Balozi Seif akiwa katika picha na baadhi ya viongozi wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kiazai Kipya walipomtembelea kwa mazungumzo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. |
Na Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wasanii kuitumia kikamilifu studio ya Muziki na Filamu iliopo Rahaleo, ili waweze kupata mafanikio ya kiuchumi pamoja na kuitangaza Zanzibar kimataifa.
Dk. Shein ametowa wito huo Ikulu Mjini hapa, katika hafla ya kupokea tuzo, Cheti na CD kutoka kwa wasanii wa filamu nchini, zilizotokana na ushindi walioupata katika mashindano yalioandaliwa na Kituo cha Azam TV.
Katika mashindano hayo yaliofanyika mwezi April, 2018 , filamu 200 kutoka nchi sita zilishindaniwa na wasanii wa Zanzibar waliibuka washindi kupitia filamu za ‘Bint Zanzibar’, ‘Sisi na wao’ pamoja na ‘Dema’.
Dk. Shein alisema Studio ya Muziki na filamu iliipo Rahaleo, ni miongoni mwa studio bora na yenye vifaa vya kisasa, hivyo amewataka wasanii kuitumia kikamilifu, ili waweze kunufaika kutokana na Hati miliki ya kazi zao pale watakapoziuza.
Alisema safari ya wasanii hao bado ni ndefu, hivyo akawataka kuongeza bidii ili kupata mafanikio, sambamba na kuitangaza Zanzibar kimataifa, akibainisha baadhi ya Mataifa ikiwemo Marekani, India na Nigeria ambapo wasanii wake wamepata mafanikio makubwa kutokana na sanaa ya uigizaji.
Aidha, aliwataka kuongeza kasi katika kuendeleza sanaa, kwa kigezo kuwa jamii inahitaji kuliwazwa baada ya shughuli mbambali za kazi. Dk. Shein, aliwapongeza wasanii hao kwa kazi kubwa waliyofanya na kuiletea sifa Zanzibar.
“Mmefanya kazi kubwa , ni kazi ya thamani…mimi nimeonyesha njia…”, alisema.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza wasanii waliojitokeza kuomba matengenezo ya Studio hiyo, wakati wa Kampeni kuelekea Uchaguzi mkuu wa 2010. Alisema serikali imetumia fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo ya studio hiyo na kuahidi kuendelea kuwaunga mkono wasanii pale mahitaji zaidi yatakapojitokeza katika studio hiyo.
Akigusia historia ya filamu Zanzibar, Dk. Shein alisema Zanzibar inajivunia kwa kuwa na magwiji wa sanaa mbali mbali, ikiwemo wa filamu pamoja na kupata bahati ya wasanii mahiri duniani kuja nchini kwa ajili ya kurekodi michezo yao.
Alisema baada ya Mapinduzi ya 1964, filamu ya mwanzo iliyojuilikana Zanzibar yasonga mbele” ilirikodiwa na baadae kusambazwa katika Mikoa yote mjini na mashamba.
Nae, Waziri wa Vijana,Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Karume, alimshukuru Rais Dk. Shein kwa juhudi zake za kuendeleza sanaa nchini na kuunga mkono mahitaji ya wasanii, ambapo alifanikisha ujenzi wa Studio ya kisasa ya Muziki na Filamu.
Aidha, aliwapongeza wasanii kwa kazi nzuri ya uigizaji akibainisha heshima kubwa wanayopata wasanii mbali mbali duniani kutokana na kazi za sanaa, hivyo akawataka kuiga mfano wao. Mapema, Katibu wa Chama cha wasanii waigizaji, Salum Maulid ‘stika’ alisema wasanii wanahitaji kupatiwa mafunzo zaidi ya uigizaji ili kuongeza uwezo wao kiutendaji.
Alisema katika utendaji wao wakazi wamekuwa wakipata mashirikiano mazuri na viongoi wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa an Michezo pamoja na COSOZA. Aliiomba Serikali kuendelea kuwaunga mkono wasanii na kusema hatua hiyo itafanikisha azma ya kuutangaza Utalii kupitia sanaa.
Aidha, alisema Chama cha wasanii Zanzibar, kimejidhatiti kuwaelekeza wasanii juu ya umuhimu wa kufanya kazi zao kwa msingi wakulinda mila, silka na utamaduni wa Wazanzibari.
No comments:
Post a Comment