KATIKA kuadhimisha wiki ya wanawake
duniani, wafanyazi wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania Plc, kupitia
mpango wake wa Pamoja na Vodacom ulio chini ya taasisi ya Vodacom Tanzania
Foundation leo wamechangia vifaa mbali mbali vyenye thamani ya shilingi milioni
9.6 kwa kituo cha watoto wenye uhitaji maalum kiitwacho Mwanangu Special
kilichopo Mkuranga, mkoani Pwani. Kituo hicho kina jumla ya watoto 40, kati yao
20 ni wale wenye mahitaji maalum kama vile mgongo wazi, vichwa vikubwa na down
syndrome.
Wafanyakazi hao wametoa vifaa kama
vile; viti maalum, magongo ya kutembelea, magongo ya kusimamia, mashine za
uzito, viatu vya ‘Special Orthopedics’, vitanda vya watoto walemavu, mashine za
kufulia nk. ambavyo ni mahitaji muhimu kwa watoto hao. Mbali na misaada hiyo,
wafanyakazi wa Vodacom pia walijitolea muda wao kucheza na kufurahi pamoja na
watoto hao kwa ajili ya kuwapatia faraja.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bw.
Filberto Sanga aliipongeza kampuni ya Vodacom kwa mpango huo akisema “Serikali
yetu imedhamiria kuboresha maisha ya kila mtanzania ili kutimiza dira ya
maendeleo ya taifa na jitihada kama hizi kutoka kampuni binafsi zinasaidia
serikali kutimiza malengo yake”. Bw. Sanga pia aliishukuru kampuni ya Vodacom
huku akifafanua namna ambavyo msaada huo utasaidia kuhudumia watoto wenye
ulemavu nchini na kuhimiza taasisi zingine kufuata nyayo za Vodacom.
Mpango wa Pamoja na Vodacom umekuwa
ukitumiwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo ili kurejesha fadhila kwa jamii.
Mpango huu umewafanya wafanyakazi wa kampuni hiyo kuwa mawakala wa mabadiliko
kwa kusaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Akizungumza wakati wa makabidhiano,
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Bi Jacquiline
Materu alisema “Wafanyakazi wa Vodacom, tunashauku ya kuisaidia jamii yetu na
huu umekuwa ni utaratibu wetu kwa miaka zaidi ya 12 kupitia Vodacom Tanzania
Foundation. Katika kusherehekea wiki hii ya wanawake duniani, tumeona ni vyema
kusherehekea na wadogo zetu, kuwapatia mahitaji muhimu na pia kuwawezesha kuwa
na nyenzo muhimu za kuwasaidia kufikia ndoto zao kwani ulemavu sio kikwazo cha
mafanikio”.
No comments:
Post a Comment