WAZIRI MKUU AUNDA TUME KUCHUNGUZA AJALI YA MOROGORO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 12 August 2019

WAZIRI MKUU AUNDA TUME KUCHUNGUZA AJALI YA MOROGORO


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akitazama mahali ambapo lori la mafuta lilipinduka na kushika moto hatimaye kusababisha vifo vya watu 69 kwenye eneo la Msamvu mjini Morogoro wakati alipotembelea eneo hilo, Agosti 11, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waombolezaji  wakati aliposhiriki  katika maandalizi ya kutambua miili na maziko ya watu 69 waliofariki dunia katika ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kushika moto  katika  eneo la Msamvu mjini Morogoro. Alizungumza na waombolezaji hao kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waombolezaji  wakati aliposhiriki  katika maandalizi ya kutambua miili na maziko ya watu 69 waliofariki dunia katika ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kushika moto  katika  eneo la Msamvu mjini Morogoro. Alizungumza na waombolezaji hao kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya Mawaziri na viongozi wa mkoa wa Morogoro walioshiriki katika maandalizi ya kutambua miili na maziko ya watu 69 waliofariki dunia katika ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kushika moto kwenye eneo la Msamvu mjini Morogoro. Alikuwa  kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019. Kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Morogoro, Innocenti Kalogelisi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Stephene Kebwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe na kulia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Baadhi ya waombolezaji wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza baada ya kushiriki katika maadalizi ya kutambua miili na mazishi ya watu 69 waliofariki dunia katika ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kushika moto kwenye eneo la Msamvu mjini Morogoro. Alizungumza na waombolezaji hao kwenye viwanja vya Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameunda tume maalumu kwa ajili ya kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali ya moto iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 69 hadi mchana huu na wengine 70 kujeruhiwa wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka, mjini Morogoro.

“Hii tume inaanza kazi Agosti 11, 2019, Hadi ijumaa inipe taarifa yake na hata kama mimi sijawajibika initaje. Ajali ya namna hii si mara ya kwanza ilitokea Mbeya eneo la Mbalizi. Naomba niwasihi Watanzani pale gari linapoanguka tusitume kama fursa twende tukaokoe binadamu waliopo pale”.

Waziri Mkuu ameunda tume hiyo Agosti 11, 2019, wakati akizungumza na waombolezaji waliofika katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao. Niko mbele yenu nikimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli aliyenituma kuja kuungana nanyi kwenye siku hii ya huzuni”.

Waziri Mkuu amesema lazima wajiridhishe kama Serikali ilitekeleza vizuri jukumu lake kwa sababu ajali imetokea saa mbili asubuhi katikati ya mji, hivyo tunataka kujua ajalj ilipotokea kila mmoja alitumiza jukumu lake.

Amesema ajali imetokea karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi na kuna polisi sasa je hawa wananchi waliopata ajali walienda na madumu ya kuchotea mafuta inamaana waliamka asubuhi wakijua ajali itatokea. “Najua pale ajali inapotokea trafiki wana wahi haraka hata kama kwa gari la kukodi. Watu walikuja na madumu, wengine kuchomoa betri nani aliwazuia.Je lilipoanza kuungua gari la zima moto lilikuja kwa wakati gani”.

Waziri Mkuu amesema lazima wajiridhishe ndani ya Serikali kama wamewajibika. “Kuna vitu vingi lazima tuviangalie tujue nani hakutimiza majukumu yake. Nadhani ujumbe mnaupata si vyema tutakimbilia vitu badala ya watu. Tunasikitika sana kwa yaliyotukuta hata upande wa Serikali tunasikitika kuwapoteza Watanzania”.

Pia, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu jitihada za kuokoa waliopata majeraha kwamba zinaendelea vizuri na jukumu lao kubwa kuwaombea marehemu wapumzike kwa amani na pia wawaombee wajeruhi waweze kupona. Waziri Mkuu ameongeza kuwa, Rais Dkt. Magufuli tayari ameshatoa kibali cha kutolewa fedha kwa ajili ya kununuliwa vifaa tiba na dawa zinazohitajika.

Akizungumzia kuhusu idadi ya vifo na majeruhi waliotokana na ajali hiyo ambayo inatangazwa kupitia vyombo mvalimvali vya habari, Waziri Mkuu amesema ni vema takwimu hizo wakaacha zikatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Stephen Kebwe.

“Kwenye vyombo vya habari tuelewane kwenye takwimu za vifo na majeruhi. Msiseme suala la takwimu anayetoa ni Mkuu wa Mkoa na matukio haya yapo chini yake. Nimeamua kusema hivi hizi takwimu zikitajwa nyinginyingi mnajenga hofu na taharuki kwa wananchi. Hili halikubaliki mkitaka taarifa mtafuteni mkuu wa mkoa”.

 Wakati Huo huo, amesema Rais Dkt. Magufuli alipokea taarifa mapema ya ajali ya lori la mafuta na kusababisha vifo vya Watanzania 69, ambapo alimtaka aende mkoani Morogoro kwa ajili ya kuwasilisha salamu za pole kwa wananchi wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kufuati tukio hilo la kuhuzunisha. Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anawaombea marehemu na majeruhi lakini pia amawataka wafiwa na wananchi wote wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao.

“Mheshimiwa Rais amehuzunishwa sana na msiba huu ndio maana amenituma nilete ujumbe huu kwenu.Lakini pia nimekuja na salamu za pole kutoka kwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan. Jambo hili si dogo ni kubwa kwani tumepoteza ndugu zetu wengi. Kwa idadi hii kubwa ya ndugu zetu waliotangulia mbele za haki na wale waliopo kwenye maumivu si jambo la faraja”.

Waziri Mkuu amesema wananchi wasipeleke miili kwanza makaburini ili waweze kupitia na kutambua ndugu na rafiki kwa ajili ya  kuwa na kumbukumbu ya kudumu. “Hali si nzuri ndugu zetu wameungua sana wapo wengine mnaweza msiwatambue lakini mnaweza kutambua kwa alama. Wapo wengine walivaa bangili, heleni, mkanda havijaungua”.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kama hawajawatambua Serikali imeweka utaratibu wa vipomo vya vinasaba, ambapo  kumbukumbu hizo zimechukuliwa na wataalamu wetu wa afya. “Kama ukipita ukishindwa kumuona bado tunakuruhusu kukupima vinasaba na kulinganisha na vyakwako. Bado haki ya kumpata ndugu yako iko pale pale madaktari wapo, mitambo ipo tutachukua vinasaba na kuainisha tutatoa nafasi leo hadi saa 10 kufanya utambuzi”.

Amesema Serikali inaratibu vizuri jambo hilo lakini kuanzia saa 10 itaruhusu wale waliotambuliwa kuchukua mwili lakini kama hawajajipanga vizuri itauzika na kama kuna jina litaliandika na kama hakuna jina wataandika namba ya vinasaba ili kutoa fursa kwa ndugu siku nyingine waende wakapimwe na kuoneshwa kaburi la ndugu yao.

No comments:

Post a Comment