Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akifunga Mkutano wa 26 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Mwanza. |
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu amewataka wananchi kuwachukulia askari wa Wanyamapori na Misitu kama rafiki wa umma na watendaji waliotumwa na Serikali kulinda rasilimali hizo kwa niaba yao.
Akifunga kikao cha 26 cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo jijini Mwanza, Mhe. Kanyasu amesema Askari hao waliopewa dhamana ya kulinda maeneo ya hifadhi nchini wanafanya kazi nzuri ya kuifanya Tanzania iendelee kuwa na maeneo mazuri yaliyohifadhiwa.
Amesema Askari hao wameajiriwa kwa mujibu wa sheria hivyo hutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya kazi zao na pale wanapokiuka sheria mamlaka zinazohusika huwachukulia hatua.
“Sisi kama Wizara tunaamini kwamba askari wetu na wahifadhi wetu wanafanya kazi nzuri, pale ambapo wamekuwa wakilaumiwa kwa kuwapiga na kuwanyanyasa watu kwa namna yoyote ile tumetuma Tume maalum kuchunguza na kuchukua hatua” Amesema.
Mhe, Kanyasu amesema uchunguzi unapofanyika na ikathibitika kuwa tukio lililofanyika halikuongozwa na matumizi ya sheria na kuwepo kwa haki wizara imekua ikichukua hatua.
Ameeeleza kuwa askari wanaolinda Hifadhi nchini wanategemewa na bila wao hakuna uhifadhi unaoweza kuendelea nchini akibainisha kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakipinga juhudi za uhifadhi kwa kuwatetea watu wanaovunja sheria.
“Watu hawafahamu tu, tukiwaondoa askari wetu wote katika maeneo ya hifadhi na tukawaondoa Maafisa ukaguzi wa mazao ya Misitu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) barabarani, katika kipindi cha miezi 6 nchi hii itageuka kuwa jangwa” Amesisitiza Mhe. Kanyasu.
Amesema yapo madhara makubwa yanayoweza kutokea kama hakutakuwa na uhifadhi imara ikiwemo maeneo mengi ya nchi kugeuka kuwa jangwa kutokana na uharibifu wa misitu, ukosefu wa mvua, ukosefu wa maji, chakula na ukosefu wa hewa safi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa kumekuwa na tuhuma za vitendo vya ukatili dhidi ya raia vinavyofanywa na baadhi ya askari wa Hifadhi nchini na kutoa wito kwa wananchi wote wenye ushahidi na taarifa juu ya vitendo hivyo kuziwasilisha ili hatua stahiki zichukuliwe.
Amesisitiza kuwa Serikali hairuhusu askari kufanya vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya raia badala yake imekua ikiwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa rasilimali zinazowazunguka.
Amewatahadharisha na kuwataka wananchi wawe makini dhidi ya kampeni zenye nia ovu zinazoendeshwa na baadhi ya watu zenye lengo la kuwavunja moyo askari wanaojitolea maisha yao kulinda rasilimali za taifa akieleza kuwa wapo askari waliopata madhara makubwa na kupoteza maisha kwa kushambuliwa na majangili kwa kuchomwa mishale yenye sumu na kukatwa vidole wakati wakitimiza wajibu wao.
Prof. Mkenda amesema kuwa wizara itaendelea kulinda hadhi ya vijana hao waliojitolea maisha yao kulinda rasilimali za Taifa akibainisha kuwa Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria watakaokiuka kanuni na taratibu za kazi kazi ili iwe fundisho kwa wengine.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo amesema kuwa watumishi 23 wa wanyamapori na misitu wamepoteza maisha na wengine saba kujeruhiwa katika matukio tofauti yaliyotokea wakati wakipambana na majangili.
Amesema matukio hayo yametokea mwaka 2018/2019 na hifadhi inayoongoza kwa matukio hayo ni Sengereti, Prof. Mkenda amesema kuwa watumishi hao waliofariki na wengine kujeruhiwa walikuwa wakitimiza wajibu wao wa kazi hivyo Wizara inaangalia namna ya kuwaenzi kutokana na mchango wao.
No comments:
Post a Comment