TIMU ya Afya ya Mkoa wa Rukwa inayojishughulisha na ukusanyaji wa damu kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Mkoa huo Mh. Joachim Wangabo ijumaa hii iliweka makazi yake nje ya Ofisi ya mkuu wa mkoa ili kukusanya damu kutoka kwa watumishi wa ofisi hiyo pamoja na wananchi mbalimbali wanaofika hapo kupata huduma mbalimbali.
Timu hiyo inayoongozwa na mganga mkuu wa mkoa ilianza kutekeleza maelekezo hayo tangu tarehe 14.8.2019 kwa kupita katika maeneo mbalimbali ya mji wa Sumbawanga kukusanya damu hiyo kwa kushirikiana na timu nyingine za Afya katika ngazi ya halmashauri ambazo nazo zinaendelea na zoezi hilo katika halmashauri nne za mkoa huo.
Taarifa hiyo imethibitishwa na mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu wakati alipokuwa akiongea na vyombo vya habari huku akiendelea kuwahamasisha watumishi wa serikali, waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini, viongozi wa kisiasa pamoja na wananchi wenye mapenzi mema kujitolea kutoa damu ili kuweza kuwasaidia majeruhi walioungua kutokana na kulipuka kwa lori la Mafuta katika eneo la Msamvu mkoani Morogoro Wiki moja iliyopita.
“Sisi kama wataalamu tumejipanga baada ya mheshimiwa mkuu wa mkoa kutoa haya maelekezo, kazi hii inafanyika katika halmashauri zote nne za mkoa wa Rukwa na katika halmashauri zetu kuna timu maalum ya ukusanyaji wa damu, kwahiyo toka agizo limetolewa timu zetu katika halmashauri zinaendelea na hiyo kazi,” Alisema.
Akimuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Rukwa katika zoezi hilo la kuwahamasisha watumishi wa serikali kujitolea damu, mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule ameendelea pia kuwahamasisha wananchi kuanzia ngazi za mitaa na vijiji waendelee kujitolea damu kupitia timu hiyo ya mkoa pamoja na timu za halmashauri zilizoteuliwa maalum kwaajili ya zoezi hilo lakini pia kufika katika hospitali ya mkoa kushiriki kujitolea damu.
“Damu inahitajika tunawaomba wananchi waendelee kujitolea kama ambavyo ratiba ilivyotangazwa, hii timu itakuwa inapita kwenye mitaa yetu kwenye kata zetu lakini pia kwa wale ambao watakuwa wamekosa hiyo nafasi, bado hospitali yetu ya mkoa itaweza kuwapokea waweze kuchangia damu kwaajili ya kuwanuru wenzetu ambao wamepata ajali kule Morogoro,” Alieleza.
Aidha, mmoja wa watumishi waliojitolea kuchangia damu Elvira Malema alieleza kuwa mahitaji ya damu ni makubwa na kujitolea damu hiyo huenda kukaokoa majeruhi wengine waliobakia na kudhani kuwa kama damu ingelikuwa ya kutosha huenda vifo hivyo visingevuka idadi iliyopo na hivyo kuwaomba wananchi ambao hawajafanya maamuzi ya kujitolea damu washiriki kufanya hivyo.
“Zoezi hili sikwamba linachukua muda mwingi, ni dakika tu unatolewa damu kama una uzito unaostahili, una damu ya kutosha, nawahamasisha watu wajitokeze kuchangia kwasababu leo unaweza ukaona ni kitu kinachotokea kwa mtu mwingine kwasababu hakijakufika kwenye familia yako ukadharau, kwahiyo nawahamasisha watu wajitokeze kuchangia,” Alisema.
Kwa upande wake mmoja wa madereva wa boda boda aliyefika katika ofisi hiyo kupata huduma Ayoub Wangoma ameishukuru serikali kwa kuwahamasisha madereva wa bodaboda kuchangia damu kwa kutanabahisha kuwa madereva hao wanahitaji damu kutokana na shughuli zao zinazowaweka barabarani kila kukicha na hivyo kuguswa na kampeni hiyo na hatimae kuamua kuunga mkono juhudi za mkoa kwa kujitolea damu.
“Sisi ka vijana tunaojishughulisha na bodaboda imetugusa sana na kujitoa kwa moyo kwasababu jambo kama lile waliopoteza maisha pale kuna ndugu zetu kuna wazazi wetu, kwahiyo tunapojitolea damu leo kwao kesho kwetu, inawezekana jambo kama lile tunaliongelea kwa udogo lakini mbeleni huko linaweza kutokea likatuhusu sisi wenyewe bodaboda kulingana na shughuli tunazofanya,” Alisema.
Zoezi la uchangiaji wa damu kwaajili ya kusaidia majeruhi wa ajali ya Morogoro inatarajiwa kuamalizika tarehe 18.8.2019 na taarifa ya jumla ya zoezi hilo kutolewa tarehe 19.8.2019 na hatimae damu hiyo kusafirishwa kwenda sehemu husika kulingaana na malekezo ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
No comments:
Post a Comment