Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson Mwansasu akizungumza kwenye mkutano na wakulima wa viazi mviringo katika eneo la Uyole Jijini Mbeya, jana tarehe 5 Machi 2019. Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga.
Na Mathias Canal, Mbeya
WAZIRI wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga kwa pamoja na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Mwansasu wamekubaliana kuvalia njuga kero sugu zinazowakabili wakulima wa viazi mviringo Mkoani Mbeya.
Kero zinazowakabili wakulima hao ni pamoja na faini zisizo rafiki za vifungashio, Ufungaji wa mifuko (zipu) wakati wa kusafirisha usumbufu wa mawakala wa kilimo wakati wa kusafirisha viazi pamoja na sheria ya vipimo kutokuwa rafiki kwani viazi hutofautiana uzito kutokana na msimu.
Kero nyingine ni pamoja na Rushwa kwa baadhi ya watumishi wa viwango hususani katika vituo wakati wa kupima katika vituo vya ukaguzi visivyo rasmi vilivyopo katika eneo la Makambako, Iringa, Morogoro, Mikese na Kibaha.
Katika taarifa iliyosomwa na wakulima hao jana tarehe 5 Machi 2019 mbele ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga pamoja na Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson wakulima hao waliiomba serikali kutatua changamoto hizo ambazo kwa muda mrefu zimekuwa kero bila kupatiwa majibu.
Mhe Hasunga alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kwa dhati kutatua kero zisizo rafiki kwa wakulima na watanzania wote.
“Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu sasa kwenye zao hili muhimu la viazi mviringo nami niwaahidi kutekeleza kwa haraka kadhia hii inayowasumbua Alikaririwa Mhe Hasunga
Kadhalika, aliwaeleza wakulima hao waliojitokeza katika mkutano huo kuwa Wizara yake imejipanga kuhakikisha kuwa wakulima wote nchini wanasajiliwa ili kubaini kiwango cha mashamba wanayolima na uwezo wa uzalishaji wa mazao.
Vilevile alieleza kuwa serikali imeanza mkakati wa kuwa na Bima ya mazao kwani kufanya hivyo wakulima watakuwa na ahueni pindi yanapotokea majanga katika mazao wanayolima.
Naye Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson amewapongeza wakulima hao wa viazi mviringo kwa kuwa wavumilivu wakati serikali inatafuta ufumbuzi wa kadhia hizo zinazowakabili.
Alisema kuwa wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara zitakutana kutatua kadhia hizo ili wakulima mkoani Mbeya na mikoa mingine nchini waweze kuzalisha na kusafirisha mazao yao pasina kadhia yoyote.
No comments:
Post a Comment