchini Iraq.
Uingereza imechukua hatua ya tahadhari kwa kuweka tayari manuari yake ya kivita na helikopta za kijeshi baada ya kuongezeka kwa hali ya taharuki mashariki ya kati, alisema waziri wa ulinzi Ben Wallace. Kuuwawa kwa Soleimani Januari 3 kulizorotesha uhusiano kati ya Iran na Marekani.
Jenerali Soleimani - alikuwa kiongozi wa oparesheni ya kijeshi ya Iran katika eneo la mashariki ya kati - lakini serikali ya Marekani ilimuona kuwa gaidi, ambaye alihusika na vifo vya mamia ya wanajeshi wake na kwamba alikuwa akipanga shambulio "hatari". Iran iliapa "kulipiza kisasi" kifo chake.
Bwana Trump, kwa upande wake, alionya kuwa Marekani itajibu jaribio lolote la kulipiza kisasi "pengine kwa njia kali zaidi".
"Alikuwa adui lakini sasa sio adui tena. Amekufa," Bwana Trump alisema, akitetea uamuzi wake.
"Alikuwa anapanga shambulio kubwa, shambulio hatari dhidi yetu. Sidhani mtu yeyote anaweza kulalamika kuhusiana na hilo."
Mamilioni ya raia wa Iran walijitokeza kwa mazishi ya kamanda huyo wa kijeshi, wakibeba mabango na kusema kwa sauti "kifo kwa America" na "kifo kwa Trump". Iran inaunga mkono makundi kadhaa ya wanamgambo wa kishia katika nchi jirani ya Iraq.
Siku ya Ijumaa, Soleimani alikuwa amewasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad na alikuwa katika msafara akiandamana na maafisa kadhaa wa makundi hayo, magari yao yaliposhambuliwa kwa makombora ya Marekani. Iraq sasa imejipata katika njia panda kwasababu Iran na Marekani ni washirika wake.
Maelfu ya wanajeshi wa Marekani wamekuwa nchini humo kusaidia katika mapambano dhidi ya wapiganaji wa kundi la Islamic State (IS) lakini serkali ya Iraq inasema hatua ya Marekani ilienda kinyume na makubaliano yao.
-BBC
No comments:
Post a Comment