Sehemu ya watalii 330 kutoka nchini china wakiwa katika hafla ya chakula cha usiku kilichoandaliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewapokea watalii 330 wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji kutoka jimbo la Zhejiang, China ambao waliwasili jana usiku kwenye uwanja wa ndege wa KIA.
Watalii hao ni kundi la kwanza miongoni mwa watalii 10,000 ambao wanatarajiwa kutembelea Tanzania mwaka huu,chini ya mpango unaosimamiwa baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania na kampuni ya TouchRoad International Holding Group ya China.
Akizungumza na watalii hao kwenye chakula cha jioni kilichoandaliwa kwenye hoteli ya Mount Meru Mei 12, 2019, Waziri Mkuu alimshukuru Mwenyekiti wa Touchroad Group, Bw. Liehui He kwa kuwaunganisha Watanzania na Wachina kupitia mpango wake wa kukuza utalii.
“Mbali na kutuunganisha Watanzania na Wachina, tunakushukuru pia kwa kuamua kuitangaza Tanzania kuwa nchi yenye fursa nyingi za kitalii duniani,” alisema.
Waziri Mkuu alitaja vivutio vingine vilivyopo ambavyo watalii hao wanaweza kuvifurahia kuwa ni mbuga za Ngorongoro, Serengeti, Manyara, Mlima Kilimanjaro, Mahale, Katavi na akawataka waende visiwa vya Zanzibar kuona fukwe zenye mchanga mweupe na kupata marashi ya karafuu.
Waziri Mkuu aliwapongeza watendaji wa Bodi ya Utalii na makampuni ya utalii kwa maandalizi na mapokezi mazuri kwa watalii hao. Pia alimpongeza Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kushirikiana na TouchRoad na kuifanya Tanzania ipokee watalii wengi.
Akielezea ujio wa kundi la kwanza la watalii, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii nchini, Bi. Devotha Mdachi alisema watalii hao wametokea Djibouti ambako walikaa kwa siku moja, hapa Tanzania watakaa kwa siku nne na kisha wataelekea Bulawayo, Zimbabwe ambako watakaa kwa siku mbili na kurejea China.
Mapema, akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Prof. Palamagamba Kabudi alisema ujio wa watalii hao ni sehemu ya mpango mkubwa wa nchi wa kuongeza watalii kutoka China unaofahamika kama Tour Africa - The New Horizon.
Aliwataka Watanzania wachangamkie fursa ya ujio wa wageni ili waweze kunufaika kiuchumi. “Naomba niwasihi Watanzania, hii ni fursa hatuna budi kuichangamkia ili wao wafurahie utalii nchini lakini nasi tunufaike na uwepo wao.”
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangallah alisema Serikali imeamua kuwekeza zaidi kwenye utalii kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili iweze kuongeza idadi ya watalii na hatimaye kukuza uchumi.
Alisema wameamua kubadilisha maeneo ya vipaumbele vya utalii na kujitangaza kwenye nchi nyingine ili tuweze kufikia lengo letu la kuongeza idadi ya watalii.
“Tuliamua kuwekeza katika nchi tano za kipaumbele cha kwanza ambazo ni Marekani, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na Italia. Sasa hivi uelekeo wetu ni China, Israel, Oman na nchi zote za Ghuba, Australia na Urusi,” alisema.
Jimbo la Zhejiang liko Kusini Mashariki mwa China na majimbo yenye nguvu ndogo kisiasa lakini ni mojawapo ya majimbo yenye wakazi wengi na matajiri. Pia jimbo hilo ni maarufu kwa shughuli za kilimo na linaongoza kwa uzalishaji wa chai na mazao yatokanayo na uvuvi.
Viongozi wengine waliokuwepo ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Kangi Lugola, Waziri wa Nchi (OWM-Uwekezaji), Bibi Angela Kairuki, Naibu Waziri (OWM-KAV), Bw. Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dkt. Damas Ndumbaro, Balozi wa Djibouti nchini China na Balozi wa Tanzania nchini China.
No comments:
Post a Comment