Kaimu Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Gladness Munuo (wa kwanza kushoto) ambaye pia ni Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi (CRC) akizungumza katika mkutano huo. |
Mwenyekiti wa Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA) , Bw. John Seka akizungumza katika mkutano huo. |
Mkutano kati ya Mtandao wa Asasi za Kiraia Unaotetea Maboresho ya Sheria ya usalama barabarani pamoja na waandishi wa habari ukiendelea. |
Na Joachim Mushi, Dar
MTANDAO wa Asasi za Kiraia Unaotetea Maboresho ya Sheria ya usalama barabarani umesema mwamko wa viongozi wa ngazi mbalimbali katika jamii, ndiyo silaha itakayotumika katika kufanya maamuzi ya kisheria, sera na kimkakati ili kuhakikisha Tanzania inapunguza vifo/ajali kabisa zitokanazo na ajali za barabarani.
Kauli hiyo imetolewa na asasi hizo katika mkutano mfupi na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuzungumzia Maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Mataifa ya Usalama Barabarani inayoanza rasmi tarehe 6 hadi 12 ya Mwezi Mei, 2019.
Akitoa tamko la pamoja la asasi hizo zipatazo 13, Mkuu wa Program kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA ), Bi. Marry Richard, alisema wanaamini endapo viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, taasisi na mamlaka nyingine zikijitoa na kusimama kidete kusimamia masuala ya afya, elimu, miundombinu, rushwa, ubadhirifu, demokrasia na changamoto nyingine katika jamii mabadiliko yataonekana.
Aidha alisema bado kuna hali ya mwamko mdogo katika masuala ya usalama barabarani hivyo kuomba suala hilo lipewe kipaumbele kutokana na madhara yake kugusa nyanja zote yaani kiuchumi, jamii na afya kiujumla.
"...Tunachukua fursa hii kusisitiza kwamba suala la usalama barabarani ni suala la kiuchumi, kijamii na kiafya hivyo ni vyema likatiliwa mkazo ili kuzuia ajali na rasilimali inayotumika kuwatibu majeruhi na familia za waathirika zielekezwe maeneo mengine kwa maendeleo ya nchi."
"Asasi za kiraiaa zinazohusisha na masuala ya usalama barabarani Tanzania kwa umoja wetu tumeona kuwa nafasi ya viongozi ni muhimu katika kuleta mabadiliko chanya hasa kwenye upande wa sera na sheria ya usalama barabarani," alisisitizaa Bi. Richard katika taarifa aliyoitoa.
Alisema kauli mbiu ya wiki ya maadhimisho; ni Uongozi kwa Usalama Barabarani, ambayo inaakisi nafasi ya viongozi katika kuleta mabadiliko kwenye eneo la usalama barabarani.
Kwa upande wake Mgeni rasmi katika mkutano huo ambaye ni Mbunge wa Viti maalum, Mh. Fatma Toufiq wao kama wabunge wawakilishi wa wananchi watahakikisha wanashawishi mabadiliko ya kanuni na sheria zilizo na mapungufu katika sheria ya usalama barabarani ili kupunguza madhara.
Mtandao wa Asasi za Kiraia Unaotetea Maboresho ya Sheria ya usalama barabarani unaundwa na asasi za; TAMWA, TAWLA, TLS, TMF, SIKIKA, SHIVYAWATA, SAFESPEED FOUNDATION, RSA, WLAC, WILDAF, AMEND, TCRF na TABOA.
No comments:
Post a Comment