WAFUGAJI WAANGUA KILIO MBELE YA WAZIRI MPINA BAADA YA KUCHOMEWA NYUMBA NA MAZIZI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 8 August 2019

WAFUGAJI WAANGUA KILIO MBELE YA WAZIRI MPINA BAADA YA KUCHOMEWA NYUMBA NA MAZIZI

 Mfugaji wa Kijiji cha Vilima Vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara, Dorcas Buyase akilia kwa uchungu mbele ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (hayuko pichani) aliyefika kijijini hapo kusaka suluhu ya mgogoro huo baada ya wafugaji hao kuchomewa moto nyumba zao na kukosa mahali pa kuishi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Vilima Vitatu walioondolewa na kuchomewa nyumba, mazizi na makambi ya uvuvi na kukosa mahali pa kuishi. Kulia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Vilima Vitatu, Mhe. Belela Erasto na Mbunge wa Babati Vijijini, Mhe. Jituson

 Mfugaji wa Kijiji cha Vilima Vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara, Nanu Mandaga akizungumza kwa majonzi mbele ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (hayuko pichani) aliyefika kijijini hapo kusaka suluhu ya mgogoro huo baada ya wafugaji hao kuchomewa moto nyumba zao na kukosa mahali pa kuishi

 Wafugaji wa Kijiji cha Vilima Vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara wakimsilikiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (hayuko pichani) aliyefika kijijini hapo kusaka suluhu ya mgogoro huo baada ya wafugaji hao kuchomewa moto nyumba zao na kukosa mahali pa kuishi

Wafugaji wa Kijiji cha Vilima Vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara wakiwa juu ya miti wakimsilikiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (hayuko pichani) aliyefika kijijini hapo kusaka suluhu ya mgogoro huo baada ya wafugaji hao kuchomewa moto nyumba zao na kukosa mahali pa kuishi. 

Na Mwandishi Wetu, Babati
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesitisha operesheni ya kuwaondoa na kuwachomea nyumba, mazizi ya mifugo, makambi ya uvuvi Wananchi wa Kijiji cha Vilima vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara na kuunda timu ya wataalamu kutoka Wizara 8 kufuatilia utekelezaji wa operesheni hiyo na kuwasilisha ripoti hiyo serikalini kwa maamuzi zaidi.
Operesheni hiyo iliyofanyika mwezi Julai mwaka huu  imesababisha wananchi  wengi kukosa mahali pa kuishi  kutokana na nyumba zao kuchomwa moto ambapo sasa wanaishi chini ya miti hali iliyosababisha adha kubwa kwa wanawake wajawazito, watoto na wagonjwa.
Pia mifugo yao kuvamiwa na wanyama wakali na mingine kupotea baada ya mazizi kuchomwa moto, shughuli za uvuvi kusimama baada ya makambi na zana za uvuvi kuteketezwa kwa moto hali ambayo imeleta taharuki kubwa kwa wananchi na kushindwa kujua la kufanya.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika  Kijiji cha Vilimavitatu na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu huku idadi kubwa ya wananchi wakiangua vilio mbele ya Waziri Mpina wakionesha masikitiko yao kuhusiana na unyama waliofanyiwa na Serikali ya wilaya hiyo na kumuomba kuwasaidia ili waweze kurudi katika maisha yao ya awali.
Walisema mbali na madhara hayo pia akiba ya chakula walichokuwa nacho majumbani mwao nacho kimechomwa moto hivyo kukosa kabisa chakula na kumuomba afikishe kilio hicho kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli ili wapatiwe msaada wa haraka chakula ili kunusuru wasife kwa njaa katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.
Waziri Mpina alihoji iweje operesheni hiyo ifanyike huku kukiwa na katazo la Rais Dk. John Pombe Magufuli la Januari 15 mwaka huu la kusitisha operesheni zote za kuwaondoa wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayodaiwa kuwa ni hifadhi hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.
Waziri Mpina pia ahoji iweje operesheni hiyo ifanyike kwenye eneo hilo huku kukiwa na Hukumu ya Mahakama iliyoliondoa eneo la Kijiji  cha Vilima Vitatu kwenye Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyapori Burunge (Juhibu) ambapo hukumu hiyo haikukatiwa rufaa wala kutenguliwa na Mahakama.
Pia Waziri Mpina alihoji iweje operesheni hiyo ya kuondoa mifugo  ifanyike bila kushirikisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi kama Sheria, Kanuni na miongozo inavyoelekeza hali iliyosababisha mifugo mingi kuteseka kwa kukosa huduma muhimu zikiwemo chanjo, dawa, maji na malisho na kusababisha mifugo kupotea na mingine kufa na kusababisha hasara kubwa kwa wafugaji taifa.
Kwa msingi huo, Waziri Mpina alisema operesheni imefanyika kinyume cha Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya mwaka 2003, Sheria ya Ustawi wa Wanyama Namba 19 ya mwaka 2008, Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za chakula cha Mifugo namba 13 ya mwaka 2010 na Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003.
Hivyo alisema wote waliohusika kufanya operesheni hiyo walipaswa kukamatwa na kushtakiwa kutokana na makosa ya kuvunja sheria hizo za mifugo kwani wanalo jukumu la kuzisimamia ili zisivunjwe kwakuwa  mifugo ni rasilimali muhimu kwa Taifa kama zilivyo rasilimali nyingine nchini.
Waziri Mpina alieleza kasoro nyingine za operesheni hiyo kuwa pamoja na  kutokufanya tathmini ya kina ya idadi ya wananchi, kaya, mifugo na mali zingine kabla ya operesheni kufanyika, kukosekana kwa nyaraka muhimu za kuendesha operesheni na mahusiano dhaifu baina ya wafugaji, JUHIBU na Mwekezaji Kampuni ya Chemchem Lorge ya nchini Ufaransa.
Pia Waziri Mpina alisema kasoro nyingine ni kutokamilika kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwani kama ungekamilika ungekuwa ndio muarobaini wa migogoro katika Kijiji cha Vilima Vitatu na vijiji vingine 9 vinavyounda Hifadhi ya Wanyamapori Burunge.
Pia Waziri Mpina aliwaonya viongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania kutojihusisha na vitendo kuhamasisha uvunjifu wa sheria za nchi na kama kuna masuala muhimu yanayowahusu wafugaji wafuate njia  sahihi za kukutana na mamlaka husika  kutafuta suluhu, Pia amewataka wafugaji kote nchini kufuata Sheria.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Babati Vijijini, Filbert  Mdachi alisema CCM imesikia malalamiko ya wananchi wa kuwahakikishia kuwa haki itatendeka na kumshukuru Waziri Mpina kwa kufika eneo hilo ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo ulisababisha adha kubwa kwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Kitundu alisema alisema operesheni hiyo ilifanyika baada ya kudaiwa kuwepo viashiria vya uvunjifu wa amani katika maeneo hayo na kukiri kupokea maelekezo kutoka mkoani .

No comments:

Post a Comment