WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Rwanda waje wawekeze katika sekta mbalimbali na kwamba Serikali itawapa ushirikiano wa kutosha.
Ameyasema hayo Juni 11, 2019 alipokutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Rwanda, Donatille Mukabalisa, Ofisini kwake Bungeni jijini Dodoma. Amesema Serikali ipo tayari kuwapokea wawekezaji kutoka katika nchi hiyo ili waje kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, kilimo, madini na utalii.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Tanzania na Rwanda ni nchi zenye uhusiano mzuri, hivyo amemwakikishia Spika Donatille kwamba Serikali itauimarisha uhusiano huo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambao utarajiwa kusaidia katika usafirishaji wa mizigo kwenda hadi nchini Rwanda.
Naye, Spika Donatille ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa inaoutoa kwa Serikali ya Rwanda, hivyo amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watauendeleza.
Spika huyo amesema ushirikiano wa Tanzania na Rwanda ni muhimu katika uchumi kwa kuwa wanatumia bandari ya Dar es Salaam katika kusafirisha asilimia kubwa ya mizigo yao.
Amesema wananchi nao wanatakiwa wawe na ushirikiano katika nyanja mbalimbali kama za kibiashara. Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha Watanzania wakawekeze nchini Rwanda.
No comments:
Post a Comment