Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia) akiongoza wananchi wa Manispaa ya Morogoro, mkoani Morogoro katika mazishi ya wananchi waliofariki dunia kutokana na ajali ya moto. |
Askari wakisaidia uchimbaji wa makaburi katika mazishi ya wananchi waliofariki dunia kutokana na ajali ya moto. |
Sehemu ya makaburi katika mazishi ya wananchi waliofariki dunia kutokana na ajali ya moto. |
*Huzuni, simanzi, majonzi na vilio vyatawala mjini Morogorogo
HUZUNI, simanzi, majonzi na vilio vimetawala mjini Morogoro leo wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwaakiongoza umati wa wananchi wa Manispaa ya Morogoro, mkoani Morogoro katika mazishi ya wananchi waliofariki dunia kutokana na ajali ya moto wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 71 huku wengine 59 wakijeruhiwa.
Mazishi hayo yameanza kufanyika Agosti 11, 2019 katika eneo la makaburi la Kola Hill mjini Morogoro ambapo Waziri Mkuu amemwakilisha Rais, Dkt. John Magufuli. Ametoa pole kwa wafiwa wote na amewaomba wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki cha maombolezo.
Akizungumza na wananchi katika ibada ya kuwaombea marehemu waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Msamvu mjini Morogoro iliyofanyika kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi na wadau mbalimbali kwa ushirikiano waliouonesha wakati huu wa amajonzi.
Kufuatia ajali hiyo iliyotokea jana saa 2 asubuhi baada ya lori lenye shehena ya mafuta ya petrol kupinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu mjini Morogoro wakati dereva alipokuwa akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki. Rais Dkt, Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo ya Kitaifa kuanzia jana Jumamosi Agosti 10,2019 na bendera zote zipeperushwe nusu mlingoti.
Mazishi hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isac Kamwelwe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Wengine ni Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge, viongozi wa dini na wananchi wa mkoa wa Morogoro.
No comments:
Post a Comment