BASHE AAGIZA DENGU, CHOROKO KUNUNULIWA KUPITIA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 30 January 2020

BASHE AAGIZA DENGU, CHOROKO KUNUNULIWA KUPITIA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI

Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ameagiza mfumo wa ushirika wa stakabadhi ghalani kuanza mara moja kutekelezwaji katika mikoa mitatu ya Mwanza, Shinyanga na Tabora, kwa ununuzi wa mazao ya dengu  choroko.
Aidha, Bashe, ameitaka tume ya maendeleo ya ushirika nchini, kuitisha kikao cha wadau wa kilimo kwa mikoa hiyo, kwa nia ya kutoa muongozo kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo wa Ushirika wa Stakabadhi Ghalani.
Agizo la Naibu Waziri huyo limetolewa katika kikao na wadau wa masuala ya ushirika, kwa mikoa hiyo, kilichofanyika mapema wiki iliyopota mjini Dodoma.
Naibu Waziri huyo pia alimuagiza Naibu Mrajis wa vyama vya ushirika nchini, Charles Malunde, kutembelea mikoa hiyo kukutana na wakuu wa mikoa pampja na kuzungumza na wadau, kwa nia ya kuliweka sawa jambo hilo.
Waziri Bashe, alisema serikali imebaini kuwapo kwa kasoro mwaka jana, kuzuia mfumo huo kwenye ununuzi wa mazao hayo, lakini pia aliamua kulifanyia kazi kwa kina na ndio maana amefanya haraka kutoa maelekezo hayo.
Naibu Waziri Bashe, alisema kuwa njia bora ya kumkwamua mkulima masikini wa kijijini ni kutumiwa kwa mfumo wa ushirika, ambapo wanunuzi hukutanishwa na kushindanishwa kwenye soko la pamoja.
“Kwa mfano wanunuzi wa dengu na choroko, hujitokeza na kuandikishwa na warajis waasaidizi, lakini pia mazao ya wakulima hukusanywa kwenye maghala makuu, ambapo mnada huitishwa na wanunuzi kila mmoja hujinadi kwa bei,” alisema
“Chini ya utaratibu huo na kwa usimamizi wa karibu wa wizara yetu kupitia tume ya maendeleo ya ushirika, wakulima hujikuta wakipata bei nzuri na hivyo kufikia malengo ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)  ya kumsaidia mkulima masikini,”  alisema Bashe
Alisema tayari wakulima wa mikoa hiyo walikuwa wakililia mfumo huo wa ushirika, huku wakihoji sababu za kuzuhiliwa mikoa ya kanda ya ziwa na kuruhusiwa mikoa ya kusini pekee.
“Ninachoweza kusema hapa ni kwamba, twendeni tukawasaidie wakulima kupitia mfumo wa stakabadhi ghaani, lakini pia serikali imejifunza kitu kutokana na hali hiyo,” alisema Waziri Bashe.
Aliongeza kusema kuwa kupitia mfumo huo wa ushirika, vyama vikuu vya ushirika vya Nyanza na Shirecu vitapata nguvu ya kujiendesha na pia kufikia malengo ya kufufua mitambo yao na viwanda vyao vya pamba.
Hata hivyo, alipotafutwa kwa niia ya simu kuhusu hatua waliyofikia baada ya agizo hilo la Waziri Bashe, Malunde, alisema kwa ufupi, Nitakupigia baadaye, lakini alipotafutwa tena hakupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi wa maandishi.
Meneja wa SHIRECU Ramadhan Hamis, alikiri kushiriki kikao hicho na kusema wao sasa wanasubiri maelekezo kutoka kwa tume hiyo ya ushirika, iweze kutekeleza maagizo ya Waziri.
“Kimsingi huku tupo tayari kwa ajili ya utekelezaj, hao tume waliambiwa waje kuongea na wakuu wa mikoa pamoja na wadau, kuhusu mchakato wa suala hilo, lakini tunaona mambo yako kimya,” alisema Hamis.
Mbali na kukutana na wadau hao, pia Waziri Bashe, aliiagiza tume hiyo kutoa tangazo kupitia vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa sheria ya ushirika na kuanza kutumiwa kwa mfumo huo kwa mazao ya dengu na choroklo kwa mikoa hiyo, lakini pia kuruhusu kutumika kwa mfumo kwenye maeneo mengine.
Mwenyekiti wa Tume ya Ushirika nchini Dkt. Titus Kamani, alieleza kufurahishwa kutokana na maamuzi ya Naibu Waziri Bashe, akisema hatua hiyo itasaidia kumuondolewa hasara mkulima, iliyokuwa ikisababishwa na walanguzi wa mazao vijijini waliokuwa wakitumiwa na makampuni yasiyohitaji ushirika.
Ushirika ndio sauti ya wakulima wanyonge na kwa kauli hiyo ya Waziri Bashe, tumefurahi kwamba tupo njia moja kwa nia ya kumsaidia mkulima huyu masikini, apate bei nzuri ya mazao yake, badala ya kuruhusu walanguzi kuendelea kuwalaghai huko vijijni.

No comments:

Post a Comment