SERIKALI inawahimiza wadau na jamii nzima kutunza, kulinda na kuhifadhi maeneo ya kihistoria ambayo yalitumika wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika ili historia hiyo isipotee na iweze kutumika kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza alisema hayo jana mkoani wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi siku mbili alipotembelea maeneo Dakawa na Mazibu yaliyotumiwa wapigania uhuru wa “African National Congress” (ANC) wa Afrika Kusini.
“Kazi ya kulinda, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa Ukombozi wa Afrika uliopo Tanzania ni jukumu la jamii nzima, mashirika ya umma na watu binafsi ili kuthamini na kuenzi urithi huu muhimu wa Afrika” alisema Naibu Waziri Shonza.
Ili kutunza na kuhifadhi maeneo, nyaraka, vifaa na vielelezo vingine vilivyotumiwa na Wapigania uhuru, Serikali kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeanzisha Programu ya uhifadhi na uendelezaji wa historia ya Ukombozi wa Afrika ambayo pamoja na mambo mengine;inalenga kuthamini na kuenzi mchango wa Tanzania katika kuongoza harakati za mapambano ya kudai uhuru.
“Tunawashukuru sana wenzetu wa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuendelea kutumia na kuhifadhi maeneo haya, tumeona pamoja na kwamba yalitumika katika harakati za ukombozi, lakini kimsingi miundombinu mikubwa imebaki ikiwemo shule za msingi na sekondari, zahanati pamoja na vyuo katika maeneo yote ya Dakawa na Mazimbu ambayo yanaendelea kuhifadhiwa na kutumika ili kuhakikisha historia hii haipotei” alisema Naibu Waziri Shonza.
Aidha, aliwasisitiza na kuwahimiza Watanzania kutumia fursa ya kuwepo kwa utajiri huo wa kihistoria kwa kuya tembelea maeneo hayo wakiwemo wanafunzi wa ngazi za shule ya msingi, sekondari, vyuo vya kati pamoja na vyuo vikuu ili kujifunza historia hiyo sio tu kwa nadharia, bali kwa kujionea maeneo halisi pamoja na vifaa vilivyotumiwa na wapaingania uhuru hao.
Kwa upande wa eneo la Dakawa, upo utajiri mkubwa wa kihistoria ambao una manufaa kwa vijana na Watanzania kwa ujumla. Eneo hilo lina taasisi tano ambazo zinatumika hadi sasa ikijumuisha; shule ya msingi na shule ya sekondari ya wasichana Dakawa, chuo cha VETA, Chuo cha ualimu pamoja na Kituo cha afya.
Naye Mkuu wa Ndaki ya Sayansi na Elimu Kampasi ya Solomon Mahlangu Prof. Allen Malisa alisema Kampasi hiyo ilianzishwa mwaka 1978, wakati huo eneo hilo likijulikana kama makazi ya wapigania uhuru wa ANC wa Afrika ya Kusini.
Wapigania uhuru hao ambao wengi wao wakiwa ni vijana, walilazimika kukimbia Afrika ya Kusini ili kukwepa kukamatwa na Utawala wa Makaburu, kufuatia mgomo wa vijana wa Soweto wa mwaka 1976 hatua iliyopelekea vijana wengi kukimbilia Tanzania, ambapo awali walijikuta wamekuwa wengi kwenye mji wa Dar es Salaam kiasi cha kuhatarisha usalama baina yao na vijana wazawa.
Katika kutatua tatizo hilo, mamlaka ya utawala wa wakati huo iliwahamishia wapigania uhuru hao Mkoani Morogoro, na kwa vile kulikuwepo na haja ya kuwalinda na Makaburu ambao walikuwa wanafanya kila mbinu kuwatafuta popote walipo, waliwekwa jirani na kikosi cha jeshi la wananchi cha Mzinga kwa muda. Hatimaye, walihamishiwa eneo la Mazimbu ambalo liko uwanda wa chini na hivyo kutokuonekana kirahisi kutokea mjini Morogoro.
Kwa kuwa idadi ya vijana hao ilikuwa ni kubwa, na kutokana na ugeni katika makazi hayo mapya, hawakuwa na kazi za kufanya, hivyo kutumia muda mwingi kufundishana; wakubwa wakichukua nafasi ya ualimu na kuwafundisha wadogo.
Jambo hilo liliporipotiwa kwa uongozi wa ANC kule Afrika ya Kusini, liliwagusa Viongozi na kufanya aliyekuwa Rais wa chama, Ndugu Oliva Tambo, kuagiza makazi hayo waliyopewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ijengwe shule. kwa kutekeleza maagizo hayo ya ANC, eneo hilo lilijengwa shule iliyojulikana kama “ANC school” Mazimbu.
Kufuatia kijana aliyekuwa mpigania uhuru machachari, aliyejulikana kwa jina la Solomon Kalushi Mahlangu, kukamatwa na kutiwa kizuizini mwaka 1977 na hatimaye kunyongwa hadi kufa mwezi Aprili 1979, Uongozi wa ANC ulibadilisha jina la Mazimbu “ANC school” kuwa “Solomon Mahlangu Freedom College” (SOMAFCO) ili kutambua mchango wa wapigania uhuru wa ANC kwenye kutafuta uhuru.
Naibu Waziri Shonza yupo katika ziara ya kikazi kutembelea maeneo ya ya historia ya ukombozi wa Afrika katika mikoa ya Dodoma wilaya ya Kongwa, Morogoro wilaya Kilosa, Manispaa ya Morogoro pamoja na Mkoa wa Pwani wilaya za Chalinze na Bagamoyo.
No comments:
Post a Comment