Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeupongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kwa kutekeleza miradi wanayoisimamia kwa ubora na kwa gharama nafuu.
Akizungumza mara baada ya kukagua miradi inayojengwa na Wakala huo ikiwemo jengo la ofisi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, pamoja na Jengo la Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Naghenjwa Kaboyoka, amesema kuwa kamati imeridhishwa na kazi zinazofanywa na wakala huo na hivyo kuutaka wakala huo kutobweteka na badala yake kufanya kazi kwa bidii hata kwa miradi mingine wanayoitekeleza.
"Sisi kama Kamati ya PAC kiukweli tumefurahishwa na utekelezaji wa miradi hii tulioikagua, tunawapongeza kwa kufanya kazi nzuri na inayozingatia thamani ya fedha", amesema Mheshimiwa Mwenyekiti.
Amesisitiza kuwa Kamati inapenda kuwatia moyo TBA kwa kuendelea kufanya jitihada katika usimamizi wa miradi iliyonayo ili kuondoa ile dhana iliojengeka ya kwamba kazi zinazotekelezwa na wakala huo zipo chini ya kiwango.
“Tunawapongeza TBA kwa kazi nzuri iliofanyika, baada ya kukagua tumeona kuwa serikali haikufanya makosa kutoa zabuni nyingi za ujenzi kwa TBA”, amesisitiza Mwenyekiti wa Kamati
Aidha, Wakala huo umepongezwa kwa kuweza kutoa fursa kwa wanafunzi walioko na wanaotoka vyuoni kupata mafunzo kwa vitendo ili kuwajengea uwezo ambao utaiwezesha Serikali kupata wataalama zaidi katika taaluma hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, amesema wizara itaendelea kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi kutoka vyuo vikuu ili nao waweze kuja kuwa mchango mkubwa katika kuleta maendeleo nchini kupitia sekta ya ujenzi.
Arch. Mwakalinga, ameahidi kwa Kamati hiyo kuhakikisha kuwa wataendelea kujenga majengo ya Serikali kwa kuzingatia ubora na kwa gharama nafuu.
Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daudi Kondoro, amefafanua kuwa jengo la Ofisi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano linalojengwa hivi sasa katika mtaa wa Moshi jijini Dodoma lina ghorofa tatu zenye jumla ya vyumba 84 zikiwemo ofisi za viongozi 15 zenye maliwato ndani, maafisa waandamizi 5, Ofisi za wazi 17, masijala 3, Makatibu Muhtasi 14, vyumba vya chai 4, stoo 3, vyoo 22 na vyoo vya watu wenye mahitaji maalum.
Ameongeza kuwa mradi wa ujenzi wa ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora katika Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma umefika asilimia 97 ambapo amesema kuwa kazi zinazofanyika kwa sasa ni kukamilisha kazi ya madirisha, milango ya nje ya jengo pamoja na kukagua na kurekebisha dosari zilizojitokeza wakati wa ujenzi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi)
No comments:
Post a Comment