KATIKA kutekeleza
majukumu yake ya kuhakikisha kuwa Sekta ya Fedha inachangia ipasavyo utulivu na
ukuaji wa uchumi nchini, Benki Kuu ya Tanzania ilibaini uwepo wa maduka ya kubadilisha
fedha za kigeni ambayo yalikuwa yakiendeshwa pasipo kuzingatia Sheria ya Foreign Exchange Act 1992, Kanuni za The Foreign Exchange (Bureau de Change)
Regulations 2015 na marekebisho ya mwaka 2017 na Taratibu za utoaji wa
huduma za ubadilishaji wa fedha za kigeni.
Kufuatia hali hiyo, zoezi maalum la
ukaguzi wa kina kwa maduka hayo lilifanyika Arusha Novemba 2018 na kwa Dar es
Salaam siku ya tarehe 27 Februari 2019, 1 na 8 Machi 2019 kwa kuhusisha vyombo
vya Dola na kubaini ukwepaji mkubwa wa kodi na uvunjaji wa Sheria.
Zoezi hili limebaini pia uondoshwaji wa
fedha katika mfumo rasmi wa fedha na kuelekezwa kwenye mifumo ya utakasishaji
wa fedha haramu, kupokea Amana kutoka kwa wafanyabiashara kinyume cha matakwa
ya leseni za biashara husika, kudhoofisha thamani ya shilingi, pamoja na mambo
mengine ambayo yalianza kuathiri usalama wa nchi kwa ujumla. Kwa mfano, baadhi
ya maduka yaligundulika kutumia fedha nyingi za Tanzania kununua fedha za
kigeni lakini fedha kidogo za kigeni ziliuzwa na hakuna taarifa ya matumizi ya
fedha za kigeni zilizobaki.
Ni vizuri ieleweke kuwa, zoezi la ukaguzi wa maduka ya kubadilisha
fedha za kigeni lilitekelezwa kwa kuzingatia Sheria za nchi tofauti na
malalamiko na tuhuma mbalimbali zilizotolewa za kudai uwepo wa ukiukwaji wa Sheria
na haki kwa wamiliki wa maduka hayo. Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna
mmiliki yeyote wa duka aliyewasilisha malalamiko kuhusiana na zoezi hili kwenye
mamlaka husika. Hata hivyo, Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka nyingine za
Serikali zinafuatilia kwa umakini ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo
zinazotolewa.
Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza
majukumu yake kwa umakini. Hivyo, Serikali inauthibitishia umma wa Watanzania
kuwa katika zoezi la ukaguzi wa Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni hakuna
fedha au mali yeyote iliyotaifishwa. Taratibu za kisheria zilifuatwa wakati wa
kuchukua vielelezo mbalimbali zikiwemo fedha, kompyuta, simu za viganjani,
mashine maalum za kuhifadhi taarifa na taarifa mbalimbali ili kusaidia
uchunguzi.
Aidha, lengo la zoezi hili sio kufuta biashara ya maduka ya
kubadilishia fedha za kigeni kwa watu binafsi, bali ni kudhibiti ukiukwaji wa
sheria uliokithiri, ukwepaji wa kodi na utakatishaji wa fedha haramu. Maduka
machache ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo yalizingatia Sheria na Kanuni za
Foreign Exchange na masharti ya
biashara hiyo yaliachwa kuendelea na utoaji wa huduma hiyo.
Hivi sasa Serikali imeandaa Kanuni mpya kwa
ajili ya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo zitaelekeza
jinsi ya kuomba leseni za uendeshaji wa maduka hayo kwa mtu binafsi au taasisi
yeyote na masharti ya kuzingatiwa wakati wa shughuli hizo.
Kanuni hizo zinalenga kuweka mazingira
mazuri ya biashara ambayo hayatatoa athari kwa sekta ya fedha na uchumi jumla,
na inakuwa yenye manufaa kwa nchi. Kwa kuzingatia maduka mengi yaliyokaguliwa
yamefungwa, Benki Kuu ya Tanzania imechukua tahadhari ya kuhakikisha huduma ya
ubadilishaji fedha za kigeni inaendelea nchini kwa kutolewa na benki zote
pamoja na Shirika la Posta.
Benki Kuu ya Tanzania itakuwa inatoa taarifa kuhusu
upatikanaji wa huduma hiyo na kuzihimiza benki za biashara na Shirika la Posta
kutoa taarifa kwa umma kuhusiana na huduma katika maduka yaliyofunguliwa na
benki hizo na Ofisi ya Posta.
Kwa kipindi kifupi cha utekelezaji wa zoezi
la udhibiti wa biashara ya kubadilisha fedha za kigeni, thamani ya shilingi
imeimarika na upatikanaji wa fedha za kigeni katika benki za biashara umekuwa
mzuri. Kabla ya zoezi la udhibiti wa biashara ya kubadilisha fedha ya kigeni
dola ya Marekani ilikuwa inauzwa kwa wastani wa shilingi 2,450 na baada ya
utekelezaji wa zoezi hivi sasa dola ya Marekani inauzwa kwa wastani wa shilingi
2,300.
Aidha, Benki za biashara kwa wastani hivi sasa zinakusanya jumla ya dola
za Marekani milioni 15 kwa siku. Ni matarajio ya Serikali kuwa udhibiti huu
utaziwezesha Benki za biashara na taasisi nyingine kuuza fedha za kigeni kwa
wingi kwenye soko la fedha za kigeni na hatimaye kuongeza akiba ya fedha za
kigeni.
Serikali inatoa tahadhari kwa wananchi
kutoshiriki kwenye biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa njia zisizo
halali. Hivi sasa kuna taarifa kwa baadhi ya maeneo ya mipakani na majiji ya
Dar es Salaam na Arusha wamejitokeza watu wanaofanya biashara haramu ya
kubadilisha fedha za kigeni ambao wamewaathiri baadhi ya wananchi kwa wizi.
Vyombo vya usalama ikiwemo jeshi la polisi vimeongeza nguvu katika kuhakikisha
biashara hii haramu (Black Market) inatokomezwa na hivi sasa wahalifu saba
wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.
Serikali inapenda kuwahakikishia Watanzania
wote kuwa inayo akiba ya fedha za kigeni ya kutosha zipatazo dola za Marekani
bilioni 4.67 hadi tarehe 30 Machi 2019 zenye uwezo wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka
nje ya nchi kwa kipindi kisicho pungua miezi 4.8. Hivyo, wasiwasi kuwa Serikali
imechukua hatua ya kufunga baadhi ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kwa
sababu haina akiba ya fedha za kigeni si ya kweli hata kidogo.
Aidha, hofu
kwamba nchi inarejea katika kipindi cha nyuma ambapo fedha za kigeni zilikuwa
zinatolewa kwa vibali (rationing) ili kukidhi mahitaji ya fedha hizo kwenye
utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, nazo hazina msingi.
Mapato ya Nchi yanayotokana na vyanzo vya
fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa na huduma nje ya nchi yalikuwa na thamani ya dola
za Marekani milioni 8,554.5 kwa mwaka unaishia Februari 2019 ikiwa ni ongezeko
la asilimia 1.4 ikilinganishwa na fedha za kigeni zilizopatika mwaka unaishia
Februari 2018.
Ongezeko hilo la mapato ya fedha za kigeni kwa Nchi yamechangiwa
zaidi na uuzaji wa bidhaa zisizo asilia nje ya nchi zikiwa na thamani ya dola
za Marekani milioni 3,878.5 sawa na asilimia 10.3 ikilinganishwa na mwaka
uliotangulia. Vile vile, huduma zilizotolewa nje ya nchi kama vile usafiri na usafirishaji
na utalii ziliingiza jumla ya dola za Marekani milioni 4,074.1 sawa na ongezeko
la asilimia 6.1 ikilinganishwa kiasi kilichopatikana mwaka ulitangulia.
Aidha, Serikali inachukua fursa hii kuwaeleza wananchi
kuwa nchi yetu ina akiba ya chakula cha kutosha ambacho kina utoshelevu wa
asilimia 124 kwa mwaka huu wa fedha 2018/19. Hivyo, Serikali haitarajii kutumia fedha za kigeni kuagiza chakula kutoka nje ya
nchi isipokuwa tu kama ikitokea hali ya ukame ikawa mbaya katika siku zijazo.
Serikali, kupitia Benki Kuu ya Tanzania,
inawataka wafanyabiashara ya huduma ya kubadilisha fedha za kigeni kuzingatia
na kutii Sheria ya Foreign Exchange 1992,
Kanuni ya Foreign Exchange (Bureau de
Change) Regulations 2015 na marekebisho ya mwaka 2017, Masharti ya biashara
ya huduma ya kubadilisha fedha za kigeni na Maelekezo ya Msimamizi (BOT) wa
Sekta ya Fedha Nchi. Mwisho Serikali inawapongeza wananchi wa Tanzania kwa kuwa
waelewa na watulivu wakati wote zoezi la ukaguzi likiendelea, licha ya
kujitokeza kwa taarifa za upotoshwaji wa zoezi hili.
DKT.
PHILIP ISDOR MPANGO
WAZIRI
YA FEDHA NA MIPANGO
No comments:
Post a Comment