WANAWAKE WASHAURIWA KUENDELEZA UJUZI WAO HUKU WAKIZINGATIA MAJUKUMU YA FAMILIA ZAO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 13 May 2019

WANAWAKE WASHAURIWA KUENDELEZA UJUZI WAO HUKU WAKIZINGATIA MAJUKUMU YA FAMILIA ZAO


Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB, Bi. Abella Tarimo (kushoto) akichangia mada katika mjadala ulioandaliwa na benki hiyo katika maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani. Kutoka kulia mbele ni Meneja Mikopo Chechefu wa NMB, Pauline Mohele na Meneja Uhusiano Mwandamizi, Amana na Biashara wa NMB, Beatrice Mwambije.
Meneja Uhusiano Mwandamizi, Amana na Biashara wa NMB, Beatrice Mwambije (katikati) akichangia mada katika mjadala ulioandaliwa na benki hiyo kuadhimisha Siku ya Mama Duniani. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB, Bi. Abella Tarimo pamoja na Meneja Mikopo Chechefu wa NMB,Pauline Mohele kulia.
Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya NMB, mkoani Mwanza wakitoa msaada kwenye Kituo cha Afya cha Buzuruga wodi ya Mama na Watoto-Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani.
WANAWAKE nchini wameshauriwa kutokata tamaa kufanyia kazi taaluma walizonazo huku wakizihudumia familia zao kwa mujibu wa majukumu yao nyumbani.

Ushauri huo umetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB, Abella Tarimo katika mjadaLa ulioandaliwa na benki hiyo kuadhimisha Siku ya Mama Duniani (Mother's Day).

Alisema ili wanawake waweze kufanikiwa katika jambo lolote juhudi na uwazi juu ya suala wanalolifanya zinahitajika.

"Ili mradi mtu uwe na nia na unaungwa mkono huku ukiweka jitihada za dhati bila kusahau familia yako, utafanikiwa. Wapo baadhi ya wanawake ambao wamekuwa wakijikwamisha kwa kudhani kuwa hawawezi kufanyia kazi ujuzi waliousomea na kufanikiwa huku wakizihudumia familia zao ipasavyo, jambo ambalo si sawa," alisema Bi. Tarimo.

Alisema kwa kuanzia mafanikio wanawake wafanyakazi hawana budi kujenga utamaduni wa kushirikiana pamoja na kuungana mkono bila kuathiri majukumu yao kifamilia.

Kwa upande wake Meneja Uhusiano Mwandamizi, Amana na Biashara wa NMB, Beatrice Mwambije akichangia mada katika mjadala huo, aliwataka akina mama ambao wako kazini na wamekata tamaa na hata kufikiria kuacha kazi ili wakalee familia zao kutathmini mara mbilimbili kabla ya kufanya maamuzi yao.

"Ni kweli ukiangalia majukumu ya mama mwenye mtoto mchanga anaweza kubanwa akashindwa kutekeleza kazi zake ofisini...lakini hiki kisiwe kikwazo kuna namna unaweza kujipanga na kukabiliana na yote hayo na ukaendelea na kazi pasipo kuathiri pande zote," alisema Bi. Mwambije.

Aidha aliwataka akinamama kuangalia usalama wa familia na watoto kwa maisha ya baadaye wanapokuwa wakubwa hivyo kuna kila sababu ya kuwajengea msingi imara.

 Mjadala huo ulioandaliwa na Benki ya NMB ulienda sambamba na maadhimisho ya 'Siku ya Mama Duniani’ huku ukisisitiza kutambuliwa kwa majukumu ya kinamama duniani kote kwani wanamchango mkubwa kimaendeleo.

Benki ya NMB imeadhimisha siku hii kwa kualika wadau mbalimbali kujadili mada ya mama katika matawi yake yote nchi nzima pamoja na baadhi yao kutoa misaada kwa watoto na akina mama.


#Nani kama Mama


Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya NMB matawi mbalimbali, wakiwa katika picha za kumbukumbu mara baada ya maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani.

Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya NMB matawi mbalimbali, wakiwa katika picha za kumbukumbu mara baada ya maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani.

Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya NMB matawi mbalimbali, wakiwa katika picha za kumbukumbu mara baada ya maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani.

No comments:

Post a Comment