RAIS MAGUFULI AZIPA WIKI MOJA WIZARA ZA ARDHI NA VIWANDA KUTAFUTA ARDHI KWA MWEKEZAJI SUGAR INVESTMENT TRUST - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 17 April 2019

RAIS MAGUFULI AZIPA WIKI MOJA WIZARA ZA ARDHI NA VIWANDA KUTAFUTA ARDHI KWA MWEKEZAJI SUGAR INVESTMENT TRUST

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na wanahabari akiwa na Mhe. John Chiligati aliyeongozana na Balozi wa Mauritius nchini Mhe.  Jean Pierre Jhumun, Mwenyekiti wa Kampuni ya Sugar Investment Trust (SIT) ya Mauritius Bw. Gansam Boodram baada ya kuonana na kufanya mazungumzo nabalozi huyo Ikulu Jijini Dar es salaam. Aprili 17, 2019.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akizungumza na Balozi wa Mauritius nchini
Mhe. Jean Pierre Jhumun pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Edwin Mhede, Maafisa wa Kituo cha uwekezaji na wa Ikulu baada ya 
kuonana na kufanya mazungumzo na balozi huyo Ikulu jijini Dar es salaam Aprili 17, 2019.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wiki 1 kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Viwanda na Biashara kukamilisha taratibu za uwekezaji kwa kampuni Sugar Investment Trust (SIT) ya Mauritius ambayo imecheleweshwa kuwekeza katika uzalishaji wa sukari tangu mwaka 2017.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo Aprili 17, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo Bw. Gansam Boodram aliyeongozana na Balozi wa Mauritius hapa nchini Mhe. Jean Pierre Jhumun.
Katika mazungumzo hayo Bw. Boodram ameeleza kuwa yupo tayari kulima ekari 25,000 za mashamba ya miwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari na kwamba uwekezaji huo utawezesha kuzalishwa kwa tani 125,000 za sukari, ajira za kudumu 3,000 na ajira za muda 5,000 lakini amekwama kuendelea kutokana na kusubiri majibu ya Serikali kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu upatikanaji wa eneo la uzalishaji wa miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza ufanyike uchambuzi wa haraka katika maeneo ya Bonde la Mto Rufiji Mkoani Pwani, Eneo la shamba la Mkulazi Mkoani Morogoro na eneo la Kibondo Mkoani Kigoma ili mwekezaji huyo apatiwe na kuanza mara moja uwekezaji kwa kuwa nchi inahitaji kuongeza uzalishaji wa sukari utakaomaliza upungufu wa tani zaidi ya 100,000 ambazo kwa sasa zinaagizwa kutoka nje ya nchi.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Edward Mhede kufuatilia makubaliano ya ushirikiano katika uvuvi kati ya Tanzania na Mauritius ambayo hayajatiwa saini tangu mwaka 2017 licha ya wawekezaji wa Mauritius kuonesha nia ya kutaka kuwekeza katika uvuvi na viwanda vya samaki.
Mhe. Balozi Jhumun amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa Mauritius inao uzoefu mkubwa katika uvuvi na viwanda vya samaki na kwamba kwa kuitikia wito wake wa kuhamasisha wawekezaji kuja hapa nchini, amefanikiwa kupata kampuni zilizotayari kufanya uwekezaji huo baada ya makubaliano kati ya Tanzania na Mauritius kutiwa saini.
Mhe. Rais amezionya taasisi za Serikali kikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kutoharakisha taratibu za kuwawezesha wawekezaji kuwekeza na amemhakikishia Mhe. Balozi Jhumun kuwa atafuatilia kuhakikisha uwekezaji wa kampuni ya SIT unafanyika.
“Ndugu zangu watendaji wa Serikali badilikeni, achene kukwamisha wawekezaji, fanyeni maamuzi na kama yanawashinda toeni taarifa kwenye mamlaka za juu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment